Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi (Wa tatu kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Wa Shirika la Ndee la Precision Air Patrick Mwanri na wafanyakazi wa Shirika hilo waliokuja na ndege kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma baada ya uzinduzi wa safari hizo leo April Mosi kwenye Uwanja wa Ndege wa Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi akipata maelekezo kutoka kwa Rubani Kapteni Peter Fues namna wanavyoendesha ndege mara baada ya kuzindua safari za ndege za Shirika la Ndege la Precision Air kutoka Dar es Salaam kuelekea Makao Makuu ya nchi Dodoma leo kwenye Uwanja wa Ndege wa Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi akisalimiana na Rubani Kapteni Peter Fues baada ya kutua kwenye Jiji la Dodoma wakati wa uzinduzi wa safari za shirika hilo kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma leo kwenye Uwanja wa Ndege wa Dodoma..
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma akishuka kutoka kwenye Ndege ya Precision baada ya kuzindua safari za kutokea Dar es Salaam kuelekea Dodomaleo April Mosi leo kwenye Uwanja wa Ndege wa Dodoma.
Mkurugenzi wa Shirika la Ndege la Precision Air Patrick Mwanri akizungumzia uzinduzi wa safari za ndege kutokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma zitakazokuwa kuanzia siku ya Jumatatu hadi Jumamosi leo April Mosi kwenye Uwanja wa Ndege wa Dodoma., kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi.
Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma amezindua safari za ndege za Shirika la Ndege la Precision Air kutokea Dar es Salaam kwenda Dodoma leo April Mosi.
Akizungumza baada ya Ndege aina ya PW 466 katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi amesema sekta ya anga ni muhimu sana kwa maendeleo ya Jiji la Dodoma na kuja kwa shirika la Ndege la Precision Air kutaongeza zaidi fursa kwa watalii kuja kutembelea maeneo yaliyopo ndani ya Jiji na maeneo yaliyo karibu ikiwemo Kondoa.
Katambi amesema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli imetoa fursa ya ushindani kwa sekta binafsi na Precision Air ni moja ya wabia wakubwa wa maendeleo hususani kwenye masuala ya usafiri na imekuwa ikifanya kazi zake kwa muda mrefu na uaminifu mkubwa.
“Kwanza napenda kuwapongeza Shirika la ndege la Precision Air kwa uamuzi wa kuleta safari za kutokea Dar es salaam na kuja Dodoma na pia kutoka Dodoma kuelekea Kilimanjaro, hii kwetu ni fursa kubwa sana kwa maendeeo ya Jiji letu hususani kwenye sekta ya utalii kwani lengo letu ni kuhakikisha tunafikia malengo ya kuwa moja ya Jiji kubwa ndani ya Afrika Mashariki na Kati,”amesema
“Tayari kuna ujenzi wa Uwanja mkubwa wa kimataifa utakaokuwa unashuka ndege kubwa, Rais ameshatoa fedha na utajengwa Msalato sisi tumeshaleta Dreamliner na Airbus kwahiyo hata kama na nyinyi Precision Air mna ndege kubwa mnakaribishwa kuzileta,”amesema Katambi.
Amesema, angependa kuona Precision Air wakiboresha zaidi huduma zao kwa kuongeza safari za kuelekea maeneo tofauti ya Utalii kama Kigoma, Mwanza kwani fursa ya safari hizo zipo kutokana na Dodoma kuwa Jiji kwa sasa na watu wamekuwa na uhitaji wa safari hizo.
“Ndani ya Jiji la Dodoma kumekuwa na safari za Shirika la Ndege la Air Tanzania ila kwa sasa na nyie Precision mmekuja ninafurahi kwakuwa mmeweza kuongeza chachu ya maendeleo, mmerahisisha safari za wafanyakazi wetu pamoja na wageni wanaokuja kwenye ofisi za Serikali,”amesema Katambi.
Akizungumzia uzinduzi wa safari hizo Kaimu Mkurugenzi wa Precision Air, Patrick Mwanri amesema wanayo furaha kubwa kuchangia juhuhudi za Raisi wa awamu ya tano Dkt.John Joseph Pombe Magufuli na serekali yake katika kuundeleza na kuufungua mjii mkuu Dodoma pamoja na kuendeleza sekta ya anga.
“Kwa miaka 25 tumekuwa tukitekeleza jukumu la kuiiunganisha Tanzania na kuhakikisha abiria wanasafari kwa urahisi ndani na nje ya nchi. Safari zetu za Dodoma zitarahisisha shughuli za utawala na biashara kati ya Dodoma na Mikoa mengine na zaidi,”amesema Mwanri.
Pia tuanayo furaha kwa kuweza kuwapa abiria wetu uchaguzi mzuri wa muda wa kusafiri, kwa kuzingatia aina ya soko ni ukweli ulio wazi kwamba abiria wanahitaji uhuru katika kuchagua muda wa kusafiri na ndo maana tuna Ndege ya za Asubuhi na Mchana zikiwemo safari za saa 1:00 Asubuhi, Saa 3:25 Asubuhi na Saa 7:50 Mchana kwa safari za kutokea Dar es Salaam na Safari za saa 2:25 Asubuhi, saa 4:55 Asubuhi na saa 10:55 Alasiri kwa safari za Kutokea Dodoma. Aliongeza Bw. Mwanri
Mwanri amefafanua zaidi kuwa Precision Air itakua ikifanya safari zake moja kwa moja kwenda Dodoma kila Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Jumamosi, huku Kwa siku ya Alhamisi na Ijumaa safari hizo zitakua zikipitia Kilimanjaro.
Kwa upande wa Shirika la Ndege la Precision Air, amesema amefurahi kwa mapokezi makubwa waliyoyapata ndani ya Mkoa wa Dodoma na kupewa heshima kubwa. Ndege hiyo ya Precision Air ilikuwa ikiendeshwa na Rubani Kapteni Peter Fues akisaidiwa na Khalid Othman.
Shirika la Ndege la Precision Air lilianzishwa mwaka 1993 kama shirika binafsi la ndege za kukodi, likifanya safari zake kusafirisha watalii katika vivutio vya utalii kama Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Bonde la Ngorongoro pamoja na Visiwa vya Zanzibar. Sasa Shirika hilo lenye makoa yake makuu katika Jiji la Dar es Salaam limeendelea kukua na kuwa moja ya mashirika yanayo heshimika katika ukanda wa Africa Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Toa Maoni Yako:
0 comments: