WIKENDI hii, nilikuwa nikiendesha gari ndogo kwenye barabara kuu ya Tanzania - Zambia. Nilifika mahali panapouzwa matikiti. Ni matunda niyapendayo mno. Sijawahi kupita mahali hapo nisisimame kuyanunua. Labda tu, niwe apeche-alolo.

Kama ilivyo desturi yangu, wikendi hii, nilisimama. Sikuzima gari. Nilishuka garini. Niliziacha simu zangu ndani ya gari.

Nilikuta kijiwe cha matikiti kina watu wanne. Mwuzaji, kijana mdogo tu. Wengine watatu, ni vijana wakubwa kabisa. Pembeni, magari makubwa matatu ya ujenzi wa barabara yalipaki. Kwa kuwa barabara hii ipo kwenye ujenzi, sipati shida kuelewa kuwa jamaa hawa ni madereva wa malori hayo. Mawili yakiwa na shehena ya kifusi. Moja likiwa tupu.

Niliwajulia hali. Nikawapa pole kwa kazi. Kufanya kazi za ujenzi, ni jasho hasa.

Kisha, kabla sijanunua matikiti niliyoyahitaji, nilimwambia yule kijana awachagulie wale jamaa tikiti zuri.

Kwanza hawakuamini. Pengine, kwa sababu madereva wengi wamepita, wamenunua na kwenda zao.

Jamaa wale walinishukuru mno. Ilikuwa yapata saa nane mchana. Jua kali linawaka. Nilielewa mguso wa shukrani zao. Lakini mimi, niliona nilichofanya ni jambo dogo sana. Kwa sababu, tikiti lenyewe lauzwa shilingi elfu tatu tu!

Nikakata kipande kidogo kwenye lile tikiti. Nikala huku nikiwapigisha stori. Wakati wao wakiendelea nalo, ndiposa nikamwomba mwuzaji kunichagulia matikiti kwa idadi niliyohitaji. Mawili matatu hivi kwa ajili ya zawadi niendako.

Kijana akanichagulia. Nikamwomba anisaidie kuyaweka siti ya nyuma. Tukasaidiana kuyaweka. Kwa kuwa nilikuwa bado na safari ndefu, nikakimbilia porini kuitikia kabisa wito mfupi wa mwili.

Niliporejea, nikaingia garini, nikatoa pesa ili nifanye malipo. Kisha, nikaubamiza mlango kwa nguvu.

Nikaungana na wale jamaa. Walikuwa wameshamaliza tikiti lao. Nikaomba niwaongezee. Jamaa wakakataa wakisema inatosha. Nikawaambia tuchukue hata dogo tule pamoja na mwuzaji.

Ikawa hivyo.

Nikafanya malipo. Nikaagana nao. Nikarudi kwenye gari langu.

Daaah!

Nikakuta milango yote imejiloki! Gari linaendelea kuunguruma kama kawa!

Nilidata. Sijui niielezee vipi hali niliyokuwa nayo. Nilichanganyikiwa. Akili ilikufa ganzi kwa nukta kadhaa. Nikaziona simu zangu ndani ya gari. Nikajua sina ujanja.

Ufunguo wa akiba wa gari ulikuwa zaidi ya kilometa 200 kutoka mahali nilipo. Lakini simu zangu zilikuwa ndani. Kichwani mwangu, sikuwa na namba ya simu ya mtu ambaye angekuwa tayari kufanya hima kuniletea huo ufunguo.

Nilichanganyikiwa!

Jamaa mmoja alikuwa tayari kwenye lori lake mita kadhaa mbali. Mwingine alikuwa ndiyo anapanda gari lake. Mwingine alikuwa anavuka barabara.

Aliyekuwa anavuka barabara kuliendea gari lake aliniona. Akaniuliza nini tatizo. Nikamjibu milango ya gari imejifunga kwa ndani. Nikamwambia sina namna.

Akawaita wenzake.

Wote wakaja, akiwepo kijana mwuza matikiti.

Wakaniambia hapo sina namna. Nikawaomba kama wana nyundo, nivunje kioo. Nilikuwa tayari kwa hasara ya kununua kioo kingine. Siyo tu kununua, bali pia, kuendesha bila kioo cha pembeni hadi niufikie mji ambao pengine ningeweza kununua.

Wakaniambia kuna jamaa kwenye kambi yao anaweza kunisaidia. Kambi yao ilikuwa takribani kilometa tatu kutoka tulipokuwa. Wakampigia simu. Wakamsihi achukue bodaboda kuja kunisaidia.

Jamaa huyo (nalihifadhi jina lake) akaomba kuongea nami. Akaniambia nimsubiri hadi saa 12 jioni akitoka kazini ndipo atakuja kunisaidia. Nilijaribu kumbembeleza, akasema meneja wao yupo, hawezi kutoka.

Wale jamaa hawakukubali nisubiri hadi saa 12 jioni. Kumbuka, ilikuwa saa 8 mchana. Gari lingali likiunguruma taratibu. Jua kali linawaka. Tayari, ninatokwa jasho.

Jamaa mmoja akampigia huyo jamaa aliyepo kambini. Akamsihi sana. Akamwambia amdanganye meneja (kumbuka huyo meneja ni Mchina) ameshikwa ghafla na tumbo la kuhara.

Jamaa akasema hawezi.

Nikamwambia jamaa wacha tutafute jiwe tuvunje kioo. Jamaa akaniambia niwe mpole. Akasema, anajitoa mhanga, anakwenda kambini kumfuata yule jamaa.

Sikuamini.

Jamaa akaondoka akinisihi niwe na subira. Akaliwasha lori lake likiwa na mchanga. Mchanga ambao, kimsingi, alipaswa kwenda kuumwaga saiti. Akaondoka. Wale jamaa wengine wakaniaga kuwa wanakwenda kuendelea na kazi zao. Wakanihakikishia nitasaidiwa.

Nikabaki na yule kijana mwuza matikiti. Akanihakikishia wale jamaa lazima watanisaidia. Nikapata amani moyoni. Nikamwuliza, tukate tikiti jingine? Akaniambia hapana, ametosheka.

Bila shaka, mwuzaji mwingine angejali faida.

Takribani robo saa hivi baadaye, nikaliona lile lori likisimama nyuma ya gari langu. Yule jamaa dereva aliyekuwa akipiga simu kunisaidia, alishuka wa kwanza. Upande wa pili, alishuka jamaa mwingine.

Mkononi alikuwa na bisibisi na waya mgumu mrefu. Nikatambua ndiye mhusika.

"Pole sana bro!" Ndiyo ilikuwa salamu yake. Ikimtoka kwa heshima na unyenyekevu.

"Shukrani sana (nikimtaja jina). Pole kwa usumbufu." Nilisema.

"Siyo usumbufu bro. Hii simpo tu. Sasa hivi utaendelea na safari." Alisema huku akiunyooshanyoosha waya kwa bisibisi.

Niliona hatua zote. Lakini dakika tatu kasoro baadaye, milango ya gari langu ilikuwa wazi!

Ahsante sana Mwenyezi Mungu kwa kunikutanisha na watu hawa.

Walikuwa tayari kupata shida kazini kwao kunisaidia mimi ambaye wala hawanifahamu. Sidhani kama hisani ndogo tu ya kula nao matikiti peke yake, ndiyo imewafanya wanitendee wema mkubwa hivi.

Halafu, hawakuwa tayari niwalipe pamoja na kuwabembeleza sana.

Nimejiuliza maswali mengi njia nzima. Nimepata jibu moja tu, kila jambo hutokea kwa sababu.

Pengine, nimejifunza umuhimu wa kufanya hisani hata kama ni ndogo vipi. Hata kama, unayemfanyia humfahamu, wala hakufahamu. Ama, huna wazo la kuja kukutana naye tena. Hatujui ni wakati gani, itatuletea manufaa makubwa.

Ahsante sana kunisoma.

Fadhy Mtanga,
Iringa, Tanzania.
Jumapili, Septemba 2, 2018.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: