Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira January Makamba kizungumza kwenye mkutano na viongozi na watendaji wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiwemo Wenyeviti wa Mitaa yote ya mkoa na agenda kuu ikiwa ni marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki,jana Jumanne Mei 21, 2019 katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mwanasheria toka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Manchare Heche akizungumza na wadau mbalimbali wa Mazingira ambapo amesema ni kosa kisheria pindi watakapokutwa na mifuko ya Plastiki kuanzia Juni mosi mwaka huu jana Jumanne Mei 21, 2019 katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)
Baadhi ya viongozi na watendaji wa mkoa wa Dar es Salaam wakiwemo wenyeviti wa Mitaa yote ya mkoa wakiwa katika mkutano uliofanyika leo May 21, 2019 kwenye ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)
Muonekano wa vifungashio vilivyo ruhusiwa kisheria kama vinavyo onekana katika picha.
Serikali imetoa wito kwa Watanzania kuwa ni kosa kisheria pindi watakapokutwa na mifuko ya Plastiki kuanzia Juni mosi mwaka huu.
Wito huo umetolewa leo Jumanne May 21, 2019 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba wakati akizungumza kwenye kikao cha viongozi na watendaji wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiwemo Wenyeviti wa Mitaa yote ya Mkoa huo na agenda kuu ikiwa ni marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki.
Waziri Makamba amesema ni vyema watendaji wote wa Mkoa wa Dar es Salaam wakahamasisha wananchi wao ili waweze kutekeleza agizo hilo kwani adhabu mbalimbali ikiwemo faini au kifungo gerezani zitahusika kwa atakayekiuka katazo hili kulingana na Kanuni za “Marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki za Mwaka 2019” zilizoandaliwa chini ya Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.
Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mwita Waitara amezielekeza Mamlaka ya Serikali za Mitaa kote nchini kuhakikisha wanatenga maeneo maalum ya kuhifadhia mifuko ya plastiki itakayosalia ifikapo Juni mosi mwaka huu na wananchi wa maeneo husika kujulishwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Abubakari Mussa Kunenge akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ameeleza mikakati ambayo Mkoa wanaifanya ya kudhibiti taka zinazozalishwa jijini ikiwemo mfumo mzuri wa uratibu na usimamizi kwa viongozi katika zoezi hilo.
Baadhi ya watendaji wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao wameshiriki kwenye kikao hicho wameeleza kuwa ni vyema ikaendelea kutolewa elimu kwa wananchi ili waweze kutii agizo hilo kwa wakati uliopangwa.
Bidhaa ambazo hazitaathiriwa na katazo hili ni pamoja na vifungashio vya bidhaa kama vile vifungashio vya madawa, vifungashio vya vyakula kama vile: maziwa, korosho, n.k bidhaa za viwandani, kilimo na ujenzi. Hata hivyo, vifungashio ni lazima vikidhi viwango vilivyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Toa Maoni Yako:
0 comments: