Wazee wa Wilaya ya Gairo wakipita mbele ya Mkuu wa Wila ya Gairo aliyemwakilisha mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe.
---
Tanzania ni kati ya nchi zilizosaini mkataba wa Umoja wa Mataifa mwaka 1982, ambapo dira ya kimkakati ya utoaji wa huduma na ushirikishwaji wa wazee katika maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla uliwekwa bayana.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Siriel Shaidi Mchembe akimwakilisha mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Dkt. Kebwe Steven Wilayani Gairo ambapo maadhimisho hayo yalifanyika ki Mkoa.

Mhe. Mchembe kwa niaba ya Mhe. Dkt. Kebwe alieleza kuwa Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kupitisha sera ya wazee mwaka 2003. Nchi ya kwanza ni Mauritius. Hii inaonesha jinsi nchi yetu inavyowaenzi, kuwaheshimu na kuwathamini wazee.

Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli imejipambanua kwa kuwajali wazee na ndio maana wameundiwa Wizara maalumu inayohusika na ustawi wa wao.

Kauli mbiu ya mwaka 2018 ni  “ Wazee ni hazina ya Taifa, tuenzi juhudi za kutetea haki na ustawi wa wazee" .

Akihutubia katika maadhimisho hayo, Mhe. Mchembe alieleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na Mkoa wa Morogoro katika kuenzi ustawi wa wazee.
 Mkoa umeweza kutambua wazee 200,679 ambapo wanawake ni 104,566 na wanaume ni 96,064.

Mpaka sasa wazee waliopata vitambulisho ni 37,809, wanawake 20,392 na wanaume 17,417.

Mpaka sasa Mkoa umeunda ma Baraza ya wazee 1.011 ambapo Wilaya ya Gairo na Ifakara imeunda mabaraza hayo kuanzia ngazi ya Kitongoji, Kijiji, Kata hadi Wilaya.

Wazee waliopata msamaha wa matibabu ni 4,116 wanaume ni 1,925 na wanawake 2,191 na jumla ya gharama ni Tshs. 12,774,208/-.

Hospitali zote, vituo vya afya mpaka Zahanati zina madirisha ya wazee. Kauli mbiu ya mpishe mzee apate huduma kwanza inazingatiwa kikamilifu.
 Mhe. Mchembe aliwaagiza Wakurugenzi wote Mkoa wa Morogoro kuhakikisha madirisha haya yanafanya kazi ipasavyo. Wasome Sera ya Wazee na kuielewa na kuitekeleza ipasavyo. Maagizo ya Sera yapo pia kwenye taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM 2015/20.

Wakurugenzi ambao hawajakamilisha kuunda Mabaraza ya Wazee wafanye hivyo mwisho Desemba 2018 kama Wazee walivyoomba.

Aidha Mhe. Mchembe aliwaagiza Wakuu wa Wilaya waangalie namna watakavyoweza kuwezesha uandishi wa Historia za Wilaya zao ili kuhakikisha utamaduni wa maeneo yao unarithishwa. Wazee hawa wana mambo mengi na mazuri vichwani, hata hivyo yasipowekwa kwenye vitabu hayatawezwa kurithishwa kwenye vizazi vijavyo.

Ni wakati sasa kuwa na vitabu vyenye kuelezea historia ya kijamii na kiuchumi kwenye maeneo yetu. Vijana wetu wengi ni weupe kwenye maeneo haya.

Mhe. Mchembe aliwapongeza wazee wa Mkoa wa Morogoro kwani kupitia busara na hekima zao chini ya uongozi thabiti wa Mkuu wa Mkoa Mhe. Dr. Kebwe wameweza kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji iliyokuwa ikitesa Mkoa wa Morogoro. Ushirikishwaji wa wazee umechangia sana katika hili.
 Wazee wakimsikiliza  Mhe. Mchembe.

 Mwisho Mhe. Mchembe aliwaonya wote wanaowafanyia wazee vitendo vya ukatili kwa kuwanyanyasa, kuwatenga na kuwaua kwa imani potofu za uchawi na kufunga mvua, Serikali itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi yao.

Uharibifu wa mazingira ndio unasababisha ukosefu wa mvua na sio kuwa kuna wazee wachawi wamefunga mvua. Mhe. Mchembe aliwauliza wazee wanakumbuka wamepanda miti mingapi mpaka umri wa uzee walionao leo, wengi wakasema hawakumbuki na alipowauliza wamekata miti mingapi wakasema ni mingi sana hawajui idadi. Mhe. Mchembe aliwaambia hilo ndilo tatizo linalosababisha mvua zipungue. Bado nafasi ipo wazee wakisimamia zoezi la kupanda miti tutaweza kuokoa mazingira yetu.

Mhe. Mchembe aliagiza Halmashauri zote ambazo hazijatekeleza zoezi la kutambua wazee na kuwapatia kadi za matibabu bila malipo zifanye hivyo mara moja. Mwakani kwenye sherehe kama hizi tupate picha kamili ya Mkoa wetu wa Morogoro.

Kwa upande wa wazee ukiongozwa na Mzee Msemembo, Mwenyekiti wa Wazee Gairo Bw. Yahya Kombo na timu ya 'Help Age Int' waliweza kutoa taarifa ya nini wamefanya na namna wanavyoitegemea Serikali kutatua changamoto zote zinazowakabili zikiwemo uhaba wa dawa za magonjwa ya wazee, kadi za wazee, matibabu bure na Pensheni Jamii.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wazee zaidi ya 300. Mhe. Mchembe alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji Bi. Agnes Mkadya na wafadhili wote waliofanikisha maadhimisho hayo. Kwa kweli maadhimisho yamefana sana sana. Wazee wamekusanyika kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Morogoro. Tumeona wazee wakifanya mazoezi, maigizo, ngoma, ngonjera, kuvuta kamba, kwaya na shairi.

Mwisho Mhe. Mchembe na Bi. Mkandya waliongoza kuwagawia wazee chakula kwani wao ndio wageni rasmi na leo ni siku yao.

Hongera wazee wote Mkoa wa Morogoro kwa sherehe njema, tunaendelea kuwaombea na kuwatakia uzee mwema.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: