Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Richard Kayombo akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu Makusanyo ya kodi kwa kipindi cha miezi sita kwa Mwaka wa Fedha 2018/19, katika Ofisi za TRA Makao Makuu Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Richard Kayombo akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu Makusanyo ya kodi kwa kipindi cha miezi sita kwa Mwaka wa Fedha 2018/19, katika Ofisi za TRA Makao Makuu Jijini Dar es Salaam. (PICHA NA BENEDICT LIWENGA).

Na Veronica Kazimoto, Dar es Salaam.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi trilioni 7.9 kwa kipindi cha miezi sita ya Mwaka wa Fedha 2018/19 ikiwa ni kuanzia Julai hadi Desemba, 2018 ikilinganishwa na shilingi trilioni 7.8 ambazo zilikusanywa kipindi kama hicho katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Richard Kayombo amesema makusanyo ya mwezi Desemba, 2018 yaliongezeka kuzidi makusanyo ya miezi yote iliyopita kwa mwaka huu ambapo TRA ilikusanya jumla ya shilingi trillioni 1.63.

“Mbali na makusanyo hayo ya mwezi Desemba, katika mwezi Novemba, 2018 TRA ilikusanya jumla ya shilingi trillioni 1.21 na mwezi Oktoba, 2018, zilikusanywa jumla ya shillingi trillioni 1.29. Nachukua fursa hii kuwashukuru walipakodi wote kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari na wakati”, alisema Kayombo.

Kayombo aliongeza kuwa, katika kutatua kero na malalamiko mbalimbali ya walipakodi, uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania umeamua kwamba, kila siku ya Alhamisi itakuwa ni siku maalum kwa ajili ya Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa TRA kote nchini kuwasikiliza na kutatua changamoto za walipakodi.

“Pamoja na kutenga siku hiyo maalum, tumeanzisha Kituo cha Ushauri kwa Walipakodi kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambacho kipo katika Jengo la NHC kwenye makutano ya Mtaa wa Samora na Bridge kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuwa karibu na walipakodi. Tumeanza kwa Dar es Salaam lakini vituo hivi vitaendelea kufunguliwa katika mikoa mingine nchini”, alieleza Mkurugenzi Kayombo.

Aidha, Kayombo amewakumbusha wamiliki wa majengo kote nchini kulipia Kodi ya Majengo ambayo viwango vyake ni shilingi 10,000 kwa nyumba za kawaida, shilingi 50,000/= kwa kila sakafu ya ghorofa na shilingi 20,000 kwa ghorofa za wilayani na vijijini.

“Sambamba na kuwakumbusha wamiliki wa majengo kulipia kodi ya majengo, napenda kuchukua fursa hii kuwasisitiza wafanyabiashara wadogo wadogo kuchangamkia vitambulisho vya wamachinga ambavyo vinapatikana nchi nzima katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa shilingi 20,000/=. Vitambulisho hivyo ni maalum kwa wale tu ambao mauzo yao ghafi hayazidi shilingi 4,000,000/= kwa mwaka”, alisisitiza Kayombo.

Mkurugenzi huyo wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Richard Kayombo ametoa wito kwa walipakodi na wananchi wote kwa ujumla kuendelea kulipa kodi kwa hiari na wakati na kusema kuwa, TRA imeanza kampeni rasmi ya usajili wa walipakodi wapya kote nchini kwa kuwapatia Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) bure katika maeneo wanayofanyia biashara.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: