Wakili kutoka kituo cha utetezi wa haki za binadamu, THRDC, Shilinde Swedy akizungumza na wanahabari nje Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu juu ya kilichojiri mahakamani hapo kufuatia maombi dhidi ya kushikiliwa kwa mwandishi wa Habari za uchunguzi Erick Kabendera.
Wakili kutoka kituo cha utetezi wa haki za binadamu, THRDC, Shilinde Swedy akijadili jambo na wakili wa kujitegemea Gebra Kambore Mahakamani hapo.​

Na Karama Kenyunko, Michuzi TV.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa Serikali kuwasilisha kiapo kinzani mahakamani hapo Augusti 5, mwaka 2019 kujibu hoja kuhusu kukamatwa kwa mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera.

Hakimu Mkazi Mkuu, Augustine Rwizile ametoa maagizo hayo leo Agosti Mosi, 2019 baada ya Wakili kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Shilinde Swedy kuwasilisha maombi ya kutaka Kabendera afikishwe mahakamani kwa sababu Jeshi la Polisi linamshikilia tangu Julai 29, 2019 hadi leo.

Katika maombi hayo namba 14 ya mwaka 2019 yaliyofunguliwa Julai 30, wakili huyo amedai kuwa hadi sasa saa 24 zimeshapita, hivyo anapaswa kufikishwa mahakamani dhidi ya tuhuma zozote zinazomkabili kwa ajili ya haki zake za msingi ikiwemo dhamana kwani kosa lake linadhaminika.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon ameiomba Mahakama iwape muda mpaka August 7 mwaka 2019 kwa ajili ya kuwasilisha kiapo kinzani katika maombi hayo, lakini upande wa utetezi ulipinga na kuomba wafanye hivyo, Agosti 2, mwaka 2019.

Hata hivyo baada ya mabishano na kusikiliza hoja za pande zote mbili mahakama imeamuru majibu hayo yaletwe Agosti 5,mwaka 2019 saa saba mchana.Hakimu Rwizile ameutaka upande wa Serikali kuwasilisha kiapo kinzani Agosti 5, mwaka 2019.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: