RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Kebwe Stephan Kebwe kufuatia ajali ya kuripuka kwa lori la mafuta na kusababisha vifo pamoja na majeruhi kadhaa.
Katika salamu za rambirambi ambazo Rais Dk. Shein amemtumia Mkuu wa Mkoa, alieleleza kuwa amemepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vilivyotokana na ajali ya kuripuka kwa lori la mafuta iliyotokea asubuhi ya leo, tarehe 10 Agosti, 2019 katika maeneo ya Itigi Msavu Mkoani Morogoro na kusababisha vifo vya Watanzania waliopungua 60 na majeruhi kadhaa.
Rais Dk. Shein katika salamu hizo alieleza kuwa yeye binafsi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar anatuma salamu za rambi rambi kwa wanafamilia wa marehemu, marafiki, wananchi wa Mkoa wa Morogoro na Jamahuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla.
“Kwa hakika msiba huu umetugusa wananchi sote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuondokewa ghafla na ndugu zetu ambao ni nguvu kazi ya Taifa” ilieleza sehemu ya taarifa ya Rais Dk. Shein.
Aidha, salamu hizo zilimuomba Mwenyezi Mungu ampe Mkuu huyo wa Mkoa, wanafamilia pamoja na Watanzania wote moyo wa subira katika kipindi hichi kigumu cha msiba.
Vile vile katika salamuhizo za rambirambi, Rais Dk. Shein alimuomba MwenyeziMungu awalaze mahala pema wote na awape nafuu ya haraka majeruhi wa ajali hiyo ili waweze kupata shifaa na waendelee na majukumu yao mbalimbali ya ujenzi wa Taifa.
Mapema leo asubuhi lori lililokuwa limebeba shehena ya mafuta aina ya petroli likitokea Dar-es-Salamu lilipinduka na kuwaka moto katika eneo la Itigi Msamvu wakati wananchi wakijaribu kuchota mafuta yaliyomwagika baada ya gari hilo kupata ajali na kuanguka
Toa Maoni Yako:
0 comments: