Bodi ya Wadhamini ya Hifadhi ya Taifa Tanzania (TANAPA) imeidhinisha na kuruhusu matumizi ya bajeti ya mpito ya kiasi cha shilingi 3.9 bilioni zitumike kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi, uendelezaji utalii pamoja na ujenzi wa miundombinu katika Mapori ya Akiba matano yaliyopandishwa hadhi na kuwa Hifadhi za Taifa.
Hatua hiyo imekuja kufuatia tangazo la Serikali la kuyapandisha hadhi Mapori ya Akiba ya Bihalamulo,Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika kuwa Hifadhi za Taifa kupitia kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamisi Kigwangalla alipotangaza Bungeni wakati alipokuwa akihitimisha bajeti ya Wizara mwezi Mei mwaka huu mjini Dodoma.
Ofisa Mwenye Wadhifa wa Mkuu wa Hifadhi, Damian Saru amesema hayo mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Japhet Hasunga wakati alipotembelea mapori hayo ikiwa ni ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Kagera kwa ajili ya kufuatilia hatua za uendelezaji zilizofikiwa na TANAPA katika mapori hayo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri , Mhe.Hasunga amesema ameridhishwa na hatua nzuri iliyofikiwa na TANAPA katika mapori hayo na pia ameupongeza ushirikiano kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ( TAWA) na TANAPA katika hatua ya kutoka kwenye Mapori Akiba na kuwa Hifadhi za Taifa.
Toa Maoni Yako:
0 comments: