Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba (mwenye overall ya bluu) akijadiliana jambo na Ndg. Ildefons Mnimbo ambaye ni mtaalamu kutoka kampuni ya Plasco anaesimamia zoezi la kuunganisha mabomba, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa kuunganisha bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara na lile la kutoka Ubungo kuelekea Mikocheni.
Sehemu ya eneo la barabara ya Ubungo Maziwa inayochimbwa kitaalamu bila kuvunja barabara ili kuruhusu bomba la gesi kuvuka barabara hiyo.
Bomba lenye kipenyo cha 315mm likiwa limelazwa katika mtaro tayari kufukiwa, hii ni sehemu ya bomba linalochukua gesi asilia kutoka kwenye bomba kuu linalotoka Mtwara hadi Dar es Salaam na kuunganisha na bomba linalotoka Ubungo kuelekea Mikocheni.

Na Mwandishi Wetu.

Ni miezi mitatu sasa tangu Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alipozindua rasmi mradi wa kuunganisha bomba kubwa la gesi asilia linalotoka Mtwara hadi Dar es Salaam na bomba la kipenyo kidogo linalotoka Ubungo kuelekea Mikocheni.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mha. Kapuulya Musomba alifafanua kwamba utekelezaji wa mradi huo unalenga kuongeza matumizi ya gesi asilia kwa jiji la Dar es Salaam kwa kuwaunganisha wateja zaidi wa matumizi ya majumbani na viwandani.

Mradi huu unahusisha ujenzi wa msingi kwa ajili ya kusimika mtambo wa kupunguza mgandamizo, uunganishaji wa vipande vya mabomba, kuthibitisha njia ya bomba, uchimbaji na ulazaji wa bomba litakalochukua gesi kutoka bomba kubwa, uwekaji wa viainisho vya bomba linapopita na ujenzi wa daraja la waenda kwa miguu kuvuka mto Ubungo.

Akizungumza juu ya hatua za utekelezaji, Meneja Mradi Ndg. Denice Byarushengo alisema “mradi umepiga hatua kubwa na muhimu ambapo hadi sasa ujenzi wa msingi kwa ajili ya kusimika mtambo wa kupunguza mgandamizo umekamilika kwa asilimia 97%, uthibitisho wa njia ya bomba na zoezi la kuchimba mitaro kwa ajili ya mabomba umekalimilika kwa asilimia 76.8%, uunganishaji wa mabomba umekamilika kwa asilimia 88.6%, ulazaji na ufukiaji wa mabomba umekamilika kwa asilimia 56.9%, viainisho sita (6) vya bomba linapopita vimeshawekwa na ujenzi wa dara la waenda kwa miguu umekamilika kwa asilimia 90%”.

Aidha, Meneja Mradi aliongeza kwamba utekelezaji wa mradi huu unahusisha kuvuka mto Ubungo pamoja na barabara ya Ubungo Maziwa na ya Mandela ambapo hadi sasa kazi ya kuvuka mto Ubungo imekamilika kwa asilimia 100% na ile ya kuvuka barabara ya Ubungo Maziwa imekamilika kwa asilimia 50% wakati ya kuvuka barabara ya Mandela ikiwa mbioni kuanza.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mha. Kapuulya Musomba ambaye alifanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo hapo jana alionyesha kuridhishwa na kazi na ubora wa utekelezaji wa mradi, Mha. Kapuulya alisema “pamoja na changamoto zilizopo, ninayo furaha kwamba kazi zinafanyika kwa kasi na ubora wa hali ya juu na ni matumaini yangu baada ya kuongea na mkandarasi pamoja na msimamizi wa mradi kwamba mradi utamalizika ndani ya wakati”.

Mradi wa kuunganisha bomba kubwa la gesi asilia na lile la Ubungo kuelekea Mikocheni lenye urefu wa kilomita 7.8 na uwezo wa kusafirisha gesi kiasi cha futi za ujazo milioni 7.5 kwa siku unalenga kuunganisha kiwanda cha Coca Cola Kwanza Ltd na BIDCO pamoja na wateja takribani 1000 wa majumbani ambao wataunganishwa kwa awamu.

Mradi huu utawezesha upatikanaji wa gesi asilia ya kutosha katika bomba litokalo Ubungo kuelekea Mikocheni kupitia barabara ya Sam Nujoma kusambaza gesi kwa wateja wa majumbani katika maeneo ya Ubungo, Shekilango, Mlalakuwa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sinza na Mikocheni. Mkandarasi wa mradi huu ni kampuni ya SINOMA kutoka Jamhuri ya Watu wa China na mradi unagharimu shilingi za kitanzania bilioni 4.2 ambazo ni fedha za ndani kutoka TPDC.

Vile vile mradi huu unatoa fursa kwa kampuni za wazawa kutoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuuza bidhaa za ujenzi kama vile mabomba ambapo kwa sasa kampuni ya Plasco ndio mshindi zabuni hiyo. Mkandarasi wa mradi pia ana fursa ya kutoa kazi kwa mkandarasi mwingine (sub-contracting) lengo likiwa ni kuchochea ushirikishwaji wa wazawa katika sekta ya mafuta na gesi hapa nchini.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: