Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni, akiwasili katika eneo la Kiwanda na Shamba la Miwa Mbigiri linalohudumiwa na Gereza la Mbigiri wakati wa ziara ya kutembelea mradi huo mkoani Morogoro.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(kushoto), akisikiliza maelezo yanayohusu maendeleo ya Shamba la Miwa Mbigiri linalohudumiwa na Gereza la Mbigiri wakati wa ziara ya kutembelea mradi huo mkoani Morogoro. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Serikali imetoa onyo kwa wafanyabiashara au mtu yoyote mwenye nia ya kuhujumu Miradi ya Serikali kwa maslahi binafsi kuacha mara moja na endapo mtu atathibitika kuhusika na suala hilo sheria kali zitachukuliwa dhidi yao.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni leo alipotembelea Kiwanda na Shamba la Miwa katika Gereza la Mbigiri ambalo linakadiriwa kuzalisha tani za sukari Laki Mbili kwa Mwaka na kuondoa adha ya kuagiza sukari nje ya nchi.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kukuza viwanda mbalimbali ikiwemo kiwanda cha Sukari Mbigiri na kuwezesha mamia ya wananchi kupata ajira pamoja na kukuza uchumi wa nchi.

“Kuna taarifa za baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa sukari kupenyeza maslahi yao binafsi katika miradi hii mikubwa ya serikali ikiwemo shamba hili la miwa hapa Mbigiri, nawaasa waache mara moja kwani watakapobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa juu yao ikiwemo na kosa la uhujumu uchumi” alisema Masauni

Akitoa taarifa ya shamba hilo Mkuu wa Gereza Mbigiri, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Shija Fungwe alisema shughuli zinaendelea katika shamba hilo kwa kutumia nguvu kazi ya wafungwa kutoka katika gereza hilo huku wafungwa 280 wakitumika katika shamba hilo.

“Kazi ya kupanda eneo lililo tayari inaendelea huku kazi ya kulima hekta 500 inaendelea na kati ya hizo hekta 200 zimeshalimwa kwa awali na lengo letu ikifika mwezi juni mwaka huu inatakiwa zilimwe hekta 700 tukitumia nguvu kazi ya wafungwa” Alisema ACP Fungwe

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameelekeza kubadilishwa kwa Mjumbe wa Bodi ya Kiwanda hicho, ACP Rocky Mbena anaewakilisha Jeshi la Magereza.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: