Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (kulia) akieleza jambo alipofanya ziara na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa lengo la kukagua mradi huo Wilaya ya Meru, Mkoani Arusha. Kushoto ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Asha Abdalla.
Sehemu ya vijana wakisikiliza maelezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (hayupo pichani) walipotembelea mradi wa kitalu nyumba kwa lengo la kukagua maendeleo ya mafunzo waliyopatiwa kupitia teknolojia ya kilimo cha kisasa cha Kitalu Nyumba (Greenhouse) Machi 19, 2022 Meru, Mkoani Arusha.
Kiongozi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Adam Mwakasaka (wa kwanza kulia) akieleza jambo wakati wa ziara hiyo. Wa pili kutoka kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako.
Katibu mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu) Prof. Jamal Katundu akifafanua jambo wakati wa ziara hiyo ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipotembelea mradi wa kitalu nyumba Wilaya ya Meru, Mkoani Arusha
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akiwa ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipotembelea mradi wa kitalu nyumba Wilaya ya Meru, Mkoani Arusha.
Mnufaika wa Mafunzo Bw. Pendael Mollel (kushoto) akieleza jambo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (wa pili kutoka kulia) pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipotembelea mradi wa kitalu nyumba Wilaya ya Meru, Mkoani Arusha. Wa pili kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Zainab Makwinya.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza jambo na kijana mwenye ulemavu Bw. Marko Palanjo mnufaika wa mafunzo hayo ya kilimo cha kisasa kwa utumia teknolojia ya kitalu nyumba yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
Na Mwandishi wetu - ARUSHA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutoa fursa kwa vijana nchini ili waweze kuondokana na changamoto ya ajira.
Waziri Ndalichako ameyasema hayo Machi 19, 2022 alipoambatana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipotembelea mradi wa Kitalu Nyumba (Greenhouse) katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru kwa lengo la kukagua maendeleo ya mafunzo hayo ya kilimo cha kisasa yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Amesema kuwa, katika kufanikisha hilo Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikiratibu Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ambayo imelenga kuwezesha nguvu kazi ya Taifa kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki ili kumudu ushindani wa soko la ajira na kuwawezesha kujiajiri au kuajiri wenzao.
“Mheshimiwa Rais amedhamiria kutoa fursa zaidi kwa vijana nchini na serikali anayoiongoza imekuwa ikiwapatia vijana fursa mbalimbali ikiwemo ujuzi na stadi za kazi ili waweze kushiriki kwa ufanisi katika shughuli za uzalishaji mali sambamba na kuongeza fursa za ajira,” alisema Waziri Ndalichako
Aliongeza kuwa, Serikali imetenga shilingi bilioni 9 kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kupitia mafunzo ya uanagenzi, mafunzo ya utarajali (Internship Training), mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana katika mfumo usio rasmi wa mafunzo na mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia kitalu nyumba (Greenhouse Farming Training).
Akizungumzia mafunzo hayo ya Kilimo cha Kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba, alisema kuwa zaidi ya vijana 702 kutoka katika halmashauri 7 mkoani Arusha wamenufaika na mafunzo hayo ambapo vijana hao wamepatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo ya ujenzi wa kitalu nyumba pamoja na kilimo ndani ya kitalu nyumba (Greenhouse).
Aidha, Waziri Ndalichako alitoa wito kwa Viongozi wa Halmashauri kuhakikisha wanatekeleza maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kuwezesha vijana vitendea kazi kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani (4% Vijana, 4% Wanawake na 2% Watu wenye Ulemavu) ili kuwawezesha vijana hao kufanya kazi au shughuli zenye tija.
Sambamba na hayo, amewataka vijana kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali yao ili waweze kunufaika pamoja na kushiriki katika kusukuma gurudumu la maendeleo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Adam Mwakasaka alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kushirikiana na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikipitisha bajeti kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa programu hiyo ili kuwezesha nguvu kazi ujuzi unaotakiwa katika soko la ajira.
Naye Katibu mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu) Prof. Jamal Katundu alisema kuwa ujuzi huo waliopatiwa vijana kwa ufadhili wa serikali yao umekuwa ni chachu ya kuwawezesha wajiajiri katika sekta ya kilimo.
Hali Kadhalika alielezea mipango ya ofisi hiyo namna ilivyojipanga kuongeza wigo wa mafunzo hayo ili kuwafikia vijana katika maeneo mbalimbali ya nchini.
Akitoa neno la shukrani mnufaika wa mafunzo hayo, Bi. Mariam Juma alishukuru serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamewapa hamasa vijana wengi wa mkoa huo kutambua manufaa yaliyopo kwenye kilimo hicho, waliahidi kuendeleza ujuzi huo kwa wananchi ili uwasaidie kuwakomboa kiuchumi.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wetu sisi vijana hakika hatuta muangusha, tutatumia ujuzi tuliopata kujikomboa kiuchumi,” alisema
Toa Maoni Yako:
0 comments: