Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu.
Na Mwandishi Wetu,
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeitaka jamii kuendelea kubeba jukumu la kutokuyafumbia macho matukio yote yenye kutweza utu wa mwanamke na kutoa taarifa katika mamlaka husika pindi wanaposhuhudia matukio hayo.
Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu katika taarifa yake kwa Vyombo vya Habari ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Jaji Mwaimu alisema kuwa ni vyema jamii ikaendelea kuhamasishana kuacha mitazamo potofu ya kumchukulia mwanamke kama chombo dhaifu kisichoweza kuleta matokeo chanya ya uongozi ili kujenga jamii yenye usawa.
“Kupitia jitihada mbalimbali za uhamasishaji zilizofanyika nchini kumekuwepo na ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi kwenye vyama vya siasa, Serikali, Bunge, Mahakama na katika nafasi nyingine za uongozi katika jamii,’” alisema Mwaimu
Aliongeza kuwa pamoja na jitihada mbalimbali za Serikali za kukemea vitendo vya ukatili kwa wanawake bado kumekuwepo na changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake katika kuwania nafasi za uongozi zikiwemo mila na desturi zinazominya haki za wanawake, elimu na kipato duni kwa wanawake wenye nia ya kugombea uongozi na kutojiamini.
Mwaimu aliendelea kusema kwa kuwa Serikali imeridhia mikataba na matamko mbalimbali ya Kimataifa inayotoa haki kwa kila mtu kushiriki katika nafasi ya uongozi na utawala wa nchi kwa usawa wa kijinsia, Tume inaunga mkono dhamira hiyo ya Serikali na kuwahamasisha wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
“Tume kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikiwahimiza wanawake kuendelea kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi za kijiji/mtaa hadi taifa na kuwajengea uwezo wa namna ya kudai haki zao kisheria pale wanapohisi haki hizo kuvunjwa,” alifafanua Mwaimu.
“Hivyo katika maadhimisho ya siku hii muhimu, Tume inaungana na jamii na wadau mbalimbali duniani kutambua mchango wa wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo,” aliongeza.
Jaji Mwaimu alisema kuwa kupitia Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu 2021 ambayo ni ‘Wanawake katika Uongozi: Chachu kufikia Dunia yenye Usawa’, Tume inaihamasisha jamii yote kuendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha kwamba ushiriki wa wanawake katika uongozi unaongezeka ili kufikia dunia yenye usawa.
Toa Maoni Yako:
0 comments: