Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Edwin Mwanzinga akimkabidhi funguo ya pikipiki Mtendaji wa Kata ya Lugenge Khadija Lutumo wakati wa utoaji wa mkopo wa pikipiki kwa watendaji wa Kata Halmashauri ya Mji Njombe
Mkuu wa idara ya Utumishi na Utawala Halmashauri ya Mji Njombe Abdulatif Mkata akizungumza jambo wakati wa makabidhiano ya pikipiki hizo.Kushoto kwake ni watendaji wa Kata katika Halmashauri ya Mji Njombe
Wajumbe wa Kamati ya fedha na wataalamu wa Halmashauri ya Mji Njombe wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya makabidhiano ya pikipiki hizo.
Hyasinta Kissima- Afisa Habari ,Halmashauri ya Mji Njombe.
Halmashauri ya Mji Njombe imekusudia kutatua changamoto ya upungufu wa vitendea kazi kwa watendaji wa Kata katika Halmashauri hiyo kwa kuwakopesha pikipiki.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya pikipiki hizo kwa watendaji wa Kata za Lugenge, Matola, Ihanga na Kifanya Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala Halmashauri ya Mji Njombe Abdulatif Mkata amesema kuwa lengo la Halmashauri kuwakopesha pikipiki hizo ni kutoa motisha kwa watendaji waliofanya vizuri katika utendaji wao wa kazi na kurahisisha utendaji kazi wa watendaji hao wa Kata kwa kuwa Kata wanazozisimamia ni kubwa na pikipiki hizo zitawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa urahisi kwa kuweza kufika kwenye Vijiji vya Kata na kufanikisha utoaji wa huduma kwa jamii kwa wakati.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Edwin Mwanzinga amewataka watendaji hao kuhakikisha kuwa wanazitunza pikipiki hizo na kuhakikisha kuwa zinatumika kwa ajili ya ufuatiliaji wa mapato ya Halmashauri na usimamizi wa shughuli za maendeleo katika Kata zao.
“Kwanza natoa pongezi kwa kazi nzuri mlizofanya katika Kata zenu. Pikipiki hizi tumewapatia kama mkopo ili muweze kuzitunza kwani utakapo maliza mkopo wewe ndio utakua mmiliki halali wa pikipiki hizi. Ni matumaini yangu kuwa sasa mtaenda kusimamia shughuli za maendeleo ya Kata kwa urahisi lakini kubwa zaidi kusimamia mapato ya Halmashauri kikamilifu.”Alisema Mwanzinga.
Khadija Lutumo ni Mtendaji wa Kata ya Lugenge Halmashauri ya Mji Njombe ambaye ni miongoni mwa watendaji waliokabidhiwa pikipiki hizo ambapo ameishukuru Halmashauri kwa kutoa motisha ya pikipiki kwani itasaidia kutatua changamoto ya uhaba wa vitendea kazi na ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika Kata yake na kusimamia mapato kikamilifu kwani kwa kutumia pikipiki aliyokabidhiwa swala la usimamamizi litakuwa rahisi.
Halmashauri ya Mji Njombe imefanikiwa kununua pikipiki nne zenye thamani ya Shilingi milioni tisa laki 4 kupitia mapato ya ndani na imekusudia kuhakikisha kuwa katika siku za mbeleni watendaji wote watakaofanya vizuri katika maswala ya utendaji kazi na ukusanyaji mapato wanakopeshwa pikipiki kwa kutenga bajeti na kuhakikisha Mazingira ya kazi ya watumishi wake yanaboreka siku hadi siku.
Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Mji Njombe ni miongoni mwa Halmashauri za Miji zinazofanya vizuri katika swala la ukusanyaji mapato na imejizatiti kuhakikisha kuwa kadri siku zinavyosonga mbele ikusanye zaidi ya malengo yaliyokusudiwa na kuibuka kinara katika makusanyo ya mapato.
Toa Maoni Yako:
0 comments: