MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Mei 9, 2022 kuanza kusikiliza kesi ya kukutwa na nyara za serikali dhidi ya watuhumiwa 11 wakitanzania na raia mmoja wa Guinea baada ya upelelezi dhidi ya kesi hiyo kukamilika na washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Washtakiwa hao ni Ally Ganzuuu Sharifu raia wa Guinea, Victor Mawala, Haruni Kassa, Abbas Hassan, Solomoni Mtenya, Musa Ligagabile, Khalfani Kihengele, Ismail Kassa, Kassim Saidi, Peter Nyachiwa, John Buhanza na Mussa Abdallah.
Mapema wakili wa Serikali, Candid Nasua alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo leo ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Akisoma maelezo hayo mbele ya Hakimu mkazi Mwandamizi Roda Ngimilanga, Nasua amedai, washtakiwa hao ambao ni wafanyabiashara wanadaiwa, kati ya Aprili Mosi 2016 na Juni 24, 2016, Polisi walipata taarifa za kiuchunguzi kuwa kuna mtandao mkubwa wa uhalifu wa nyama pori ambao walikuwa wanauza, wananunua, wanapokea, kuhamisha na kusafirisha nyara za serikali ambazo ni meno ya tembo.
Imedaiwa, wakiwa wanakaribia kusafirisha idadi kubwa ya meno ya tembo kutoka Tanzania, Juni 22, 2016 huko katika eneo la Maduka mawili Chang'ombe, askari walifanikiwa kuwakamata washtakiwa Haruni Kassa, Kihengele na Kassa.
Amedai upekuzi ulifanyika nyumbani kwa mshtakiwa Haruni Kassa kwa kusaidiana na mbwa maalum wa ukaguzi wa meno ya tembo ambapo walikuta chumbani shuka jeupe lililodariziwa likiwa limefunika silaha aina ya shotgun, risasi tano na simu mbili huku kwa mshtakiwa Abdallah anayeishi maeneo ya Mwanagati, walikuta begi la bluu lililokoza likiwa na meno ya tembo.
Imeendelea kudaiwa kuwa, Juni 23, 2016, mshtakiwa Haruni Kassa, aliongoza polisi kwenda kumkamata mshtakiwa Hassan ambaye katika upekuzi alikutwa na simu sita, laptop mbili, magari matatu na matairi 170 ya pikipiki.
Mshtakiwa wanne anadaiwa kuwapeleka polisi kumkamata Juma Baguma ambaye kwa sasa ni Marehemu ambapo alimtaja mtu maarufu wa ununuzi wa meno ya tembo anayeishi nje ya nchi huku pia Akiwaongoza kumkamata mshtakiwa Anguzuu ambaye katika upekuzi huko nyumbani kwake Tabata Segerea, uliofanywa na askari pamoja na mbwa maalumu wa kunusa walikamata gari aina ya Isuzu Canter ambalo baada ya Mbwa huyo kunusa na gari kufunguliwa mlango, walikuta mashine za kupimia uzito mbili na katika bodi ya gari walitengeneza sehemu maalum ya kuhifadhia meno ya tembo.
Aidha askari pia walilikamata gari lingine aina ya Mitsubishi iliyokuwa ikitumika kusafirisha meno hayo.
Inadaiwa wakati wakiendelea na upekuzi, simu ya marehemu Baguma iliita aliamliwa kupokea ndipo katika maongezi yao alikuwa amepigiwa simu na mshtakiwa Mtenya akimtaka yeye na mshtakiwa Hasaan wakaonane Kimara Stop Over ili awauzie meno ya tembo.
Baguma aliongozana na Polisi hadi Kimara ndipo mshtakiwa Mtenya na Ligagabile walipokamatwa na katika upekuzi walikutwa na vipande sita vya meno ya Tembo katika gari, Toyota Fancago yenye namba za usajili T540 DDS.
Pia inadaiwa polisi wakiongozana na Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa walikwenda nyumbani kwa mshtakiwa Anguzuu ambapo walivunja mlango na kwa msaada wa mbwa wa kunusa walifanikiwa kukuta vipande 660 vya meno ya tembo kwenye viroba, vyenye thamani ya USD 12,145,000 ambazo ni sawa na Sh 4, 656,795,000 na USD 5652 ambazo sawa na Sh 12,270,492 na mashine za kupimia uzito.
Imedaiwa washtakiwa wakati wakihojiwa walikiri kufanya biashara hiyo haramu kwa muda mrefu, mshtakiwa wa kwanza alikubali kutumia gari iliyotengenezwa maalum kwa kuhifadhia meno ya tembo wakati wakisafirisha kuyapeleka kwenye stoo yao iliyopo Mbezi Msakuzi.
Aidha washtakiwa wakihojiwa mahakamani hapo wamekubali taarifa zao binafsi lakini wamekana kuhusika kutenda makosa hayo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 9, mwaka huu.
Toa Maoni Yako:
0 comments: