Wasanii wakimsaidia kijana Hamis Salumu mwenye matatizo ya kuvimba miguu kumuingiza katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupatiwa matibabu baada ya Rais Dkt John Pombe Magufuli kujitolea kumpatia matibabu kwa kupitia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda na Wasanii wakiongozwa na Steve Nyerere.
Wasanii wakiwa nje ya Chumba cha wagonjwa wa dharula katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili kushuhudia kijana Hamis Salumu akifikishwa kwa ajili ya matibabu.
Wasanii wakimsanidia Kijana Hamis Salum kumtoa nyumbani kwao Temeke jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuelekea hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar.
WASANII wa fani mbalimbali nchini wameamua kumsaidia kijana Hamisi Salum anayesumbuliwa na tatizo la kuvimba miguu kwa kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili ili apate matibabu kwani wanaamini atapona na kutimiza ndoto zake.
Akizungumza jana Machi 12, 2019 kwa niaba ya wasanii wenzake, Msanii maarufu nchini Steve Nyerere amesema wanamatumaini makubwa Hamis atapona, kikubwa ni Watanzania kumuombea kwa Mungu.
Amefafanua Hamis alishapelekwa nchini India kwa matibabu na kisha akarejea nyumbani Tanzania na baadae tena alipelekwa Muhimbili.
Ameongeza wasanii katika kuhakikisha Hamis anapona na kutimiza ndoto zake wameamua kumfuata tena nyumbani kwao na kisha kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili akatibiwe.
Steve Nyerere amesema baada ya wao kupaza sauti zao Rais Dk.John Magufuli amesikia na kwa kupitia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda wameamua kumsaidia.
"Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli kwa kujali wanyonge, wasanii tumepaza sauti zetu kuhakikisha Hamis anasaidiwa na Rais wetu amesikia na leo amepokelewa Muhimbili kwa ajili ya kupata matibabu.Pia tunamshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa jitihada zake za kumsaidia Hamis,"amesema Steve Nyerere.
Amesisitiza kuna kila sababu ya kumsaidia Hamis kwani bado anayo matumaini na vijana wenzake wakiwamo wao wasanii wamejikusanya kumsaidia.
Kuhusu gharama ya matibabu,Steve Nyerere amesema bado hajafahamu gharama halisi itakayotumika katika matibabu ya kijana huyo lakini wanachoamini nafasi ya kupona ipo, hivyo kikubwa ni watanzania kumsaidia.
Ametoa onyo kuwa ugonjwa wa Hamis usitumike vibaya kwani wanaweza kujitokeza watu na wakatoa namba za simu ili wawe wanatumiwa fedha kumbe ni matapeli."Hamis anahitaji kusaidiwa na si kutumika kibiashara."
Toa Maoni Yako:
0 comments: