Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiangalia mkorosho uliopandwa katika shamba la pamoja la koshoro la Masigati Wilayani Manyoni alipotembelea shamba hilo hivi karibuni
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi (mwenye koti jeusi) akitoa maelezo ya shamba la
pamoja la Korosho la Masigati Manyoni kwa kundi la wanachuo na wakufunzi wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa waliotembelea shamba hilo. Mwenye shati la kitenge ni Luteni Kanali RG Magemeson, Mshauri wa Jeshi la Akiba Mkoa wa Singida, anayefuata ni Mkufunzi, Mheshimiwa Balozi Peter Kallaghe. Kushoto kwa Mkuu wa Mkoa ni Brigadia Generali Liv Jian Mkufunzi wa chuo hicho.
Picha ya pamoja baina ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi mwenye kilemba na kikosi cha wakufunzi na wanachuo cha Ulinzi cha Taifa walipotembelea shamba la kilimo cha pamoja cha korosho wilayani Manyoni hivi karibuni.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi (mwenye koti jeusi) akiwa pamoja kundi la wanachuo na wakufunzi wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa wakikagua shamba la kilimo cha pamoja la Korosho eneo la Masigati Manyoni.
Mshauri wa Jeshi la Akiba Mkoa wa Singida, Luteni Kanali RG Magemeson (mwenye shati la kitenge), akipokea zawadi ya kiwekeo cha funguo kutoka kwa Mkuu wa msafara na Mkufunzi wa chuo hicho, Mhe. Balozi Peter Kallaghe baada ya kufanya kazi nzuri ya kuratibu ziara hiyo wakiwa kwenye Mkoa wa Singida.
Na John Mapepele
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amesema uanzishaji wa mpango wa kilimo cha pamoja (block farming) kwenye zaidi ya ekari 12000 wa zao la korosho eneo la Masigati mkoani Singida umefanya eneo hili kuwa miongoni mwa kivutio kikubwa cha utalii wa kilimo duniani utakaochangia katika uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa kuwaaga wanachuo wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa waliotembelea mradi wa shamba la kilimo cha pamoja cha Korosho Masigati wilayani Manyoni leo, Dkt Nchimbi alisema Mkoa wa Singida unaendelea kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kupitia mkakati wa kuwainua wananchi wote baada ya kubuni kilimo cha pamoja ambapo alisema lengo ni kila mwananchi apate angalau ekari kuanzia tano.
“Katika kipindi hiki cha takribani miaka miwili tunashukuru Mungu kuwa tumeleta mabadiliko makubwa ya kitabia na kifikra kwa wananchi wetu kupitia mradi huu ambao wengi wao wameendelea kujiunga siku hadi siku na kufurahia utajiri ardhi yao” alisitiza Dkt Nchimbi
Alisema licha ya kupata ekari 12000 katika wilaya ya manyoni pia wamepata ekari 500 katika eneo la Itigi na Ekari 500 kwenye eneo la Ikungi ambazo zote zinaendelezwa kwa mtindo wa kilimo cha pamoja.
Dkt. Nchimbi aliongeza kuwa mpango wa baadaye ni kuongeza eneo na kuanzisha ushirika wa pamoja wa wakulima wa Korosho ambapo pia wametenga maeneo kwa ajili ya kujenga viwanda na maghara kwa ajili ya kuchakata na kuhifadhia Korosho.
“Mpango wetu wa baadaye kwenye eneo hili ni kuweka miundombinu ya kisasa na viwanda vikubwa.Tunataka minada yote ifanyike hapahapa”alisisitiza Mkuu wa Mkoa
Aidha alitoa rai kwa wananchi popote nchini kuja kulima zao hilo kwenye eneo hilo huku akionya kuwa Serikali itamtoa mtu yoyote atakayebainika kutumia eneo hilo kwa lengo lisilokusudiwa.
“Tunaelewa wanakuja ili kupata hati ya eneo hili ili wafanye matumizi mengine.Nawatangazia kuwa wasijidanganye kwa kuwa hati inayotolewa hapa ni maalum kwa ajili ya kulima zao la Korosho na siyo vinginevyo hivyo tupo makini sana katika hilo” alisema
Alisema kutokana na tafiti zilizofanywa na Taasisi ya Kilimo ya Naliandele, imeonyesha kuwa eneo hilo ni bora ukilinganisha na maeneo mengi hapa nchini na kwa kuwa korosho za eneo hili zinawahi zaidi kukua na pia zinazaa mara mbili kwa mwaka kutokana na eneo hili kuwa na misimu miwili ya kiangaza hivyo kutoa maua mara mbili kwa mwaka mmoja.
Aidha alisema kutokana na eneo hili kuwa na umuhimu wa pekee katika kilimo cha Korosho tayari taasisi mbalimbali za kilimo za Serikali zimeanzisha ofisi za kudumu ili kuwasaidia wananchi kwenye kilimo cha zao hilo. Alizitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni Taasisi ya Utafiti wa kilimo Naliandele na Bodi ya Korosho nchini.
Dkt. Nchimbi alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kutoa pikipiki nne kwa ajili ya kusadia kazi hiyo na kwamba aliahidi jumla ya pikipiki kumi.
“Kipekee kabisa nachukua nafasi hii kumpongeza Rais wetu kwa kweli yupo pamoja na sisi katika mpango huu ametutia nguvu sana, tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu aishi miaka mingi” alisema
Alisema mapindunzi ya kijani ya kilimo cha Korosho yameifanya Singida kuwa tofauti na ya awali iliyosadikiwa kuwa Singida ya njaa,masikini, kame na isiyokuwa na fursa ambapo hata watumishi wa umma walikuwa anakataa kuhamia.
Alisema baada ya kufanikiwa katika mradi huu mkoa unatarajia kuanzisha mradi mwingine kama huo kwa mazao ya kudumu baada ya kufanya tafiti za kutosha ili kuinua uchumi wa wananchi wa kawaida wa mkoa huo.
Alisema mkakati wa sasa ni kuufanya Singida kuwa mkoa wenye uchumi mkubwa kwa kuwa mbali ya kuwa na rutuba na hali ya hewa nzuri pia una utajiri wa raslimali za kutosha ikiwa ni pamoja na vivutio mbalimbali vya kihistoria kama kijiji cha kilimatinde ambacho kinahistoria ya kuwa kituo cha njia kuu ya watumwa toka miaka ya 1885 na ngome ya utawala wa Mjerumani na Mwingireza, mabwawa makubwa ya samaki na kituo kikubwa duniani cha Hija kilichopo Sukamahela.
Kiongozi wa msafara wa Chuo Ulinzi cha Taifa, Mhe. Balozi Peter Kallaghe alipongeza juhudi na mapinduzi makubwa yanayofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Singida ambapo alisema mageuzi haya yanapaswa kuigwa na mikoa yote hapa nchini ili kuunga mkono jitihada za kuifanya Tanzania kuwa Serikali ya viwanda ifikapo 2025 yanayoongozwa na Rais John Pombe Joseph Magufuli.
Toa Maoni Yako:
0 comments: