WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu Wilaya na Watendaji wa Kata waweke utaratibu wa kusikiliza na kutatua kero za migogoro ya ardhi katika maeneo yao badala ya kusubiri viongozi wa kitaifa au Mawaziri.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Februari 10, 2022) Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbeya Vijijini, Mheshimiwa Oran Njeza aliyetaka kujua ni lini Kamati ya mawaziri itarejea kukamilisha migogoro kati ya wananchi na TANAPA na TFS kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

“Nitoe wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu Wilaya na Watendaji wa Kata na viongozi wote kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa wafike maeneo hayo. Natambua kuna migogoro ya mipaka kati ya vijiji na vijiji, pia ipo ya wafugaji na wakulima, hakikini migogoro hii na muikamilishe hukuhuko badala ya kusuburi Mawaziri wasafiri kuja huko, kila mmoja akiwajibika migogoro hii itapungua kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu ameiagiza kamati ya Mawaziri nane iliyoundwa kwa ajili ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi kuweka mpango kazi wa kwenda Mbeya Vijijini wakaangalie aina ya migogoro iliyopo na nini kifanyike baada ya kuhakiki.

Akijibu swali la Mheshimiwa Leah Komanya aliyetaka kujua mkakati wa Serikali katika kukabiliana na ukame hasa kwenye eneo la malisho ya mifugo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi ikiwemo misitu ili isaidie kuleta mvua na kukabiliana na ukame.

“Kutokana na ukame hatuwezi kupata malisho, hivyo ni lazima tuhifadhi mazingira ili malisho yapatikane, pia wizara ya mifugo inatoa elimu kwa wafugaji ikiwemo kuwaeleza kuwa wafuge kitaalam kulingana na ukubwa wa malisho waliyo nayo ili kukabiliana upungufu wa malisho unaotokana na uwepo wa mifugo mingi.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania waache tabia ya kukata miti katika maeneo yao ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na ukame ili misitu hiyo iweze kusaidia kupatikana kwa mvua za kutosha. “Ndugu zangu wafugaji endeleeni kufuga kitaalamu, kuweni na mifugo michache mnayoweza kuihudumia badala ya kuwa mifugo mingi msiyoweza kuimudu.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itachukua hatua kali za kisheria kwa baadhi ya wafanyabishara wanaoweka mkakati wa kusumbua jamii kwa kuuza bidhaa kwa bei ya juu. “Serikali tunaweka mazingira rafiki ya uwekezaji lengo ni kusaidia upatikanaji wa bidhaa kwa wingi, bei nafuu na wakati wote, na tutaendelea kulifanyika kazi hili kupitia taasisi zetu za Serikali”

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa watanzania kuendelea kudumisha amani na usalama ili kuwawezesha wenye nia ya kufanya biashara wakati wowote ikiwemo nyakati za usiku kufanya hivyo. “Malengo yetu ni kuboresha uchumi wa nchi, kama nchi haipo salama hatuwezi kufikia malengo.”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: