Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) , Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam wakati alipokutana nao kuelezea malengo yao tokea wameingia katika DAWASA mpya ambayo imeziunganisha mamlaka mbili. Picha zote na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Mawasiliano wa DAWASA, Nelly Msuya akitoa machache.
Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) imezindua kampeni mpya iitwayo 'Tunawahitaji' ambayo italenga kuwarudishia maji wateja waliokatiwa kutokana na kushindwa kulipa bili (wadaiwa sugu).
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja amewsema kampeni hiyo ina lengo la kuwarudishia maji wale wote waliokatiwa kutokana na kutokulipa bili kwa muda mrefu.
"Nimewaagiza mameneja wawarudishie maji wote halafu walipe bili za mwezi mmoja na baada ya hapo wakubaliane watalipa kwa miezi mingapi madeni ambayo wanadaiwa," alisema Luhemeja.
Amesema kuwa kuna wateja takriban 10,000 walikatiwa maji kipindi cha miaka iliyopita hivyo wanawataka wajitokeze ili warejeshewe huduma hiyo.
"Nimeagiza watu wa utawala wafanye hivyo haraka.'Tunawahitaji', malengo ni kutoka nje ya box kuanza kuwatafuta wateja ili tuwaunganishe maji, na hii ni kampeni ya kudumu," alisisitiza.
Malengo mengine ya kampeni hiyo ni kupunguza upotevu wa maji kufikia asilimia 9, kupeleka maji katika maeneo yote pamoja na kukusanya fedha ili Dawasa iweze kujiendesha.
"Dawasa sasa hivi imekuwa ni taasisi kubwa. Asilimia 35 ya mapato yetu yanaenda kwenye maendeleo....tuna miradi ya maji tunaitekeleza Kisarawe, Mkuranga, chalinze na Mlandizi kwenda Chalinze hivyo itategemea tuwe na fedha za kutosha.
"Hivyo kampeni hii pia ina lengo la kurudisha imani kwa wateja, kuunganisha huduma kwa maeneo ya Kiluvya na Kigamboni, pia kampeni imelenga kuwafikia wananchi wa kawaida, hivyo kama kuna mfanyakazi wa Dawasa anawasumbua wananchi wapige simu tutawashughulikia," alisema Luhemeja.
Kwa upande wa Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Mawasiliano wa DAWASA, Nelly Msuya amewashukuru wanahabari kwa namna ambavyo wamezidi kuwa pamoja katika kuwapasha habari wananchi.
"Kikubwa nawaomba ushirikiano huu tulionao uzidi kudumu maana kiukweli mmekuwa kiungo muhimu katika mamlaka yetu," amesema Nelly.
Toa Maoni Yako:
0 comments: