Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Bambare wilayani Kondoa, ambapo wananchi hao walimuomba awasaidie mabati ili kuweza kukamilisha ujenzi wa madarasa kijijini hapo.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kondoa, Dodoma Alhaji Othman Gora akiwasalimia Wananchi wakati wa mkutano wa hadhara kati ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na Wananchi wa Kijiji cha Bambare alipotembea Kijiji hicho.
Bw. Haji Juma akimuelezea Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (hayupo pichani), changamoto ya mabati yaliyokwamisha umaliziaji wa madarasa hayo kijijini hapo
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akiteta jambo na Diwani wa Kata ya Bambare Bw. Adam Iyerya alipotembea Kijiji hicho.
Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Bambare wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (hayupo pichani), alipokuwa anatolea majibu ya baadhi ya changamoto zilizotolewa na wanakijiji hao.


Na Mwandishi wetu, Kondoa

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amemuagiza Afisa Mipango wa Wilaya ya Kondoa Bw. Joshua Mnyangáli kufuatilia yalipopelekwa mabati ya Shule ya Msingi Gayo iliyopo katika Kijiji cha Bambare yaliyotolewa na Mbunge huyo ili kumalizia vyumba vya madarasa ya shule hiyo.

Agizo hilo amelitoa alipofanya ziara katika Kijiji cha Bambare wilayani Kondoa wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya ukarabati wa shule, vituo vya afya na miundombinu ya maji.

Dkt. Kijaji alisema kuwa hajui nini kimetokea hadi shule hiyo haijapelekewa mabati wakati alinunua mabati zaidi ya 1000 na kuagiza yagawanywe idadi sawa kutoka na na uhitaji wa kila shule ili ujenzi wa vyumba vya madarasa ukamilike na wanafunzi waweze kusoma vizuri.

Wananchi wa Kijiji hicho walieleza kuwa kumekuwa na changamoto ya mabati kwa ajili ya umaliziaji wa vyumba vya madarasa ambayo walikuwa wameanza kujenga kwa kutumia nguvu kazi yao.

Dkt. Kijaji alishangazwa na taarifa za ukosefu wa mabati kwa ajili ya kuezeka maboma hayo ya madarasa wakati alikwishatoa mabati na ndio sababu amemwagiza Afisa Mipango wa Wilaya hiyo kufuatilia yalipo mabati hayo na yapelekwe kijijini hapo ili kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa.

Mbunge huyo alisema kuwa iwapo kutakua na matumizi yasiyofaa ya mabati hayo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kukwamisha juhudi za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Katika kuhakikisha vyumba hivyo vya madarasa vinakamilika kwa haraka nachangia tena shilingi milioni moja ili kuharakisha umaliziaji wa vyumba hivyo vya madarasa uweze kufanyika kwa haraka ili wanafunzi wetu waweze kutumia madarasa hayo”, alisema Dkt. Kijaji.

Aidha Dkt. Kijaji aliuagiza uongozi wa wilaya hiyo hukakikisha wanafuatilia vizuri utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi inayofadhiliwa na Serikali ili kuhakikisha ina kamilika kwa wakati kwa sababu Serikali haianzishi mradi mpya bila kutoa fedha zote za miradi husika.

Kwa upande wake Afisa Mipango wa Wilaya ya Kondoa Vijijini Bw. Joshua Mnyangáli alimuahidi Dkt. Kijaji kutekeleza agizo hilo na kuhakikisha mabati hayo yanafikishwa sehemu husika kama ilivyoelekezwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: