Articles by "HABARI NA MATUKIO"
Showing posts with label HABARI NA MATUKIO. Show all posts

Na Mwandishi Wetu. 

Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Bw. Tido Mhando, amewataka Waandishi wa Habari nchini kutafakari upya wajibu wao katika kuijenga jamii kupitia maudhui yenye tija, akieleza kuwa ipo haja ya kurejesha hadhi na nguvu ya taaluma hiyo katika kujenga fikra na maendeleo ya taifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Bw. Mhando amesema pamoja na JAB kusimamia utoaji wa ithibati kwa kuzingatia vigezo vya elimu na sheria, bado kuna umuhimu wa Waandishi wa Habari kuendelea kujengewa uwezo kupitia mafunzo ya kitaaluma.

“Tukitazama baadhi ya vyombo vyetu vya habari, iwe ni magazeti, redio au televisheni, mambo ya kufikirisha kwa kiasi kikubwa yamepungua. Waandishi wa Habari wanapaswa kutafakari kama hiyo ndiyo taswira wanayotaka kuiacha katika jamii ya Watanzania,” amesema.

Amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuunda mtazamo wa jamii, hivyo kuna wajibu wa kuhakikisha maudhui yanayotolewa yanajenga uelewa, yanakuza maendeleo na yanalinda maslahi ya taifa.

“Tunachosimamia ni kuhakikisha Mwandishi wa Habari anayepata ithibati anakuwa na kiwango cha elimu kisichopungua Diploma, lakini tunataka pia Waandishi wa Habari waendelee kupata mafunzo ili waweze kuimarika zaidi kitaaluma,” amesema.

Amesema ipo haja ya sekta ya habari kutafakari aina ya maudhui yanayopewa kipaumbele, akisisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kujenga fikra na mwelekeo wa jamii.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Rabia Hussein Mohamed kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Immaculata Kajetan Banzi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Cyprian Phocas Mkeha kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Yohane Bokobora Masara kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Dkt. Juliana Laurent Masabo kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Abdi Shaaban Kagomba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.

Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiapa Kiapo cha Maadili kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kuwaapisha Majaji 9 wa Mahakama ya Rufani, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi mbalimbali kwenye picha na Majaji wa Mahakama ya Rufani, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.
Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, Mariam Ibrahim amemshuru Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Taifa , Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kupendekeza jina lake na Kamati Kuu ya chama hicho kulipitisha na hatimaye kushinda kwa kura nyingi.

Ametoa shukrani hizo kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa ,Rais Dk.Samia Suluhu Hassan alipokuwa akisalimia viongozi mbalimbali wa Chama hicho wakati wa Semina ya Uongozi na Maendeleo kwa madiwani wote wanawake  wa Mkoa wa Pwani.

“Nitumie nafasi hii kwa dhati ya moyo wangu kumshukuru Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Taifa Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kunipendekeza mimi na Kamati Kuu kurudisha jina langu na kuja katika Mkoa wa Pwani na kupigiwa kura nyingi.

“Waheshimiwa madiwani hatujaonana toka Uchaguzi mkuu ulivyopita hivyo naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru nyote kwa kura zenu za kishindo.Nasema ahsanteni sana,amesema mbele ya madiwani hao pamoja na viongozi wa Mkoa huo.
 
Amesisitiza ameamua kutoa shukrani hizo kwasababu ndio mara yake ya kwanza wanakutana ambapo ametumia nafasi hiyo pia kuwaaahidi kuendelea kushirikiana nao na yupo tayari kwa wakati wowote ambao atahitahika.“Tutakuwa pamoja katika kila hali.”






Na Mwandishi Wetu

BABATI — Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Babati mkoani Manyara imesitisha kusikiliza kesi ya jinai namba 291 ya mwaka 2026 iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Babati Mjini, Paulina Gekul, inayomkabili Brayton Lucas (17), baada ya kujiridhisha kuwa mshtakiwa huyo ni mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18 na hivyo shauri hilo linapaswa kusikilizwa katika Mahakama ya Watoto kwa mujibu wa sheria.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya Wakili wa upande wa utetezi, Thadei Lister, kuiomba mahakama kujiridhisha kuhusu umri wa mshtakiwa kwa kuwasilisha nyaraka mbalimbali ikiwemo cheti cha kuzaliwa kilichoonesha kuwa Brayton alizaliwa Novemba 12, 2008 na kwa sasa ana umri wa miaka 17 na miezi sita, tofauti na taarifa zilizokuwa katika hati ya mashtaka zilizomtaja kuwa na miaka 19.

Katika shauri hilo, Paulina Gekul alidai kuwa Brayton Lucas, ambaye alikuwa akichunga mifugo yake, alihusika katika wizi wa mbuzi 15 wenye thamani ya shilingi milioni tatu, kosa linalodaiwa kufanyika chini ya kifungu cha 268 cha sheria ya wizi wa mifugo. Kesi hiyo ilikuwa na jumla ya watuhumiwa watatu.

Mahakama pia ilielezwa kuwa mtoto huyo alikuwa amechanganywa katika shauri moja na watuhumiwa watu wazima, jambo ambalo upande wa utetezi ulidai ni kinyume na sheria zinazolinda haki za mtoto.

 Baada ya kupitia nyaraka zilizowasilishwa, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Babati, Ahmed Mgodo, alisema mahakama imejiridhisha kuwa Brayton Lucas ni mtoto na hivyo haina mamlaka ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo. Kutokana na uamuzi huo, mahakama ilisimamisha shauri hilo dhidi ya mshtakiwa huyo na kuagiza polisi kuandaa hati mpya ya mashtaka kwa mujibu wa sheria zinazohusu watoto.

Brayton Lucas alipatiwa dhamana huku washtakiwa wawili wengine wakiendelea kushikiliwa. Wakili Thadei Lister amesema wako tayari kuendelea kumtetea mtoto huyo iwapo atafikishwa katika Mahakama ya Watoto.

Akizungumza nje ya mahakama, Wakili Thadei alisema Brayton ni mwanafunzi wa kidato cha nne ambaye alitoweka akiwa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha na wazazi wake walikuwa wakimtafuta kwa kipindi cha miezi mitatu kabla ya kupata taarifa kuwa amekamatwa Babati kwa tuhuma za wizi.

Mama mzazi wa Brayton alisema mtoto wake alitakiwa kuwa shuleni baada ya kumaliza kidato cha nne na tayari alikuwa amepangiwa shule, lakini aliondoka nyumbani bila kutoa taarifa na baada ya juhudi za muda mrefu za kumtafuta walipata taarifa kuwa alikuwa Babati akifanya kazi.
Wakati huo huo, Diwani wa Kata ya Maruvango Wilaya ya Arumeru Mashariki, Digna Nassari, amesema taarifa za kupotea kwa mtoto huyo zilikuwa zimetolewa polisi miezi mitatu kabla ya kufunguliwa kesi dhidi yake na Paulina Gekul.

Aidha, Digna amesema Brayton ni miongoni mwa watoto 16 kutoka kata hiyo waliotoroka shule, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana kuhakikisha watoto wanarudi katika mfumo wa elimu na kupata ulinzi unaostahili

Pichani, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya wajumbe wa makundi yaliyoshiriki mikutano hiyo, yakiwemo United People’s Alliance (UPA), SSOMA, SPLM-IO, pamoja na People’s Coalition for Civil Action na Federal Democratic Party. Picha na Issa Michuzi

Na Mwandishi Wetu.

Mikutano ya ngazi ya juu iliyohusisha makundi mbalimbali ya upinzani nchini Sudan Kusini imefanyika jijini Dar es Salaam tarehe 21 na 22 Mei, 2026 ikiwa ni sehemu ya juhudi mpya za kufufua mchakato wa amani jumuishi baada ya kusuasua kwa utekelezaji wa makubaliano ya amani ya mwaka 2018.

Mazungumzo hayo yaliongozwa na Rais wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika kwa Ukanda wa Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu.

Majukumu yake makuu yanajumuisha: Upatanishi wa Amani: Kusimamia diplomasia ya kuzuia migogoro na kuongoza mazungumzo jumuishi ili kutatua changamoto za kisiasa na kiusalama katika ukanda huo.

Ushirikiano wa Kikanda: Kufanya kazi kwa karibu na jumuiya na taasisi mbalimbali kama vile IGAD na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kujenga misingi thabiti ya amani na usalama.

Kwa ujumla, mikutano hiyo ilionyesha dhamira ya Umoja wa Afrika na wadau wa kikanda katika kuimarisha mazungumzo ya kisiasa na kuhakikisha mazingira ya amani na utulivu yanaimarishwa kuelekea uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu nchini Sudan Kusini.

Mikutano hiyo pia ililenga kuisaidia Umoja wa Afrika kupata picha kamili ya hali ya kisiasa na kiusalama nchini Sudan Kusini kabla ya uchaguzi uliotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huo wa 2026. 

Na Mwandishi Wetu

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Dotto Kuhenga, ametoa mhadhara kuhusu nafasi ya vyombo vya habari nchini Tanzania na mchango wake kwa jamii kwa wanafunzi na maprofesa kutoka Chuo Kikuu cha Washington and Lee cha nchini Marekani.

Mhadhara huo uliotolewa kwa wanafunzi wa Programu ya Masomo ya Majira ya Kiangazi (Summer School), ulihusisha majadiliano mbalimbali kuhusu vyombo vya habari, jamii na mafunzo katika mazingira ya kimataifa.

Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Facebook, Dkt. Kuhenga alisema kikao hicho kilijaa majadiliano ya kuvutia, maswali mbalimbali pamoja na kubadilishana uzoefu na mitazamo tofauti kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika maendeleo ya jamii.

Alieleza kuwa majadiliano hayo yalitoa fursa ya kujifunza zaidi kupitia maingiliano ya kitaaluma na kuimarisha uelewa kuhusu namna vyombo vya habari vinavyoweza kuathiri jamii katika mazingira ya sasa ya kidijitali.
Aidha, alisema uzoefu huo umekuwa ukikumbusha kuwa ualimu wenye matokeo chanya haujengwi katika kutoa maarifa pekee, bali pia kupitia kusikiliza, kujifunza na kukua kwa pamoja kupitia majadiliano yenye tija.

Mhadhara huo umeonekana kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na kubadilishana uzoefu wa kimataifa katika sekta ya elimu, mawasiliano na vyombo vya habari.
Na Mwandishi Wetu.

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) inahitaji kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 7 ndani ya kipindi cha miaka miwili kwa ajili ya kufanikisha matibabu ya ubingwa bobezi ya upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu pamoja na upandikizaji wa figo kwa wananchi wenye uhitaji mkubwa wa huduma hizo.

Mahitaji haya yametangazwa leo tarehe 21 Mei 2026 katika Ukumbi wa NIMR Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Abel Makubi katika mkutano wake na wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri, Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jumuiya ya Miitandao Tanzania (JUMIKITA).

Alisema kwa sasa kuna watoto 50 wanaohitaji upondikizaji wa uloto na wengine 50 kwa ajili ya upandfikizaji wa figo.

Mkutano huo ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo, hapo Julai 15 ,2026 ambapo safari ya maadhimisho haya ilizinduliwa rasmi mwezi Oktoba mwaka 2025.
Tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo Oktoba 13,2015, Hospitali ya Benjamin Mkapa imekuwa na dhamira ya kutoa huduma za kibingwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika kuzuia, kuchunguza, na kutibu magonjwa mbalimbali, pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya na kufanya tafiti.

Kwa sasa, BMH inahudumia takribani wananchi milioni 10 kutoka mikoa nane ya Tanzania, ikiwa na vitanda 400 na watumishi 1,073, wakiwemo madaktari bingwa na bingwa bobezi zaidi ya 100.

Kwa mujibu wa Profesa Makubi Hospitali hiyo inatoa huduma 20 za kibingwa na huduma 18 za ubingwa bobezi zikiwemo upandikizaji wa viungo, upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua, uchunguzi wa mishipa ya moyo, huduma za radiolojia ya kisasa, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, ubadilishaji wa nyonga na magoti, upasuaji wa njia ya matundu madogo, pamoja na uchujaji wa damu.

Profesa Makubdi amesema ndani ya miaka 10 ya utendaji, hospitali imepata mafanikio makubwa yaliyochangiwa na uwekezaji wa serikali katika miundombinu na vifaa vya kiasi cha shilingi bilioni 283, huku idadi ya watumishi ikiongezeka kutoka 20 tu mwaka 2015 hadi kufikia 1,076 mwaka 2026.

Hospitali imefanikiwa kupanua na kuboresha huduma za matibabu ya kibobezi, ikiwemo uanzishwaji wa huduma muhimu za upandikizaji figo na uloto kwa watoto wenye selimundu, pamoja na kukuza tiba utalii kwa kuhudumia wagonjwa wa kigeni na viongozi mashuhuri, wakiwemo wagonjwa 2,897 kutoka Burundi, 526 kutoka Comoro, na wengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ubora wa huduma umeongezeka kupitia upasuaji wa matundu na uanzishwaji wa Kliniki ya Kifalme (Royal Clinic) mnamo tarehe 10 Julai 2025, ambayo imeshalaza na kuhudumia wagonjwa 18,607, wakiwemo wagonjwa wa kimataifa 390 waliofanyiwa uchunguzi mkubwa wa afya (Master Health Check-up).

BMH pia imepata ithibati ya kimataifa ya maabara ya ISO 15189:2022, imeboresha mifumo yake ya TEHAMA, imeweka mfumo wa kisasa wa kuelekeza wagonjwa (queuing system) na kutoa maoni, na imefanikiwa kupunguza muda wa mgonjwa kusubiri huduma kutoka wastani wa saa 8 hadi saa 3 tu.

"Tunatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya na hasa ndani ya BMH, na ninatoa wito kwa Watanzania wote kushiriki kuokoa maisha ya wagonjwa huku sisi tukiahidi kuendelea kuishi kwa kauli mbiu yetu ya kuvaa viatu vya mgonjwa, uwajibikaji, na kujituma, " alisema Profesa Makubi.
Katika kuimarisha miradi ya kimkakati, hospitali inaendelea na ujenzi wa jengo la matibabu ya saratani lenye thamani ya shilingi bilioni 32, jengo la matibabu ya figo la shilingi bilioni 44.9 linalojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Japani iliyochangia bilioni 28 na Serikali ya Tanzania iliyochangia bilioni 16.9, uanzishwaji wa Kituo cha Umahiri cha upandikizaji uloto, pamoja na chuo kinachotoa elimu ya ngazi ya Stashahada.

Akizungumzia mwelekeo Preofesa Makubdi alisema taasisi hiyo kwa miaka 10 ijayo inajipanga kubobea zaidi na kuwa kijiji cha utalii wa matibabu katika Makao Makuu ya nchi, Dodoma.

Kuelekea kilele cha tarehe 15 Julai 2026, matukio mbalimbali yamepangwa na mengine tayari yamefanyika ili kuongeza uelewa na ushiriki wa wadau, ikiwemo mikutano iliyofanyika mwezi Aprili 2026 jijini Dar es Salaam na Arusha na Watendaji Wakuu wa Mashirika na Taasisi zote za Umma, ambapo takriban shilingi bilioni 4 zimeshapatikana kutoka kwa wadau wa sekta ya umma na kampuni zenye ubia na serikali.
Aidha, Kongamano la Kisayansi lililoangazia hali ya huduma za upandikizaji viungo nchini lilifanyika tarehe 6 Mei 2026 katika Ukumbi wa Domiya Estate likishirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi, na hivi sasa maandalizi ya dhifa za chakula cha jioni (Gala dinners) pamoja na mbio maalumu za Marathon yanaendelea ili kuchangisha fedha hizo.

Zoezi hili la harambee la kusaidia mfuko wa matibabu ya upandikizaji uloto na figo linafanyika kwa kushirikiana kwa karibu na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa lengo la kuwasaidia Watanzania wasio na uwezo ambao idadi yao inaongezeka kila siku.

Harambee hiyo kubwa itakayofanyika tarehe 15 Julai 2026 jijini Dodoma, inatarajiwa kuongozwa na Mgeni Rasmi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Profesa makubdi ameyaomba Mashirika, taasisi, makampuni, wadau, na wananchi wote kuchangia kupitia njia rasmi zilizowekwa ambazo ni namba ya malipo (Control Number) 986930000001 au kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa akaunti namba 102501000407 zote zikiwa kwa jina la BMH Organ Transplant.
Na Mwandishi Wetu-Kigali, Rwanda

TUME ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeshiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia Barani Afrika (NEISA 2026) uliofanyika Mei 19, 2026 mjini Kigali, Rwanda, ukiwakutanisha viongozi wa kitaifa, wataalamu wa nishati, wawekezaji pamoja na mashirika ya kimataifa kujadili mustakabali wa nishati ya nyuklia barani Afrika.

Mkutano huo ulilenga kujadili namna bora ya kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme, kupunguza uchafuzi wa mazingira, kusaidia maendeleo ya viwanda, kukuza ubunifu wa teknolojia za nyuklia pamoja na kuvutia uwekezaji katika miradi ya nishati kwa ajili ya kuimarisha uchumi endelevu.

Katika mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alisema Tanzania inaendelea kutathmini matumizi ya nishati ya nyuklia kama sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuongeza vyanzo vya nishati nchini.

Rais Samia alieleza kuwa teknolojia mpya za Small Modular Reactors (SMRs) na Micro Modular Reactors (MMRs) zinaweza kuwa suluhisho sahihi kwa nchi zinazoendelea kutokana na uwezo wake wa kuzalisha nishati kwa ufanisi na usalama zaidi.

Aidha, alitaja maeneo muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya nyuklia kuwa ni pamoja na mifumo imara ya udhibiti, wataalamu wenye ujuzi pamoja na usimamizi madhubuti wa usalama kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Alisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika uzalishaji wa nishati yanahitaji maandalizi ya mifumo ya udhibiti, uwezo wa taasisi, upatikanaji wa fedha, uelewa wa wananchi na ushirikiano wa kikanda.

Katika ushiriki wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania, Profesa Najat Kassim Mohammed alihudhuria mkutano huo akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Nyuklia na Huduma za Ufundi, Dkt. Remigius Kawala.

Profesa Najat alipata fursa ya kushiriki kikao cha ndani kilichoongozwa na Rais Samia ambapo alitoa ufafanuzi kuhusu maendeleo ya nyuklia nchini pamoja na miradi inayotekelezwa na TAEC kwa kushirikiana na International Atomic Energy Agency.

Miongoni mwa mipango hiyo ni Rays of Hope unaolenga kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani nchini, Atoms4Food unaohamasisha matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika sekta ya kilimo pamoja na ushiriki wa TAEC katika mpango wa matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa uzalishaji wa umeme.

Profesa Najat alisisitiza umuhimu wa Tanzania kuendelea kuwekeza katika utafiti, usalama na mafunzo ya wataalamu ili kuhakikisha matumizi salama na endelevu ya teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, viwanda, utafiti wa madini na uzalishaji wa nishati.

Kupitia mkutano huo, TAEC ilipata nafasi ya kubadilishana uzoefu na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali kuhusu usalama wa nyuklia, mifumo ya udhibiti wa teknolojia za nyuklia pamoja na uwekezaji katika miundombinu ya kisasa ya nishati.

Aidha, ushiriki wa Tanzania katika NEISA 2026 uliendana na maono ya serikali ya kukuza sekta ya nishati na kuimarisha ushirikiano wa kikanda ndani ya Afrika Mashariki.

Katika mkutano huo, viongozi mbalimbali wa Afrika walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kuendeleza miradi ya nyuklia, kuongeza uwekezaji na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani.

Kwa ujumla, ushiriki wa TAEC katika NEISA 2026 umeiwezesha Tanzania kuendelea kujijengea nafasi katika mjadala wa kimataifa kuhusu mustakabali wa nishati ya nyuklia barani Afrika pamoja na kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kitaalamu, kiteknolojia na kiuchumi kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Mkutano wa NEISA 2026 uliandaliwa kwa ushirikiano wa International Atomic Energy Agency, United Nations Economic Commission for Africa, World Nuclear Association pamoja na Rwanda.