Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemary Senyamle akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya wafanyabiashara iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi. Semina hiyo imefanyika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Diana Masalla akitoa elimu ya kodi wakati wa semina ya wafanyabiashara iliyofanyika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Afisa Maadili Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Adelaida Rweikiza akiwasilisha mada kuhusu Mfumo wa Maadili kwa Watumishi wa TRA wakati wa semina ya wafanyabiashara iliyofanyika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Afisa Kodi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Shaban Makumlo akiwasilisha mada kuhusu Msamaha wa Riba na Adhabu kwenye Malimbikizo ya Madeni ya Kodi wakati wa semina ya wafanyabiashara iliyofanyika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Baadhi ya wafanyabiashara wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa mada mbalimbali wakati wa semina ya wafanyabiashara hao iliyofanyika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro. (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO).
Na Veronica Kazimoto, Same.
Wafanyabiashara Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wamefurahia elimu ya kodi iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikiwa na lengo la kuwaongezea uelewa juu ya Msamaha wa Riba na Adhabu kwenye Malimbikizo ya Madeni ya Kodi, Mabadiliko ya Sheria za Kodi kulingana na Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018 na Mfumo wa Maadili kwa Watumishi wa TRA.
Wakizungumza mara baada ya kumaliza semina hiyo, wafanyabiashara hao wamesema kuwa, wamefurahishwa na elimu waliyoipata kutoka TRA na kwamba itawasaidia katika shughuli zao za kila siku.
"Binafsi leo nimefurahi sana kupata elimu ya kodi ambayo kwa hapa Same tuna takribani mwaka mzima bila kupatiwa elimu hii, kwa kweli ninaomba TRA watupatie semina hizi mara kwa mara ili tuweze kuendesha biashara zetu kwa ufanisi", alisema Regina Msuya ambaye ni Mfanyabiashara wa Vifaa vya Shule na Ofisi.
Msuya ameongeza kuwa, ni muhimu Mamlaka ya Mapato Tanzania iangalie namna ya kuongeza muda wa semina hizo ili waweze kuyapata kwa undani masuala yote yanayohusiana na kodi.
Kwa upande wake Mfanyabiashara anayemiliki Baa wilayani hapa Tizinga Mbogo, mbali na kufurahishwa na elimu ya kodi aliyoipata, ameiomba TRA kushirikiana na ofisi ya Afisa Biashara ili kuondoa changamoto zinazowakabili ambazo utatuzi wake hutegemea ofisi hizo mbili.
"Kwanza kabisa naomba elimu hii iendelee maana tumejifunza mambo mengi mazuri kutoka kwa wenzetu wa TRA, aidha naomba Afisa Biashara ashirikiane na Mamlaka ya Mapato Tanzania hapa wilayani kwetu kwa ajili ya kututalia kero ambazo zinategemea maamuzi ya ofisi hizi mbili," alieleza Mbogo.
Awali akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemary Senyamle, amewahimiza wafanyabiashara wote wenye malimbikizo ya madeni ya kodi yanayotokana na riba na adhabu kuwahi kutuma maombi ya msamaha pamoja na kuwataarifu wenzao wenye madeni kama hayo.
Elimu ya kodi inaendelea kutolewa katika Mikoa ya Kaskazini ambapo baada ya kumaliza Mkoa wa Tanga, sasa elimu hiyo inatolewa katika Mikoa ya kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Toa Maoni Yako:
0 comments: