Dereva wa Bohari ya Dawa (MSD), Mkoa wa Mtwara, Bonventure Chacha Magesa, akishusha maboksi ya dawa kwenye Zahanati ya Kijiji cha Minyembe kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara DC mkoani Mtwara jana.
 Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Minyembe, Seleman Ismail (kulia), akisaidia na Wajumbe wa Kamati ya Afya wa Kijiji cha Minyembe kubeba maboksi ya dawa wakati wakizipokea kutoka MSD. Katikati ni Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Salum Dalanga na Mstafa Chindutu.
 Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Salum Dalanga, akipanga maboksi yenye dawa.
Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD, Florida Sianga (kulia),akisaidia kupanga dawa kabla ya kuzikabidhi.

 Dawa na mikoba maalumu yenye vifaa vya kujifungulia wajawazito ikipangwa kabla ya makabidhiano katika Zahanati ya Minyembe.
 Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD Mkoa wa Mtwara, Larisa Manyahi (kushoto), akikabidhi dawa kwa wajumbe wa kamati ya afya wa Kijiji cha Minyembe.
 Mkazi wa Kijiji cha Mkutimango, Mussa Nkala, akizungumzia upatikanaji wa dawa katika zahanati ya kijiji hicho.
 Muuguzi wa Zahanati ya Mkutimango, Farida Mchopa akisaidia kupokea boksi la dawa kutoka kwa Dereva wa Bohari ya Dawa (MSD), Mkoa wa Mtwara, Bonventure Chacha Magesa.
 Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD Mkoa wa Mtwara, Larisa Manyahi (kushoto), akisaidia kuhesabu mifuko maalumu yenye vifaa vya kujifungulia wajawazito kabla ya kuikabidhi Zahanati ya Mkutimango.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mkutimango, akizungumzia upatikanaji wa dawa katika zahanati hiyo.

Na Dotto Mwaibale, Mtwara DC

WANANCHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara DC wameipongeza Serikali kwa kuwapekea dawa, vifaa tiba na vitendanishi jambo ambalo limewaondolea usumbufu wa kupata matibabu wanapoumwa.

Pongezi hizo walizitoa kwa nyakati tofauti wilayani humo jana wakati wakizungumza na waandishi wa habari pamoja na maofisa wa Bohari ya Dawa (MSD), katika vijiji vya Mkutimango na Minyembe ambao wanawatembelea wateja wao kujua changamoto zao ili kuzitafutia ufumbuzi.

Mkazi wa Kijiji cha Mkutimango, Mussa Nkala alisema anaipongeza MSD na Serikali kwa kufanikisha kuwafikishia dawa kwa wakati tofauti na miaka ya nyuma ambapo walikuwa wakilazimika kwenda kuzinunua katika maduka ya watu binafsi.

" Watu katika familia yangu wakiumwa huwa nawaleta kutibiwa katika Zahanati yetu hii Mkutimango na hakuna siku waliyokosa dawa ingawa mimi mwenyewewe nikiumwa natumia dawa za asili kujitibu" alisema Nkala.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mkutimango alisema hapo awali waliweka utaratibu wa wananchi wakiumwa wanakwenda kumuita nyumbani kwake na yeye uwasindikiza kwenda kutibiwa kwenye zahanati hiyo kwa ajili ya usalama wa wauguzi na dawa na vifaa vingine.

"Zamani tuliweka utaratibu huo lakini hivi sasa baada ya kupata mlinzi huwa wanaenda moja moja kutibiwa bila ya kupitia nyumbani kwangu" alisema.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa yeye na familia yake wanapoumwa huwa wanaenda kutibiwa kwenye zahanati hiyo na kuwa miezi michache iliyopita alijikata kidoleni na panga ambapo alipatiwa matibabu kwa haraka na sasa amepona jereha hilo.


Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Minyembe, Salum Dalanga alisema hivi sasa hakuna changamoto ya upatikanaji wa dawa kwenye zahanati hiyo dawa na mahitaji mengine yanayohusu afya yanapatikana.

Mjumbe wa Kamati ya Afya ya Kijiji cha hicho, Mstafa Chindutu alisema mara kwa mara wamekuwa wakipokea dawa kutoka MSD na kuzipokea kwa utaratibu uliopo na orodha ya dawa zote wanazozipokea na thamani yake hubandikwa kwenye ubao wa zahanati hiyo ili kila mwananchi aweze kuona.

Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo ya Minyembe, Seleman Ismail alisema dawa zote muhimu  wamekuwa wakizipata kwa wakati na hawajawahi kupungukiwa kutokana na utaratibu waliojiwekea wa kutoa oda pale wanapoona zinapungua na kuwa katika eneo hilo ugonjwa unaosumbua zaidi ni malaria.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Jully Maleko alisema hivi sasa upatikanaji wa dawa vifaa tiba na vitendanishi vya maabara mkoani humo ni asilimia 97 ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo ilikuwa  chini ya asilimia 40.

Ofisa Uhusiano Mkuu wa MSD, Etty Kusiluka alitoa mwito kwa vituo vya afya, zahanati na Hospitali mkoani humo kujiunga na mfumo maalum wa kieletroniki utakao wasaidia kujua upatikanaji wa taarifa muhimu za upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara na bei zake, taarifa za akaunti zao na taratibu za maombi ya bidhaa wanazo hitaji kutoka MSD. 

Alisema mfumo huo unajulikana kama“MSD-Customer Portal” unaweza kutumika na wateja wake popote walipo nchini na kuwaondolea usumbufu waliokuwa wakiupata awali wakati wakuagiza dawa, ambapo ili walazimu kusafiri ofisi za Kanda ya MSD inayowahudumia au kupiga simu ili kupata taarifa hizo na nyinginezo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: