Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)

Serikali imetatua tatizo la kuwepo kwa karatasi za risiti zinazofutika maandishi zinazotolewa na Mashine za Kielektroniki za kutolea Risiti (EFDs) kwa kuwataka wafanyabiashara wote kununua karatasi hizo kwa mawakala waliothibitishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Tanga Mjini Mhe. Mussa Bakari Mbarouk, aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu risiti zinazotolewa na Mashine za EFDs kufutika maandishi kwa muda mfupi na muda ambao utatolewa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kurekebisha hali hiyo.

Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alieleza kuwa Serikali inatambua kuwa kuna karatasi feki, lakini tatizo la kufutika kwa risiti halihitaji kutoa muda kwa TRA wa kufanya marekebisho kwa kuwa Serikali ililifanyia kazi, hivyo ni jukumu la wafanyabiashara kufuata maelekezo ya ununuzi wa karatasi hizo kwa wakala waliothibitishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Naibu Waziri Kijaji, akijibu maswali ya Msingi ya Mbunge huyo aliyetaka kujua bei halisi za Mashine ya EFDs na kwa nini Serikali isitoe Mashine hizo bure kwa wafanyabiashara, alisema kuwa kuna aina tano za Mashine ambazo mfanyabiashara anaweza kununua kulingana na mahitaji yake.

“Mashine za EFDs ni kama Rejista za kielektroniki za kodi (ETR) ambayo bei yake ni Sh. 590,000 na hutumiwa na wafanyabiashara wasiotumia mifumo ya Kompyuta na kihasibu na Mashine za kielektroniki zinazoweka alama/saini (Electronic Signature Devices) ambazo hutumiwa na walipa kodi wanaotumia mifumo ya kompyuta na kihasibu, bei yake ikiwa ni kati ya Sh. 1,000,000 hadi 1,200,000”, alieleza Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa Mashine nyingine ni Printa za kielektroniki za kodi (Electronic fiscal printers) ambazo hutumia mfumo maalum wa kompyuta, bei yake ikiwa ni kati ya Sh. 1,500,000 hadi Sh. 1,700,000, pia zipo mashine ya Printa za Pampu za Mafuta ya Petroli au Dizel (EFPP) ambazo hutumiwa na wafanyabiashara wa mafuta, bei yake ikiwa ni Sh. 6,000,000 ikijumuisha gharama za ufungaji na uunganishwaji kwenye pampu za mafuta.

Aidha kuna Mashine ya Printa za Maduka ya kubadilisha Fedha za Kigeni, bei ya mashine hizo ni Sh. 2,150,000 ikiwa ni pamoja na program ya mfumo wa software.

“Ubora wa Mashine hizo ni lazima uthibitishwe na Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA kabla mashine hizo hazijaingizwa sokoni na kuanza kutumika”, alifafanua Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji alisema kuwa wafanyabiashara wasiosajiliwa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) wanaponunua mashine za EFDs hulipa gharama za ununuzi wa mashine hizo na baadae Serikali hurejesha gharama kwa kumruhusu mlipakodi kujirejeshea fedha zake kwa utaratibu wa Input- Output tax kwenye mauzo ya mwezi husika.

Vilevile kwa wafanyabiashara wasiosajiliwa kwenye VAT na wanaoandaa hesabu za mizania, hujirejeshea gharama za ununuzi wa mashine kwa kuingiza gharama husika kama gharama za kuendesha biashara kwa mujibu wa sheria ya Kodi ya Mapato.

Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa, kwa wafanyabiashara wasioandaa hesabu za mizania wanajirejeshea gharama za mashine kwenye kiasi cha kodi walichokadiriwa kwa mwaka husika na iwapo hawatakuwa wamejirejeshea kwa asilimia miamoja, kiasi kilichobakia kitasogezwa mwaka unaofuata.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: