Samwel Shelukindo, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye UNESCO, akiwa kwenye picha ya pamoja na Prof. Hamisi Malebo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO (kulia) na Balozi Macocha M. Tembele, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa (kushoto) wakiwa kwenye Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Na Mwandishi Wetu, Ufaransa
JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imechaguliwa kuwa mjumbe wa Bodi Tendaji ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kipindi cha mwaka 2021-2025; kwenye Mkutano Mkuu wa 41 wa UNESCO unaoendelea Paris, Ufaransa.
Kwenye uchaguzi huo, uliofanyika Novemba 17,2021 , Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepata kura 160 kati ya 178 zilizopigwa na nchi wanachama. Nchi zingine zilizochaguliwa kutoka kundi la Afrika kuhudumu kwenye bodi hiyo ni Angola, Botswana, Djibouti, Afrika Kusini na Congo.
Pamoja na masuala mengine, Bodi Tendaji inahusika na usimamizi wa utekelezaji wa bajeti ya Shirika kupitia miradi mbalimbali itakayopendekezwa. Hivyo nafasi hiyo itakuwa ni fursa ya kushiriki katika maamuzi ya Shirika hilo kwa kuzingatia mahitaji ya kundi la nchi zinazoendelea.
Toa Maoni Yako:
0 comments: