RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Makampuni ya S.S. Bakhresa, Sheikh Said Salim Bakhressa kufuatia vifo vya wafanyakazi watano wa Azam Media Limited kutokana na ajali ya barabarani.

Ajali hiyuo imetokea juzi (Jumatatu) Julai 8, 2019 katika eneo la katikati ya Igunga (Tabora) na Shelui (Singida). Wafanyakazi hao ni kati ya watu saba waliofariki dunia katika ajali hio baada ya basi aina ya Coaster waliokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na gari la mizigo wakati wakielekea Wilayani Chato kwa ajili ya uzinduzi wa Hifadhi hiyo ya Taifa ya Chato-Burigi. 

Katika salamu hizo za rambirambi Rais Dk. Shein alieleza kuwa amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya ajali hio na kwamba yeye binafsi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla wamejawa na simanzi nzito kufuatia vifo vya wafanyakazi hao.

“Kutokana na msiba huu, natoa salamu za rambirambi kwako Sheikh Said Salim Bakhressa, ndugu, wanafamilia wa marehemu, marafiki, wafanyakazi wote wa Makampuni ya S.S. Bakhressa pamoja na watazamaji, wasikilizaji na wafuatiliaji wa vipindi na habari mbali mbali zinazotolewa na Azam Media Limited, ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, ilieleza sehemu ya salamu za rambirambi alizozituma Dk. Shein. 

Kadhalika, Rais Dk. Shein katika salamu hizo za rambirambi amemuomba Mwenyezi Mungu ampe moyo wa subira Sheikh Said Bakhressa katika kipindi hiki kigumu pamoja na wale wote walioguswa na msiba huo wakiwemo wafanyakazi wote wa nyanja ya habari. 
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein amemuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu hao pahala pema peponi na awape afuweni na afya njema wale wote waliojeruhiwa katika ajali hio, ili waweze kuendelea na majukumu yao mbali mbali. 

Uongozi wa Azam Media Limited umethibitisha wafanyakazi waliofariki kuwa ni Salim Mhando, Said Haji, Florence Ndibalema, Sylvanus Kasongo, Charles Wandwi pamoja na dereva na utingo wa gari hilo ambapo waliojeruhiwa na kulazwa ni Mohamed Mwinshehe, Mohamed Mainde na Artus Masawe.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: