*Aprili Mosi ni Maadhimisho ya Siku ya upandaji miti
Na Said Mwishehe, Globu ya jamii.
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umesema ili kukabiliana na athari za uharibifu wa misitu ipo haja ya kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na hali hiyo ikiwemo ya kila familia kuanzisha bustani ndogo yenye miche inayoweza kutoa kivuli na matunda ambayo inayolingana na idadi ya wanafamilia.
Ambapo hiyo itakuwa rahisi kuitunza miche hiyo kwa kutumia maji yanayopatikana nyumbani au kutumia umwagiliaji wa matone ya maji kwa kutumia chupa (drip irrigation).
Hayo yamesemwa kwenye taarifa ya TFS iliyotolewa leo Machi 28,2019, kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Upandaji Miti ambayo ni Aprili 1, 2019 na kitaifa maadhimisho ya siku hiyo yatafanyika wilayani Same mkoani Kilimanjaro ambayo yatakwenda sambamba kwa ngazi ya mikoa yote Tanzania Bara kupanda miti.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Tulizo Kilaga amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu ni ya kipekee kwa kuwa ni mwaka ambao utaratibu wa kuadhimisha siku hiyo utafanyika kwa kupanda miti zaidi badala ya kutumia fedha nyingi katika sherehe ya maadhimisho ya siku hiyo. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni 'Tanzania ya Viwanda inawezekana, panda miti kwa maendeleo ya Viwanda'.
Akifafanua zaidi kuhusu hatua nyingine za kuchukua kukabiliana na athari za uharibifu wa misitu ni kuongeza kiwango cha upandaji miti kwa kupanda mbegu moja kwa moja ardhini kwa baadhi ya miti hasa katika mikoa iliyo na maeneo yenye mvua nyingi ikiweepo Mikoa ya Tanga, Iringa, Mbeya na Njombe.
Pia kustawisha miti kwa kutumia miche inayojiotea yenyewe ardhini kama maotea. Miche hiyo inapandwa katika sehemu zilizokusudiwa ikiwa bado midogo. Njia hii inatumika hasa kwenye sehemu zenye mvua nyingi na udongo tifutifu.
Kilaga amesema ni vema kustawisha misitu ya asili kwa kutenga na kulinda eneo kutokana na uharibifu wa kimazingira ili mbegu ziote zenyewe (natural regeneration). Njia hiyo imefanikisha shughuli za kustawisha misitu na malisho ya mifugo mkoani Shinyanga na kwamba wananchi wa Shinyanga wanatumia utaalam wao wa jadi unaojulikana kwa jina la Ngitili wa kutenga maeneo na kuyapumzisha ili mbegu zijiotee zenyewe, matokeo yake mkoa huo umeongeza zaidi ya hekta 500,000 za ardhi ambayo ilikuwa imeharibika kabisa hapo awali lakini sasa ina miti.
Pia kuanzisha mashamba makubwa ya miti kwa lengo la kutunza mazingira na kujiongezea kipato na kwmaba katika kuadhimisha siku hiyo TFS itapanda miti katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa kushirikiana na wadau ambapo katika jiji la Dar es Salaam upandaji huo utafanyika eneo la Kilongawima Mbezi Beach kwa kupanda mikoko na mivinje.
"Wadau na wananchi wote mnakaribishwa kushiriki zoezi hili muhimu kwa mstakabari wa nchi yetu. Maadhimisho ya Siku ya Taifa ya kupanda miti yalifanyika kwa mara ya kwanza Januari Mosi mwaka 2001 kutokana na Waraka wa Waziri Mkuu namba 1 wa mwaka 2000 na kuhuhishwa mwaka 2009 na kuifanya siku hiyo kufanyika Aprili Mosi kila mwaka ukimtaka kila mwananchi kupanda miti kwa manufaa yake.
"Mwaka jana Siku ya Taifa ya Kupanda Miti iliadhimishwa kitaifa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Aprili 3 hadi 5, 2018.Ni wajibu wa kila mmoja wetu kutathimini athari atakazopata kutokana na ufyekaji na uharibifu wa misitu ili aamue kwa dhati kuihifadhi misitu kwa ajili ya kuwanufaisha watu wa kizazi hiki na vizazi vijavyo,"amesema.
Kuhusu maadhimisho ya siku hiyo ya upandaji miti ,Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania unatoa mwito kwa kila Mtanzania kutathmini tulikotoka, tulipo na tunapokwenda kuhusiana na hali ya misitu.
Toa Maoni Yako:
0 comments: