Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Muigizaji wa Tamthilia maarufu ya ESMERALDA kutoka nchini Mexico, aliyekuja nchini kwa mapumziko ya siku saba na watoto wake, wakati Waziri Mkuu akiwa mkoani Arusha kwenye ziara ya kikazi. Julai 23, 2019. Tokea kushoto ni watoto wa muigizaji huyo, Carlo Collado (14) na Luciano Collado (15). Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wafanyakazi wa hoteli ya The Retreat at Ngorongoro iliyoko wilayani Karatu, wakati akiwa mkoani Arusha kwenye ziara ya kikazi. Julai 23, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
*Zimo Ngorongoro, Serengeti, Manyara na Tarangire
*Ni Leticia Calderon, aliyeigiza filamu ya ESMERALDA
MUIGIZAJI maarufu wa filamu kutoka Mexico, Bi. Leticia Calderon (51) amesifia rasilmali ya hifadhi za wanyama ambayo Tanzania imejaliwa kuwa nayo.
Muigizaji huyo ambaye amefanya kazi hiyo kwa miaka 36, na ameigiza sinema maarufu ya ESMERALDA, yuko nchini kwa mapumziko ya siku saba kwenye hifadhi za wanyama za ukanda wa Kaskazini.
Akisalimiana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi, Bi. Calderon amesema amevutiwa na uzuri wa hifadhi za Tanzania na idadi kubwa ya wanyama aliowaona kwenye hifadhi za Taifa za Tarangire, Manyara na Ngorongoro.
“Kwa miaka mingi nilikuwa natamani sana kuja Tanzania kuona wanyama. Tuliyoyaona yametufurahisha mimi pamoja na wanangu. Nchi yenu ina uzuri wa kustaajabisha. Watu wenu ni wema na wakarimu,” alisema Bi. Calderon.
“Ninafurahi kwamba ndoto yangu imetimia. Tulienda Tarangire, Manyara na Ngorongoro ma sasa tunajiandaa kwenda Serengeti. Tulipokuwa Ngorongoro, tuliona simba wanne, majike wawili na madume wawili. Tumefurahi sana na nikirudi nyumbani, nitawaonyesha picha marafiki zangu na kuwaalika waje kutembelea Tanzania,” alisema.
Bi. Calderon ambaye amefuatana na wanaye wawili Luciano Collado (15) na Carlo Collado (14) alisema wakimaliza mapumziko yao huko Serengeti watakwenda Masai-Mara kwa siku tatu na kisha wataelekea Paris, Ufaransa kumtembelea rafiki yake ambaye waliigiza filamu pamoja huko nyuma.
Bi. Calderon pia ameigiza tamthilia ndefu (soap operas) 29 katika jiji la Mexico City ambalo ni mji mkuu wa Mexico. Mbali ya Esmeralda, filamu nyingine maarufu ambazo ameigiza ni En Nombre del Amor (In the Name of Love); Amor Bravia (Valiat Love) na La Indomable (The Taming of the Shrew).
Waziri Mkuu alimshukuru mwanamama huyo na wanaye kwa kuichagua Tanzania kwa mapumziko yao na akawatakia heri katika safari yao ya mbugani.
Akizungumza na wafanyakazi wa hoteli ya The Retreat at Ngorongoro iliyoko Karatu ambako muigizaji huyo alikuwa amefikia, Waziri Mkuu aliwataka wafanyakazi wa hoteli hiyo na wengine walioko kwenye hifadhi za Taifa, wafanye kazi kwa bidii ili huduma zao ziwavutie watalii wengi zaidi.
“Tunampongeza mwenye hoteli kwa uwekezaji huu mkubwa lakini niwasihi wafanyakazi mchape kazi ili wageni wengi zaidi waweze kuvutiwa na huduma zenu,” alisema Waziri Mkuu.
“Sasa hivi tunapata watalii wengi na watu maarufu kama hawa, wamechagua kuja kupumzika Tanzania. Mheshimiwa Rais Magufuli ameshanunua ndege sita, nyingine mbili zinakuja, moja itawasili Oktoba, na nyingine Januari, mwakani. Na tayari kuna ndege tatu nyingine zimeagizwa. Lengo lake ni kuimarisha usafiri wa ndani kwa kutumia ndege,” alisema.
“Zamani ilikuwa ni vigumu sana kuja Tanzania moja kwa moja. Ili mtalii afike, ilibidi apitie nchi nyingine na huko akidakwa anaondokea hukohuko. Sasa hivi, akitoka kwao ataweza kuja Tanzania moja kwa moja, akitua KIA anakuja Karatu au Serengeti moja kwa moja,” alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments: