Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akipokea zawadi kutoka kwa Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa Nchini (UN- WFP), Bi. Sarah Gordon- Gibson, alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma.


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa katika picha ya pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa Nchini (UN- WFP), Bi. Sarah Gordon- Gibson, (katikati), baada ya mazungumzo baina yao, jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Shaaban, kushoto ni Mratibu wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa Nchini (UN- WFP), Bi. Neema Nina Sitta na Kamishana Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Sauda Msemo.


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akisalimiana na Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa Nchini (UN- WFP), Bi. Sarah Gordon- Gibson, alipomtembelea kwa mazungumzo ofisini kwake jijini Dodoma.


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akizungumza wakati wa kikao na Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa Nchini (UN- WFP), Bi. Sarah Gordon- Gibson, (Hayumo pichani) alipomtembelea kwa mazungumzo ofisini kwake jijini Dodoma. Kulia ni Kamishna Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Sauda Msemo na Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Shaaban.


Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa Nchini (UN- WFP), Bi. Sarah Gordon- Gibson, akizungumza wakati alipomtembelea Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (Hayumo pichani), kushoto ni Mratibu wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa Nchini (UN- WFP), Bi. Neema Nina Sitta jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)

Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Dodoma

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameliomba Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP), kununua shehena ya nafaka kutoka kwa wakulima hapa nchini kwa ajili ya matumizi yake ya kulisha wakimbizi maeneo mbalimbali wanayoyahudumia.

Dkt. Nchemba ametoa wito huo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika hilo Bi. Sarah Gibson, ambapo wawili hao wamejadiliana masuala kadhaa ya ushirikiano kati ya Serikali na Shirika hilo la Mpango wa Chakula Duniani.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka 6 kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2021, Tanzania imezalisha ziada ya chakula kiasi cha tani milioni 17.8 na kwamba ukosefu wa soko la mazao hayo ya kilimo unakwamisha juhudi za wakulima kujikwamua kiuchumi.

Dkt. Nchemba aliliomba Shirika hilo la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kusaidia upatikanaji wa masoko na fedha kwa ajili ya kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji kutakako iwezesha nchi kuzalisha chakula kwa wingi na kuwezesha Tanzania kuwa ghala la chakula.

“Rai ya Wizara na Serikali kwa ujumla ni kuendelea kushirikiana katika maeneo ambayo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ameyawekea kipaumbele ya kutafuta masoko ya bidhaa za wakulima wetu kwahiyo WFP na maeneo mnayoyahudumia mnaweza kusaidia kupata masoko ili wakulima waweze kunufaika na uzalishaji wao” Alisema Dkt. Nchemba.

Alilipongeza Shirika hilo kwa juhudi zake za kuisaidia Tanzania kukabiliana na changamoto ya utapiamlo kwa watoto na kuliomba kuendelea kusaidia eneo hilo kwa kuleta mawazo yenye ubunifu wa namna ya kukomesha tatizo hilo nchini.

Aidha, Dkt. Nchemba aliliomba Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa kuiwezesha Serikali kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi itakayosaidia kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP), Bi. Sarah Gibson, alisema kuwa msimu huu, Shirika lake limenunua tani 76,000 za chakula nchini Tanzania kwa gharama ya dola za Marekani milioni 25 na kuzisambaza kwenye maeneo yenye uhitaji.

“Katika kipindi hicho pia tumetumia kiasi cha dola za Marekani milioni 19 kwa ajili ya kuboresha shughuli za uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusafirisha chakula kinachopelekwa kwenye maeneo yenye uhitaji hususan maeneo ya wakimbizi” alisema Bi. Gibson

Alidokeza kuwa Shirika lake limepanga kutumia zaidi ya dola za Marekani milioni 336 kwa ajili ya kuendesha shughuli zake katika kipindi cha miaka mitano ijayo kuanzia Mwaka 2022 hadi mwaka 2027 ambapo wanatarajia kuwafikia zaidi ya watu milioni moja.

Bi. Sarah Gibson alisema pia kuwa Shirika lake limepanga kurejesha huduma ya chakula mashuleni hapa nchini baada ya kusitisha huduma hiyo miaka michache iliyopita kutokana na umuhimu wa chakula kwa watoto wakiwa shuleni

“Pia tumepanga kuanzisha mpango wa kuwasaidia watu kupata fedha taslimu kwa njia ya kushiriki kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali katika maeneo yao ikiwemo miradi ya kilimo, ujenzi wa miundombinu pamoja na kuwapatia mikopo midogo midogo pamoja na masoko ya uhakika wakulima wadogo wadogo” alisema Bi. Gibson
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: