Na Salome Majaliwa - JKCI.
ULAJI wa vyakula visivyokuwa na afya ni moja ya sababu zinazosababisha watu kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza ukiwemo ugonjwa wa moyo -Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akitoa mada kuhusu afya na mazoezi kwenye mkutano wa wahandisi unaofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Katika mada hiyo ya afya na mazoezi Prof. Janabi alifundisha kuhusu ugonjwa wa shambulio la moyo na kiharusi, tezi dume, saratani, kukoma kwa hedhi na huduma zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
Prof. Janabi ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema hivi sasa watu wanapenda kula vyakula ambavyo ni hatari kwa afya zao zikiwemo chips na bagger badala ya kula kwa wingi matunda na mboga za majani.
“Dhibitini vyakula mnavyokula hii ikiwa ni pamoja na kutokula vyakula vyenye mafuta mengi ambavyo vinapelekea mishipa ya moyo kuziba kutokana na mafuta na kusababisha tatizo la kiharusi pia fanyeni mazoezi ya mara kwa mara”, alisisitiza Prof. Janabi.
Alisema ugonjwa wa moyo ni moja ya magonjwa yanayoua watu wengi wakiwemo watoto ambao wasipopata chanjo za muhimu zinazotolewa chini ya umri wa miaka mitano pia mama mjamzito asipopata chanjo kuna uwezekano mkubwa kwa watoto kuzaliwa na kupata magonjwa ya moyo.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mrutu akimpa dawa ya moyo mhandisi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kupima afya wakati wa mkutano wa 16 wa Wahandisi uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam. Wahandisi waliopima magonjwa ya moyo na kukutwa na matatizo walipewa dawa bila malipo.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakitoa huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wahandisi wakati wa Mkutano wa 16 wa Wahandisi unaofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wahandisi wakiwa katika foleni ya kufanya upimaji wa magonjwa ya moyo katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa Mkutano wa 16 wa Wahandisi ulifanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam. Taasisi hiyo ilishiriki kutoa huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wahandisi hao.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Adela Martine akitoa ushauri kwa mhandisi aliyepata huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo katika banda la Taasisi hiyo wakati wa mkutano wa 16 wa Wahandisi unaofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akitoa elimu ya Afya na mazoezi kwa wahandisi wakati wa Mkutano wa 16 wa Wahandisi uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jana Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali za Sekondari za Jijini Dar es Salaam wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi (hayupo pichani) alipokuwa akitoa mada ya Afya na mazoezi kwa wahandisi wakati wa Mkutano wa 16 wa Wahandisi unaofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
Beatrice Nchimbi ambaye ni Mwanafunzi wa shule ya Sekondari Kisutu akiuliza swali baada ya kupata elimu ya afya na mazoezi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi (hayopo pichani) wakati wa Mkutano wa 16 wa Wahandisi unaofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
Picha na JKCI.
Kwa upande wa ugonjwa wa shambilio la moyo alizitaja dalili zake kuwa ni maumivu kwenye kifua ambayo yanakwenda kwenye mgongo upande wa kulia na kushoto na kuwasihi wanapoona dalili kama hiyo wawahi mapema kwa daktari.
Alizitaja aina za ugonjwa wa kiharusi kuwa ni mshipa unaopeleka damu kwenye ubongo kuziba na kushindwa kusambaza damu (ischemic) na mshipa wa damu kupasuka na kumwaga damu katika ubongo (hemorrhagic) ukipata aina hii ya kiharusi ni ngumu kupona.
Kuhusu ugonjwa wa tezi dume Prof. Janabi alisema wanaume wenye umri wa kuanzia miaka 50 kwenda juu wako katika hatari ya kupata ugonjwa huo na kuzitaja baadhi ya dalili kuwa ni kwenda haja ndogo mara kwa mara hasa nyakati za usiku na ukipata haja ndogo haitoki yote.
Akielezea kuhusu kitendo cha mwanamke kukoma hedhi alisema mwanamke aliyekuwa katika hali hiyo ni yule ambaye hawezi kuzaa tena na wengi wao huwa ni wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea.
Alizitaja dalili za kukoma kwa hedhi kuwa ni pamoja na kupoteza hamu ya kufanya tendo la ndoa, mama kuwa mkali na mwenye hasira, joto la mwili kuwa kali. Ili kukabiliana na kipindi hicho aliwashauri wanawake kufanya mazoezi na kuvaa nguo nyepesi ili kulikabili joto na kuepuka kula vyakula vyenye viungo vikali kama pilipili.
Prof. Janabi alimalizia kwa kuzitaja baadhi ya sababu zinazosababisha ugonjwa wa saratani kuwa ni kutokwenda haja kubwa kwa wakati, kutokupata muda wa kutosha wa kulala, kutokula chakula kwa wakati , msongo wa mawazo na kutokunywa maji ya kutosha.
Toa Maoni Yako:
0 comments: