Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Dkt. Diocles Ngaiza, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu upatikaji wa dawa kutoka Bohari ya Dawa (MSD), mkoani humo mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mfamasia wa wilaya hiyo, Dominic Malabeja.
Wauguzi wa Zahanati ya Kaisho iliyopo wilayani Kyerwa mkoani Kagera, wakisaidia kubeba maboksi yenye dawa baada ya kupelekewa na Bohari ya Dawa (MSD) wilayani humo mwishoni mwa wiki. Kutoka kulia ni Devotha Maganga, Editha Nyaruzi na Yolanda Joseph.
Jengo la Zahanati ya Kata ya Kaisho.
Taswira ya moja ya Jengo la Kituo cha Afya cha Murongo wilayani Kyerwa.
Afisa Huduma kwa Wateja wa Bohari ya Dawa (MSD), Cornelia Mwillawi (kushoto), akimuonesha fomu maalumu ya kujaza baada ya kukabidhiwa dawa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Murongo, Dkt.Rashid Eid (kulia), baada ya kukabidhiwa dawa mwishoni mwa wiki. Katikati ni Tabibu wa kituo hicho, Denis Rugemalira.
Tabibu wa kituo hicho, Denis Rugemalira (kulia), akijadiliana jambo na Afisa Huduma kwa Wateja wa Bohari ya Dawa (MSD), Cornelia Mwillawi baada ya kukabidhi dawa katika kituo hicho.
Na Dotto Mwaibale, Kyerwa Kagera.
KUTOKUFAHAMU Lugha ya Kiswahili imekuwa ni changamoto kubwa ya upatikanaji wa matibabu katika Kituo cha Afya cha Murongo kilichopo mpakani mwa Tanzania na Uganda wilayani Kyerwa mkoani Kagera.
Hayo yalielezwa na Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dkt. Rashid Eid, mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao walikuwepo mkoani Kagera kuangalia taratibu za usambazaji dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Kagera zinazofanywa na Bohari ya Dawa (MSD)
"Changamoto kubwa tuliyonayo ni wagonjwa wetu tunaowapatia matibabu katika hiki kituo chetu cha afya cha Murongo kutojua lugha ya kiswahili hivyo ulazimika kutumia lugha ya alama kuweza kuelewana kama vile kama mgonjwa anaumwa kichwa basi atashika kichwa na kama tumbo vilevile atashika tumbo" alisema Dkt. Eid.
Alisema katika eneo hilo kunamuingiliano mkubwa wa watu kutokana na kuoleana kwani kuna Waganda waliooa Tanzania na Watanzania waliooa Uganda na kuwa kwa pande zote hizo mbili wananchi wake hawajui kuzungumza kiswahili zaidi ya makabila yao ya Kiganda, Kinyankole, Kihaya na Kinyambo.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo kuna wakati hulazimika kuwaita wafanyakazi wa kituo hicho wanao elewa kiswahili kutafsiri lugha wakati wanapozungumza na mgonjwa ambaye hajui kiswahili ili kubaini ugonjwa wake.
Akizungumzia upatikanaji wa dawa kutoka MSD alisema zinapatikana kwa wakati na kuwa pamoja na kituo hicho kuwepo na muingiliano huo wa watu kutoka nchi jirani ya Uganda hawana ubaguzi wa kutoa huduma kwao
"Kituo chetu kinatoa huduma kwa watu wote bila ya ubaguzi na hatujawahi kupungukiwa dawa kwa vile tunapo agiza dawa tunakuwa na idadi ya pande zote mbili na kuongeza za ziada jambo ambalo limsaidia tusiwe tunapungukiwa kwa dawa zote muhimu" alisema Dkt.Eid.
Alisema katika kituo hicho cha afya kwenye mwezi wa sita wagonjwa wanaotibiwa ni kati ya 50 hadi 80 kwa siku lakini kwa hivi sasa ni wagonjwa kuanzia 20 hadi 40 ingawa hakufafanua kwanini idadi hiyo inapungua katika kipindi hicho.
Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dkt. Diocles Ngaiza alisema upatikana wa dawa katika wilaya hiyo kutoka MSD ni mzuri ukilinganisha na miaka 2015 ambapo walikuwa wakipata asilimia 30 lakini sasa hivi ni zaidi ya 70.
Katika ziara hiyo wilayani Kyerwa MSD ilikabidhi dawa katika Kituo cha Afya cha Murongo na Zahanati ya Kaisho.
Toa Maoni Yako:
0 comments: