Mhasibu Mkuu wa Serikali Bw. Francis Mwakapalila, akiwahimiza washiriki wa mafunzo ya Mfumo mpya wa Ulipaji Serikalini- MUSE, kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini- TARURA, kuhakikisha wanauelewa na wanautumia ili kuiwezesha Serikali kupata taarifa za Fedha kwa wakati, katika ukumbi wa Hazina Ndogo mkoani Morogoro.
Mtaalamu wa Mfumo wa Ulipaji Serikalini kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Ndewingia Mashauri, akitoa mafunzo kwa wahasibu na wahandisi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini- TARURA, kutoka maeneo mbalimbali nchini, mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Hazina Ndogo mkoani Morogoro.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini- TARURA, Mhandisi Victor Seff, akieleza uhitaji wa Mfumo wa ulipaji Serikalini katika Taasisi anayoiongoza ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za fedha kwa urahisi, wakati wa mafunzo ya mfumo huo yaliyofanyika katika ukumbi wa Hazina Ndogo mkoani Morogoro.
Washiriki wa mafunzo ya Mfumo wa Ulipaji Serikalini- MUSE, kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini- TARURA, wakifuatilia mada zilizotolewa na wataalamu, katika ukumbi wa Hazina ndogo, mkoani Morogoro.
Mhasibu Mkuu wa Serikali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Francis Mwakapalila (katikati), Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini- TARURA na Wizara ya Fedha na Mipango, baada ya ufunguzi wa mafunzo ya Mfumo mpya wa ulipaji Serikalini kwa wahasibu na wahandisi wa TARURA, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Hazina ndogo mkoani Morogoro. (Picha na Geofrey Kazaula, TARURA)
Na Geofrey Kazaula, TARURA, Morogoro
Mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE) umeanzishwa na wataalamu wa ndani ili kuunganisha mifumo mingine iliyopo, lengo likiwa ni kupunguza gharama na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za fedha.
Hayo yameelezwa na Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bw. Francis Mwakapalila, ambaye alikuwa mgeni Rasmi katika ufunguzi wa mafunzo ya Mfumo wa Ulipaji Serikalini- MUSE kwa wahasibu na wahandisi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini- TARURA mkoani Morogoro.
Bwana Mwakapalila alisema kuwa mfumo huo umetengenezwa na wataalam wa ndani kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na utaanza kutumiwa na TARURA kisha kutumiwa na Taasisi zote za Serikali pamoja na Wizara baada ya kujiridhisha na ufanisi wake.
“Nitoe wito kwa washiriki wote wa mafunzo haya kuhakikisha wanauelewa vizuri mfumo na kuwa tayari kuutumia mara tu baada ya mafunzo kukamilika kwa kuwa mfumo huu ni muhimu kutoka na mabadiliko ya teknolojia katika mifumo ya fedha duniani”, alisema Bw. Mwakapalila .
Naye Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, amewataka wataalam wa Wakala huo wanaoshiriki mafunzo, kutokuwa na mtazamo hasi kuhusu mfumo na badala yake changamoto watakazo kutana nazo waziwasilishe mahali husika ili kuweza kutafutiwa ufumbuzi kwa kuwa mfumo huo ndio suluhisho la matumizi bora ya fedha za Serikali.
Aidha ameeleza kuwa Wizara ya Fedha na Mipango imetoa wataalam wa kutosha ili kuhakikisha wahasibu wote wa TARURA wanapatiwa mafunzo na kuuelewa mfumo kwa kina.
Kwaupande wake Mkurugenzi wa Mifumo ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. John Sausi, alieleza kuwa mfumo huo utaiwezesha Serikali kuangalia malipo yanayofanyika Katika Taasisi, Kampuni na wadau wengine wanaotoa huduma Serikalini .
Alisema kuwa mfumo huo ulianza baada ya kukusanya mahitaji kutoka kwa wadau mbalimbali zikiwemo Taasisi Ishirini za Serikali na kwamba Taasisi ya TARURA itakuwa ya kwanza kutumia mfumo huo kupitia wahasibu wake na wahandisi watakao kuwa wakiidhinisha malipo.
Bwana Sausi, alisema mafunzo hayo yanawahusisha wahasibu na wahandisi wa TARURA nchi nzima kuanzia ngazi ya Halmashauri lengo likiwa ni kumwezesha Mtendaji Mkuu wa TARURA kuona malipo yote yanayofanyika na Wakala huo katika sehemu mbalimbali kwa wakati.
Wizara ya Fedha na Mipango imekuwa ikitumia Mifumo ya Fedha tangu miaka ya Sitini na kutokana na ukuaji wa teknolojia imeamua kufanya maboresho ya mifumo hiyo ili kuendana na mahitaji ya sasa na kurahisisha kupata hesabu sahihi za fedha kwa wakati.
Toa Maoni Yako:
0 comments: