Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, akizungumza na viongozi wa ngazi za mikoa, wilaya na Idara mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kikao chake cha Tathmini ya Ziara ya Siku mbili katika maeneo ya kimazingira yaliyoathirika na mabadiliko ya tabianchi na maeneo ya kiafya, kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo, Wawi Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, Tarehe 24/11/2021.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Othman Masoud Othman, akitoa maelekezo kwa viongozi wa Hospitali ya Vitongoji wakiongozwa na Dokta Sharif Hamad Khatib (kulia) akiwa na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui katika muendelezo wa ziara yake ya kimazingira na Afya kisiwani Pemba, Tarehe 24/11/2021.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,Mhe.Othman Masoud Othman,akipokea maelezo kutoka kwa Mganga mkuu mfawidhi wa Hospitali ya Vitongoji Wilaya ya Chake chake Mkoa wa Kusini Pemba, Dokta Sharif Hamad Khatib, juu ya mazingira na changamoto za hospitali hio akiwa katika muendelezo wa ziara yake kisiwani Pemba, Tarehe,24/11/2021.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Othman Masoud Othman, akisalimiana na viongozi mbalimbali wa kiserikali na kichama mara baada ya kuwasili katika Hospitali ya Vitongoji iliyopo Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba, katika muendelezo wa ziara yake Kisiwani humo, Tarehe 24/11/2021.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema kunahitajika uelewa mkubwa wa watu wote katika suala la mazingira ambalo ni uhai na linalogusa sekta zote za uzalishaji na maendeleo nchini.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo akiongoza Kikao cha Majumuisho ya Ziara yake ya Siku mbili ya kimazingira na afya kisiwani hapa, kilichofanyika katika Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo, Wawi Wilaya ya Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.

Amesema hakuna nyanja yoyote ya maisha, sekta ya maendeleo au wizara ya serikali, ambayo kwa namna moja au nyingine haitoguswa na suala la mazingira, bali kilichozoeleka katika jamii ni kulichukulia kwa wepesi na mtazamo wa juujuu.

Mheshimiwa Othman ametoa wito kwa wadau wote kujumuika katika kuungamkono juhudi za kukabiliana na athari za mazingira zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, zikiwemo upandaji wa mikoko na kuepuka ukataji wa miti ya asili kiholela.

“Katika tishio kubwa ambalo linalotishia mazingira ni ardhi yetu ambayo ni chache, kuvamiwa na maji ya bahari bali la msingi kwa sasa ni kuweka mikakati na sisi kuiendea bahari ingawa kwa kufuata miongozo ya kitaalamu”, amesema Mheshimiwa Othman.

Mheshimiwa Othman ametoa wito kwa mamlaka zinazohusika kuweka miongozo, taratibu, kuzingatia haki za wananchi na mbinu mbadala za kuepusha uharibifu wa makusudi wa mazingira katika maeneo mbali mbali yakiwemo machimbo ya mawe na mchanga ya Micheweni, Pujini na Shumba Viamboni, ili kuyafanyia kazi malalamiko na kuepuka visingizio vikiwemo vya ukosefu wa ajira.

Kabla ya kikao hicho Mheshimiwa Othman ametembelea Hospitali ya Vitongoji ‘Cottage’ sambamba na kukagua Bohari Kuu ya Dawa kisiwani Pemba, ambapo ameeleza matumaini yaliyopo kutokana na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na moyo wa kujitolea wa watumishi mbali mbali wa Wizara ya Afya wakiwemo madaktari, katika kuwapatia wananchi huduma bora za afya licha ya changamoto nyingi zinazowakabili.

Mheshimiwa Othman amesema pamoja na juhudi zote, maendeleo hayatowezekana katika visiwa vya Unguja na Pemba na Tanzania kwa ujumla, bila ya kuwepo misingi mikubwa ya kuwavutia wawekezaji, ambayo ni pamoja na amani, utulivu, umoja na mshikamano, bali amewaasa viongozi na wananchi wote kuielewa dhima ya kuyalinda maridhiano ya kisiasa, chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, kwaajili ya mustakabali mwema wa nchi.

Naye Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui, ameeleza juhudi za makusudi za Serikali kuwapatia wananchi huduma bora za afya kwa ufanisi ambazo ni pamoja na ujenzi wa Jengo kubwa linalotarajia kuwahudumia wagonjwa takriban 200 kwa wakati mmoja, katika Hospitali ya Vitongoji, Wilaya ya Chake Chake Pemba, ambayo maandalizi yake yamekamilika.

Aidha Daktari dhamana wa Hospitali hiyo, Dokta Sharif Hamad Khatib, ameeleza changamoto kubwa zinazowabili katika kuwapatia wananchi huduma bora za afya hospitalini hapo, zikiwemo uhaba wa eneo la kutosha la kuwahudumia wazazi na wajawazito wanaofika kwaajili ya kujifungua.

Kikao hicho cha tathmini kimewajumuisha Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bi Salama Mbarouk Khatib, Wakuu wa Wilaya zote nne kisiwani hapa, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dokta Omar Dadi Shajak, Wakurungezi, Maafisa Wadhamini, Wakuu wa Idara Maalum za Serikali, Watendaji, Maafisa na Watumishi wa Wizara mbali mbali za Serikali, Wabunge, Wawakilishi na Viongozi mbali mbali wa kijamii na vyama vya siasa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: