RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi, alipowasili katika ukumbi wa Mkutano Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo leo 11-4-2019.(Picha na Ikulu)
/RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashari Tanzania Profesa Palamagamba Kabudi kushoto na ujumbe wake wakati wa mazungumzo yao yaliofanyika leo Ikulu Zanzibar,11-4-2019(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, akiagana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika leo Ikulu Zanzibar, kushoto Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Gavu(Picha na Ikulu).

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa wakati Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatimiza miaka 55 ni vyema misingi ya Muungano ikaendelezwa ikiwa ni pamoja na kuiimarisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipofanya mazungumzo na Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki aliyefika Ikulu ikiwa ni pamoja na kupokea maelekezo na miongozo kutoka kwa Rais kufuatia kuteuliwa kushika wadhifa huo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli hivi karibuni.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alieleza kuwa ni miaka 55 ambayo inatimia rasmi mnamo Aprili 26 mwaka huu tokea kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao viongozi wake walioasisi Muungano huo Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Marehemu Julius Kambarage Nyerere waliweka misingi madhubuti.

Hivyo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuimarishwa na kuendelezwa misingi hiyo ambayo leo umeupelekea Muungano wa nchi mbili hizo kuwa imara, madhubuti sambamba na kuleta maendeleo endelevu kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alieleza kuwa miongoni mwa misingi hiyo ni pamoja na mashirikiano katika masuala mazima ya diplomasia ikiwa ni pamoja na mashirikiano na mataifa ya nje chini ya taasisi inayohusiana na Mambo ya Nje ambayo kwa hivi sasa ni Wizara hiyo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa Wizara hiyo ina umuhimu mkubwa katika kuendeleza masuala ya kidiplomasia hivyo mashirikiano ya pamoja yanahitajika kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili liweze kufikiwa lengo lililokusudiwa.

Aliongeza kuwa azma ya Wizara hiyo kuanzisha utaratibu wa kubadilishana uzoefu kati ya watendaji wa Wizara hiyo wa upande wa Zanzibar na wale wa Tanzania Bara kuja Zanzibar kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupanua wigo wa kiutendaji na mashirikiano.

Aidha, Rais Dk. Shein alimpongeza Profesa Kabudi kwa kuteuliwa na kukubali kushika wadhifa huo na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wake chini ya uongozi wake wataendelea kumpa mashirikiano ili Wizara hiyo iendelee kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kupongeza mashirikiano yaliopo kwa uongozi na watendaji wa Wizara hiyo na kueleza kuwa hatua hiyo ndio siri kubwa ya mafanikio ambayo yamefikiwa na yale yanayotekelezwa katika kuimarisha diplomasia ya uchumi.

Nae Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Wizara hiyo mbali ya kujikita na masuala ya mahusiano na mataifa ya nje pia ni sikio na jicho la mambo yote yanayohusu Muungano na yale yasiyohusu Muungano kutokana na umuhimu wake.

Profesa Kabudi alitumia fursa hiyo kutoka pongezi kwa Rais Dk. Shein pamoja na Rais Dk. John Pombe Magufuli na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini kushika wadhifa wa kufanya kazi hiyo ya uwaziri katika Wizara hiyo.

Waziri Kabudi aliongeza kuwa kuna kila sababu ya kuiendeleza misingi ya Muungano ambao unatimiza miaka 55 mnamo Aprili 26 mwaka huu ambapo misingi hiyo imeleta mafanikio na maendeleo makubwa kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri huyo alieleza mikakati iliyowekwa na Wizara yake ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu kati ya watendaji wa Ofisi ndogo ya Zanzibar na Makao Makuu ya Wizara hiyo kwa lengo la kupanua wigo na kuimarisha utendaji.

Profesa Kabudi alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa ataendelea kushirikiana na viongozi wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake kwa azma ya kuendeleza na kuimarisha malengo ya Wizara hiyo sambamba na kutekeleza misingi ya Muungano.

Pamoja na hayo, Waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alimueleza Rais Dk. Shein mchakato uliopo hivi sasa wa kuandaa Sera ya Diaspora ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo itapata msaada mkubwa kutoka Sera ya Diapora ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo imeshaundwa.

Pia, Waziri huyo alieleza hatua zinazoendelea katika ujenzi wa Ofisi ya Ubalozi pamoja na nyumba ya Balozi wa Tanzania huko Mascat nchini Oman ikiwa ni miongoni mwa kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na nchi hiyo.

Sambamba na hayo, Waziri huyo alipongeza maendeleo yaliyofikiwa Zanzibar hasa katika sekta za afya, elimu, maji, miundombinu, utalii na uwekezaji hasa kwa wawekezaji wazawa ambao wamewekeza hapa Zanzibar ukiwemo mradi wa mji mpya wa Fumba.

Pia, Waziri Kabudi alipongeza juhudi zilizofikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya utalii ambapo hivi sasa Zanzibar imekuwa kivutio kikubwa cha watalii kutoka maeneo mbali mbali duniani likiwemo eneo la Masharki ya Kati.

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alimuonesha Profesa Kabudi chumba maalum kilichotumika kwa hatua za awali na viongozi waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa ajili ya kutiaji saini makubaliano ya Muungano. 
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: