Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Umoja wa Afrika umefunguliwa leo jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo pamoja na mambo mengine, Mawaziri watapitia Andiko na mikakati ya utekelezaji wa kaulimbiu ya Mwaka 2022 ya “Lishe na Usalama wa Chakula barani Afrika”. Kaulimbiu hiyo inalenga kusisitiza umuhimu wa lishe bora kwa ajili ya ukuaji na ustawi wa watoto barani Afrika, bara ambalo kwa miaka mingi limekuwa linakabiliwa na uzalishaji mdogo wa chakula. Hivyo, nchi za Afrika zinashauriwa kutekeleza mapendekezo ya Progarmu ya Afrika ya Maendeleo ya Kilimo na Azimio la Malabo kuhusu kilimo ili kuondokana na changamoto ya lishe duni.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo na katika mijadala yake, pamoja na mambo mengine, anatarajiwa kusisitiza umuhimu wa kukifanya Kiswahili kuwa moja ya lugha ya kazi katika Umoja wa Afrika.

Mhe. Mulamula atakumbusha suala hilo kwa sababu limeainishwa katika kaulimbiu ya mwaka 2021 ambayo pamoja na mambo mengine, imehimiza matumizi ya lugha za kiafrika na Kiswahili ni moja ya lugha hizo ambayo inakuwa kwa kasi na kuzungumzwa na watu wengi barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Aidha, Waheshimiwa Mawaziri watapokea taarifa kuhusu ugonjwa wa UVIKO-19 ambapo katika hotuba ya ufunguzi ya Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo alisistiza umuhimu wa nchi wanachama kuzingatia tahadhari za maambukizi ya UVIKO-19 ikiwa ni pamoja na kuhamasisha watu wao kupata chanjo ya ugonjwa huo, huku jitihada zikiendelea kuhakikisha kuwa nchi za Afrika zinapata idadi ya kutosha ya chanjo kwa ajili ya watu wake.

Katika Mkutano huo pia, Mawaziri wa Mambo ya Nje watapitia na kupitisha bajeti ya Mwaka 2022 ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika na kufanya uchaguzi wa nafasi mbalimbali za uongozi, zikiwemo makamishna wawili wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Rais na Makamu wa Rais wa Chuo Kikuu cha Pan Africa, wajumbe wanne wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na wajumbe wanne wa Bodi ya Ushauri ya Afrika ya Kupambana na Rushwa.

Vile vile, Mkutano wa 39 wa Mawaziri utapitia na kupitisha miundo ya taasisi saba za Umoja wa Afrika, ukiwemo muundo wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara barani Afrika ambalo Tanzania imeridhia Mkataba wake hivi karibuni. Kupitishwa kwa miundo hiyo itakuwa ni fursa zikiwemo za ajira kwa nchi wanachama, hivyo, Balozi Mulamula amewataka Watanzania kuzichangamkia, pindi zitakapotangazwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: