Na Mwandishi wetu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vya siasa, wagombea, wananchi na watendaji wa uchaguzi kuzingatia na kuheshimu matakwa na masharti ya Sheria za Uchaguzi, Sheria za Nchi na Maadili ya Uchaguzi wakati wa upigaji kura, kuhesabu, kujumlisha kura, na kutangaza matokeo katika uchaguzi mdogo utakaofanyika kesho Jumapili kwenye majimbo ya Ukonga na Monduli na kata 9 za Tanzania Bara.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage katika risala yake kuelekea uchaguzi huo mdogo unaofanyika kufuatia sababu mbalimbali ikiwamo wabunge na madiwani kujizulu, kufariki, kutohudhuria vikao na kufutwa uanachama.
Jaji Kaijage aliwataka wadau hao wa uchaguzi kushirikiana na Tume kuhakikisha kuwa viashiria vya kuvunjika kwa amani na utulivu vinaepukwa ili uchaguzi utakaofanyika uwe huru, wazi na wa haki.
Mbali na wito huo, Mwenyekiti huyo aliwasihi wapiga kura wote waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na wanaoishi kwenye maeneo yanayofanya uchaguzi mdogo, kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuwachagua viongozi wanaowataka wawaongoze kwa kipindi cha takribani miaka miwili ijayo.
“Wananchi wafanye na kutekeleza zoezi la kuwachagua wawakilishi wao bila hofu, woga, wasiwasi au ushawishi kwani chini ya Kanuni ya 3.1 (b) ya Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, Serikali imepewa wajibu wa kuhakikisha kuwa kuna hali ya usalama, amani na utulivu katika kipindi chote cha Uchaguzi.”, aliongeza Jaji Kaijage na kusisitiza kuwa:
“Ni matumaini ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa, hali ya amani na utulivu kwenye maeneo ya Uchaguzi ambayo imekuwepo hadi hivi sasa, itaendelea kudumishwa ili kuhakikisha uchaguzi huu mdogo unafanyika na kumalizika salama kwa ustawi wa Taifa letu.”
Alivikumbusha vyama vya siasa na wagombea kuwa mwisho wa mikutano ya kampeni ni leo saa kumi na mbili kamili (12:00) jioni na baada ya muda huo, vyama, wagombea na mashabiki wasifanye kampeni za aina yoyote, kama vile kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni, vipeperushi, bendera, mavazi na vingine kwa kuwa kesho ni siku ya uchaguzi.
“Pale panapokuwa na malalamiko yoyote ya ukiukwaji wa Sheria na Taratibu za Uchaguzi, malalamiko hayo yafikishwe kwenye mamlaka inayohusika kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa Sheria. Vivyo hivyo, viongozi wa vyama vya siasa, wagombea au wafuasi wao na wananchi kwa ujumla wajiepushe na vitendo vinavyoweza kusababisha fujo au vurugu katika vituo vya kupigia, kuhesabia na kujumlishia kura”, alisema.
Jaji Kaijage aliwataka wapiga kura kuondoka kituoni na kwenye maeneo ya kituo cha kupigia kura mara baada ya kupiga kura yake kwa kuzingatia tafsiri sahihi ya Kifungu cha 104 (1) kikisomwa pamoja na Kifungu cha 72(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania kwenye Shauri la Madai Anuai (Misc. Civil Cause No. 37 la mwaka 2015) mpiga kura.
Aliongeza kuwa mbali ya wale ambao Sheria za Uchaguzi zinawaruhusu kuingia na kuwepo kwenye vituo vya kupigia kura, wananchi wanatakiwa kujiepusha na mikusanyiko au mikutano katika maeneo ya vituo vya kupigia kura na vyama vya siasa vimeweka mawakala vituoni ambao watalinda maslahi ya vyama husika na wagombea wao.
Alikumbusha kuwa wanaoruhusiwa kuingia kwenye Vituo vya kupigia, kuhesabia na kujumlishia kura ni wale tu walioainishwa kwenye kifungu cha 72(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na kifungu cha 63(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Alivitaka vyama siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi huo kuweka mawakala katika vituo vyote vya kupigia na kujumlishia kura kwa utaratibu ambao vilikubaliana na Tume tarehe 10/07/2018 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Alivikumbusha kuwa mawakala hao wanaruhusiwa kuwepo katika vituo vya kupigia kura na wanatakiwa kufuata na kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zinazoongoza Uchaguzi katika kipindi chote cha kupiga, kuhesabu, kujumlisha kura na kutangaza matokeo.
Jumapili ya tarehe 16 Septemba, 2018, ni Siku ya kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Majimbo ya Ukonga katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam, Monduli katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli mkoani Arusha na uchaguzi mdogo wa Udiwani katika Kata Tisa (9) zilizopo katika Halmashauri 5, za mikoa 4 ya Tanzania Bara.
“Uchaguzi huu Mdogo wa Ubunge na Udiwani Tanzania Bara, utahusisha jumla ya wapiga kura 470,936 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kutakuwa na Vituo vya Kupigia Kura 1,143.
Jaji Kaijage aliwakumbusha wapiga kura wa Majimbo ya Ukonga, Monduli na kata zote kuzingatia kuwa upigaji kura utafanyika katika vituo vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambavyo vitafunguliwa saa moja kamili (1:00) asubuhi na kufungwa saa kumi kamili (10:00) jioni.
Alisema iwapo, wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao wamefika kabla ya saa kumi jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura. Mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa kumi kamili (10:00) jioni.
Alisisitiza kuwa watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye Jimbo au Kata husika na wana kadi ya mpiga kura na wale walio wamepoteza kadi zao za kupigia kura au zimeharibika au zimechakaa watumie Pasi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Hata hivyo, alisema mpigakura ataruhusiwa kutumia vitambulisho hivyo mbadala, iwapo tu; atakuwa aliandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2015, jina lake liwe katika orodha ya wapiga Kura katika kituo anachokwenda kupiga Kura na majina yake yaliyopo katika Daftari la Mpiga Kura yafanane kwa herufi, maneno na tarakimu na majina yaliyopo katika kitambulisho mbadala.
Toa Maoni Yako:
0 comments: