Mbunge wa Singida Magharibi, Mheshimiwa Elibariki Kingu, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Makungu waliokuwa na mabango yenye ujumbe wa kero mbalimbali walipo usimamisha msafara wake wakati akipita kijijini hapo akienda kuhutubia mkutano wa hadhara Kata ya Iyumbu wilayani Ikungi mkoani humo jana.

Na Dotto Mwaibale, Singida.

MBUNGE wa Singida Magharibi Mhemiwa, Elibariki Kingu alilazimika kutoa machozi baada ya wananchi wa Kijiji cha Makungu kilicho katika Halmshauri ya Wilaya ya Ikungi kumpokea kwa mabango yenye ujumbe wa kero mbalimbali ambazo alianza kuzifanyia kazi lakini watendaji kushindwa kuzisimamia.

Wananchi hao waliokuwa na jaziba waliusimamisha msafara wake kijiji hapo jana wakati akielekea Kata ya Iyumbu kufanya mkutano wa hadhara ambapo walikuwa na mabango yaliyo kuwa yakielezea changamoto mbalimbali walizonazo.

Changamoto kubwa walizoziandika kwenye mabango hayo ni kutokuwa na shule, maji, zahanati na barabara ya uhakika ambapo walimtaka mbunge awape majibu ya kero hizo.

Akizungumza na wananchi hao Kingu alisema baada ya kuchaguliwa alitoa mifuko ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa zahanati, Shule ya Msingi Makungu pamoja na fedha sh.milioni 70 kwa ajili ya mradi wa maji na kilicho hitajika ni nguvu ya wananchi kuendeleza miradi hiyo.

Baada ya mbunge huyo kutoa maelezo hayo ndipo ilipobainika kuwa saruji iliyotolewa na mbunge huyo tangu mwaka 2016 kwa ajili ya miradi hiyo bado ilikuwa imefungiwa ndani na watendaji wa kijiji hicho bila kuifanyia kazi huku cheki ya sh.600,000 iliyotolewa na Halmshauri ya Wilaya ya Ikungi kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo kwenye kijiji hicho ikipoteza muda wake bila ya fedha kutolewa benki.

"Wananchi wangu mmesikia wenyewe jinsi nilivyo jitahidi kusaidia katika ujenzi wa zahanati na shule kwa kuwaletea saruji sasa hapo mwenye kosa ni nani mimi au watendaji wenu waliofungia saruji ndani kwa muda wote huo bila ya kuzifanyia kazi" alihoji Kingu.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Iyumbu, Kingu aliwataka watendaji hao kufanya kazi badala ya kuwa mzigo kwa wananchi huku akisema ni lazima ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) itekelezwe kwa vitendo kwa kuwaletea maendeleo wananchi na si vinginevyo.

Kingu aliwaambia viongozi hao kuwa wawe na huruma kwa wananchi kutokana na ukubwa wa jimbo hilo kwani kutoka makao makuu ya wilaya hadi katika kata hiyo ambayo ipo mpakani mwa mkoa wa Singida na Tabora ni kilometa 240 ni sawa kutoka Morogoro hadi Dodoma hivyo wasikubali kupoteza bure nguvu za maendeleo kwa ajili ya wananchi kutokana na vifaa vingi vya ujenzi kusafirishwa kwa umbali huo na wao kuvitelekeza bila ya kuvifanyia kazi.

Katika mkutano huo mambo mengi yalijitokeza na sababu ya kukwama kwa miradi hiyo ya maendeleo kuwa kumechangiwa na watendaji wa vijiji na viongozi wa siasa kusigana kwa kuingiliana majukumu yao ya kazi huku diwani wa kata hiyo akishindwa kusimamia miradi hiyo.

Mkutano huo ulikwisha kwa kutiliana saini mkataba wa kumaliza miradi hiyo ambapo Kingu aliahidi kwenda katika kata hiyo kupiga kambi ya siku 10 ili kuhakikisha miradi hiyo inaanza upya kufanyiwa kazi huku akitoa ahadi ya kutoa sh.milioni 5 kutoka mfuko wa jimbo kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa zahanati.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: