Mabasi ya Ndani ya Mkoa wa Njombe yakiwa kwenye eneo lao la Magesho katika stendi kuu mpya ya Njombe.
Mabasi yakiingia kwenye lango la mabasi katika stendi kuu mpya ya Njombe.
Mwasibu wa Mapato George Mwaseba akito maeleko kwa abiria kwenye geti la kutokea abiria wanaoenda kwa miguu utaratibu ambao awali haukuwepo kwenye stendi ya zamani.
Mabasi yaendayo Mikoani yakisubiri muda wa kuanza safari kuelekea Mikoani.
Mwasibu wa Mapato George Mwaseba akito maeleko kwa abiria kwenye geti la kutokea abiria wanaoenda kwa miguu utaratibu ambao awali haukuwepo kwenye stendi ya zamani.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda (Wa kwanza kulia), Mratibu wa Mradi wa ujenzi wa stendi mpya Njombe Mhandisi Rais Tembo (Katikati) akifuatiwa na Mweka hazina wa Halmashauri Dorcas Mkello wakiwa wamekaa katika eneo la kusubiria abiria kwenye stendi kuu mpya Njombe.
Mtoza Ushuru wa Halmashauri akipokea fedha kwa ajili ya kulipia ushuru wa stendi kwa mabasi madogo kwenye mojawapo ya mabasi yanayofanya shughuli zake ndani ya Mkoa.
Mabasi yakiingia na kutoka kwenye Lango la Mabasi kuashiria kuendelea kwa shughuli za usafirshaji katika stendi kuu mpya Njombe.
Na Hyasinta Kissiama-Afisa Habari H/Mji Njombe.
Kufuatia agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli la kutaka stendi kuu mpya ya Njombe kuanza kutumika ifakapo May 11,2019 hatimae stendi hiyo imeanza kazi rasmi leo.
Akizingumza na Waandishi wa Habari, Abiria na Wananchi waliofika katika stendi hiyo mpya, Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Ruth Msafiri amewapongeza Wananchi kwa kuitikia wito wa kuhamia katika stendi mpya licha ya kuwepo na shughuli za umalizia wa ujenzi wa stendi hiyo zikiendelea.
“Nawapongeza Wananchi kwa kujitokeza kwa wingi. Wengi mmekuja kushuhudia kama kweli stendi imeanza lakini pia kwa wasafiri, wadau wa vyombo vya usafirishaji mwitikio umekuwa mkubwa na hii inaonesha wazi jinsi mlivyokuwa na kiu ya siku nyingi kuitumia stendi hii” Alisema MKuu wa Wilaya.
Mkuu wa Wilaya aliongezea kuwa”Tunamshukuru Mhe. Rais kwani kupitia maelekezo yake kumefanya stendi hii ianze kufanya kazi. Ametusaidi sana katika kutusukuma katika siku hizi za mwishoni na leo tumetekelza agizo lake stendi imeanza kufanya kazi na Wananchi wanafuraha iliyopitiliza” Alisema
Johanes Kyelula ni Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na Usalama wa Stendi ambaye yeye alisema kuwa anaipongeza Halmashauri kwa kufanikiwa kuanza kutumika kwa stendi hiyo kama alivyo agiza Rais na watahakikisha kuwa wanasimamia ulinzi ndani ya stendi na kuhakikisha kuwa nidhamu katika stendi mpya inakuwepo ikiwa ni sambamba na kuwachukulia hatua na wote watakaotoa lugha za matusi kwa abiria au kuona watu wasio na nia njema ya kuwaibia abiria kwenye stendi hiyo.
Glory Sanga ni mmojawapo wa wafanyakazi katika mabasi yanayofanya safari zake nje ya Mkoa wa Njombe ambaye yeye amesema kuwa stendi mpya mpaka kukamilika kwake itakuwa ni miongoni mwa stendi bora na zenye viwango vya hali ya juu ukilinganisha na Mikoa ambayo amekuwa akipita yenye stendi.
“Mimi ni Kondakta na nimekuwa nikisafiri Mikoani nimeona utofauti wa stendi hii na hizo za Mikoa mingine. Stendi hii imejengwa kwenye ubora hata ukiangalia kwa macho. Japokuwa haijakamilika yote, ni matumaini yangu itakapo kamilika yote itakuwa ni miongoni mwa stendi za kuigwa katika Tanzania. Naipongeza Halmashauri ambao ndio wasimamizi wa ujenzi wa stendi kwa kazi nzuri” Alisema Glory
John Msemwa miongoni mwa abiria walifika kwenye stendi mpya leo amesema kuwa changamoto nyingi kwa sasa zimepungua ukilinganisha na stendi ya awali.
“Kwanza stendi ya zamani ilikuwa ndogo sana hii stendi ni kubwa, miundombinu ni mizuri vyoo maji yapo vyoo vizuri, visafi hata ukiangalia huku hakuna matope kama kule kwenye stendi ya mwanzo. Stendi ya awali matope mengi hasa wakati wa mvua hakuna hata sehemu ya kukaa. Huku kuna maeneo mengi ya kukaa ikikamilika itakuwa kivutio cha watalii wa ndani” Alisema Msemwa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda alisema kuwa mpaka sasa ujenzi wa stendi hiyo umekamilika kwa asilimia 95 na amesema kuwa shughuli zolizosalia zinatarajia kukamilishwa ndani ya wiki mbili zijazo.
“Tunashukuru kwa pongezi kwani haikuwa kazi rahisi. Asilimia tano zilizosalia tutazikamilisha ndani ya wiki mbili. Licha ya mabasi kuanza tulikuwa pia na kikao na wahandisi ili kuona ni namna gani kazi zilizosalia tunazikamilisha ndani ya wiki mbili licha ya kuwepo na changamoto ya mvua za mara kwa mara.”Alisema Mwenda
Mwenda aliongezea kuwa licha ya kutoa huduma kwa wWananchi stendi hiyo pia ni chanzo kikuu cha mapato kwa Halmashauri na wanataraji kukusanya milioni mia tatu kwa mwaka hayo yakiwa ni makisio ya chini.
Mkurugenzi huyo pia aliendelea kuwasisitizia wananchi kuhakikisha kuwa wanafuata utaratibu uliowekwa wa kuchangia gharama ya Tsh 200 kwa wale ambao wanaingia stendi pasipokuwa na tiketi ya abiria.
Akiongelea suala wa Wajasiriamali wadogo Bi Mwenda alisema umeandaliwa utaratibu mzuri na punde wataelekezwa utaratibu kwa wajasiriamali hao na amewasisitiza kuhakikisha kuwa wanakuwa na kitambulisho cha wajasiriamali.Mwenda amewapongeza wananchi kwa mwitikio wao na kusema kuwa ataendelea kutoa tarifa ya mabadiliko yoyote yatakayokuwepo katika stendi hiyo kadri muda unavyozidi kwenda na kwa kadri ya matengenezo yanayoendelea katika stendi hiyo.
Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Mji Njombe ni miongoni mwa Halmashauri 18 Nchi zinazonufaika na mradi wa uboreshaji na uimarishaji Miji ambapo kwa upande wa Halmashauri ya Mji Njombe inatekeleza ujenzi wa soko la kisasa na ujenzi wa stendi kuu ya mabasi ambapo kwa upande wa stendi inakadiriwa kutumia bilioni 9 mpaka kukamilika kwake.
Toa Maoni Yako:
0 comments: