Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shana akiwaonyesha waandishi wa habari noti bandia ambazo zilikamatwa juzi eneo la Mjini Kati jijini Arusha.
Dola bandia zilizokamatwa jijini Arusha, baada ya Askari Polisi kuweka mtego na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili
Na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha

Jeshi la Polisi mkoani hapa Machi 21,2019 lilifanikiwa kuwakamata watu wawili ambao ni Ladislaus Peter Mkimu na William Ngalivuva wote wakazi wa jiji la Arusha kwa tuhuma za kupatikana na noti bandia.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi (ACP) Jonathan Shana, alisema kwamba tukio hilo lilitokea muda wa saa 4:00 Asubuhi katika eneo la Mjini Kati jirani na hospitali ya Saint Thomas.

“Mara baada ya kupata taarifa toka kwa msiri, askari wetu walianza kufuatilia na walipogundua waliweka mtego uliofanikisha kuwakamata watuhumiwa hao, ambao awali walikutwa na kiasi kidogo cha noti hizo na katika mahojiano watuhumiwa hao walikiri kuwa na noti nyingine kwenye makazi yao eneo la Lemara ambapo zilipatikana noti 1,697’’. Alisema Kamanda Shana.

“Jumla ya noti hizo bandia zilizopatikana ni Dola 16,200 zenye thamani ya fedha za kitanzania Shilingi 37,260,000 na zingeweza kuleta athari kubwa katika uchumi wa nchi yetu”. Aliongeza Kamanda Shana.

Aidha alitoa onyo kwa wahalifu wa aina hii kwamba Jeshi la Polisi lipo macho saa Ishirini na Nne na litaendelea kufanya msako wa nyumba kwa nyumba ili kuwakamata wahusika pamoja na mitambo yao.

Mimi kama Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha nitahakikisha kabla ya wananchi wa mkoa wa Arusha pamoja na Watalii hawajaingiwa hofu juu ya watu wa namna hii sisi tutakuwa tumeshawachukulia hatua”.
“Wale wanaopenda kuvuna pasipo kupanda, wanaopenda kutawanya pasipo kukusanya mwisho wao umefika”. Alionya Kamanda Shana.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: