Articles by "HABARI ZA KIJAMII"
Showing posts with label HABARI ZA KIJAMII. Show all posts

Na Mwandishi Wetu. 

Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Bw. Tido Mhando, amewataka Waandishi wa Habari nchini kutafakari upya wajibu wao katika kuijenga jamii kupitia maudhui yenye tija, akieleza kuwa ipo haja ya kurejesha hadhi na nguvu ya taaluma hiyo katika kujenga fikra na maendeleo ya taifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Bw. Mhando amesema pamoja na JAB kusimamia utoaji wa ithibati kwa kuzingatia vigezo vya elimu na sheria, bado kuna umuhimu wa Waandishi wa Habari kuendelea kujengewa uwezo kupitia mafunzo ya kitaaluma.

“Tukitazama baadhi ya vyombo vyetu vya habari, iwe ni magazeti, redio au televisheni, mambo ya kufikirisha kwa kiasi kikubwa yamepungua. Waandishi wa Habari wanapaswa kutafakari kama hiyo ndiyo taswira wanayotaka kuiacha katika jamii ya Watanzania,” amesema.

Amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuunda mtazamo wa jamii, hivyo kuna wajibu wa kuhakikisha maudhui yanayotolewa yanajenga uelewa, yanakuza maendeleo na yanalinda maslahi ya taifa.

“Tunachosimamia ni kuhakikisha Mwandishi wa Habari anayepata ithibati anakuwa na kiwango cha elimu kisichopungua Diploma, lakini tunataka pia Waandishi wa Habari waendelee kupata mafunzo ili waweze kuimarika zaidi kitaaluma,” amesema.

Amesema ipo haja ya sekta ya habari kutafakari aina ya maudhui yanayopewa kipaumbele, akisisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kujenga fikra na mwelekeo wa jamii.

Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, Mariam Ibrahim amemshuru Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Taifa , Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kupendekeza jina lake na Kamati Kuu ya chama hicho kulipitisha na hatimaye kushinda kwa kura nyingi.

Ametoa shukrani hizo kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa ,Rais Dk.Samia Suluhu Hassan alipokuwa akisalimia viongozi mbalimbali wa Chama hicho wakati wa Semina ya Uongozi na Maendeleo kwa madiwani wote wanawake  wa Mkoa wa Pwani.

“Nitumie nafasi hii kwa dhati ya moyo wangu kumshukuru Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Taifa Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kunipendekeza mimi na Kamati Kuu kurudisha jina langu na kuja katika Mkoa wa Pwani na kupigiwa kura nyingi.

“Waheshimiwa madiwani hatujaonana toka Uchaguzi mkuu ulivyopita hivyo naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru nyote kwa kura zenu za kishindo.Nasema ahsanteni sana,amesema mbele ya madiwani hao pamoja na viongozi wa Mkoa huo.
 
Amesisitiza ameamua kutoa shukrani hizo kwasababu ndio mara yake ya kwanza wanakutana ambapo ametumia nafasi hiyo pia kuwaaahidi kuendelea kushirikiana nao na yupo tayari kwa wakati wowote ambao atahitahika.“Tutakuwa pamoja katika kila hali.”






Na Mwandishi Wetu

BABATI — Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Babati mkoani Manyara imesitisha kusikiliza kesi ya jinai namba 291 ya mwaka 2026 iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Babati Mjini, Paulina Gekul, inayomkabili Brayton Lucas (17), baada ya kujiridhisha kuwa mshtakiwa huyo ni mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18 na hivyo shauri hilo linapaswa kusikilizwa katika Mahakama ya Watoto kwa mujibu wa sheria.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya Wakili wa upande wa utetezi, Thadei Lister, kuiomba mahakama kujiridhisha kuhusu umri wa mshtakiwa kwa kuwasilisha nyaraka mbalimbali ikiwemo cheti cha kuzaliwa kilichoonesha kuwa Brayton alizaliwa Novemba 12, 2008 na kwa sasa ana umri wa miaka 17 na miezi sita, tofauti na taarifa zilizokuwa katika hati ya mashtaka zilizomtaja kuwa na miaka 19.

Katika shauri hilo, Paulina Gekul alidai kuwa Brayton Lucas, ambaye alikuwa akichunga mifugo yake, alihusika katika wizi wa mbuzi 15 wenye thamani ya shilingi milioni tatu, kosa linalodaiwa kufanyika chini ya kifungu cha 268 cha sheria ya wizi wa mifugo. Kesi hiyo ilikuwa na jumla ya watuhumiwa watatu.

Mahakama pia ilielezwa kuwa mtoto huyo alikuwa amechanganywa katika shauri moja na watuhumiwa watu wazima, jambo ambalo upande wa utetezi ulidai ni kinyume na sheria zinazolinda haki za mtoto.

 Baada ya kupitia nyaraka zilizowasilishwa, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Babati, Ahmed Mgodo, alisema mahakama imejiridhisha kuwa Brayton Lucas ni mtoto na hivyo haina mamlaka ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo. Kutokana na uamuzi huo, mahakama ilisimamisha shauri hilo dhidi ya mshtakiwa huyo na kuagiza polisi kuandaa hati mpya ya mashtaka kwa mujibu wa sheria zinazohusu watoto.

Brayton Lucas alipatiwa dhamana huku washtakiwa wawili wengine wakiendelea kushikiliwa. Wakili Thadei Lister amesema wako tayari kuendelea kumtetea mtoto huyo iwapo atafikishwa katika Mahakama ya Watoto.

Akizungumza nje ya mahakama, Wakili Thadei alisema Brayton ni mwanafunzi wa kidato cha nne ambaye alitoweka akiwa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha na wazazi wake walikuwa wakimtafuta kwa kipindi cha miezi mitatu kabla ya kupata taarifa kuwa amekamatwa Babati kwa tuhuma za wizi.

Mama mzazi wa Brayton alisema mtoto wake alitakiwa kuwa shuleni baada ya kumaliza kidato cha nne na tayari alikuwa amepangiwa shule, lakini aliondoka nyumbani bila kutoa taarifa na baada ya juhudi za muda mrefu za kumtafuta walipata taarifa kuwa alikuwa Babati akifanya kazi.
Wakati huo huo, Diwani wa Kata ya Maruvango Wilaya ya Arumeru Mashariki, Digna Nassari, amesema taarifa za kupotea kwa mtoto huyo zilikuwa zimetolewa polisi miezi mitatu kabla ya kufunguliwa kesi dhidi yake na Paulina Gekul.

Aidha, Digna amesema Brayton ni miongoni mwa watoto 16 kutoka kata hiyo waliotoroka shule, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana kuhakikisha watoto wanarudi katika mfumo wa elimu na kupata ulinzi unaostahili
Na Mwandishi Wetu-Kigali, Rwanda

TUME ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeshiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia Barani Afrika (NEISA 2026) uliofanyika Mei 19, 2026 mjini Kigali, Rwanda, ukiwakutanisha viongozi wa kitaifa, wataalamu wa nishati, wawekezaji pamoja na mashirika ya kimataifa kujadili mustakabali wa nishati ya nyuklia barani Afrika.

Mkutano huo ulilenga kujadili namna bora ya kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme, kupunguza uchafuzi wa mazingira, kusaidia maendeleo ya viwanda, kukuza ubunifu wa teknolojia za nyuklia pamoja na kuvutia uwekezaji katika miradi ya nishati kwa ajili ya kuimarisha uchumi endelevu.

Katika mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alisema Tanzania inaendelea kutathmini matumizi ya nishati ya nyuklia kama sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuongeza vyanzo vya nishati nchini.

Rais Samia alieleza kuwa teknolojia mpya za Small Modular Reactors (SMRs) na Micro Modular Reactors (MMRs) zinaweza kuwa suluhisho sahihi kwa nchi zinazoendelea kutokana na uwezo wake wa kuzalisha nishati kwa ufanisi na usalama zaidi.

Aidha, alitaja maeneo muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya nyuklia kuwa ni pamoja na mifumo imara ya udhibiti, wataalamu wenye ujuzi pamoja na usimamizi madhubuti wa usalama kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Alisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika uzalishaji wa nishati yanahitaji maandalizi ya mifumo ya udhibiti, uwezo wa taasisi, upatikanaji wa fedha, uelewa wa wananchi na ushirikiano wa kikanda.

Katika ushiriki wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania, Profesa Najat Kassim Mohammed alihudhuria mkutano huo akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Nyuklia na Huduma za Ufundi, Dkt. Remigius Kawala.

Profesa Najat alipata fursa ya kushiriki kikao cha ndani kilichoongozwa na Rais Samia ambapo alitoa ufafanuzi kuhusu maendeleo ya nyuklia nchini pamoja na miradi inayotekelezwa na TAEC kwa kushirikiana na International Atomic Energy Agency.

Miongoni mwa mipango hiyo ni Rays of Hope unaolenga kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani nchini, Atoms4Food unaohamasisha matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika sekta ya kilimo pamoja na ushiriki wa TAEC katika mpango wa matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa uzalishaji wa umeme.

Profesa Najat alisisitiza umuhimu wa Tanzania kuendelea kuwekeza katika utafiti, usalama na mafunzo ya wataalamu ili kuhakikisha matumizi salama na endelevu ya teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, viwanda, utafiti wa madini na uzalishaji wa nishati.

Kupitia mkutano huo, TAEC ilipata nafasi ya kubadilishana uzoefu na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali kuhusu usalama wa nyuklia, mifumo ya udhibiti wa teknolojia za nyuklia pamoja na uwekezaji katika miundombinu ya kisasa ya nishati.

Aidha, ushiriki wa Tanzania katika NEISA 2026 uliendana na maono ya serikali ya kukuza sekta ya nishati na kuimarisha ushirikiano wa kikanda ndani ya Afrika Mashariki.

Katika mkutano huo, viongozi mbalimbali wa Afrika walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kuendeleza miradi ya nyuklia, kuongeza uwekezaji na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani.

Kwa ujumla, ushiriki wa TAEC katika NEISA 2026 umeiwezesha Tanzania kuendelea kujijengea nafasi katika mjadala wa kimataifa kuhusu mustakabali wa nishati ya nyuklia barani Afrika pamoja na kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kitaalamu, kiteknolojia na kiuchumi kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Mkutano wa NEISA 2026 uliandaliwa kwa ushirikiano wa International Atomic Energy Agency, United Nations Economic Commission for Africa, World Nuclear Association pamoja na Rwanda.

MONACO - Benki ya CRDB imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuunga mkono maendeleo ya Taifa kupitia sekta mbalimbali kwa kushiriki katika Mkutano Mkuu wa 81 wa Michezo ya Majeshi Duniani (81st CISM General Assembly) uliofanyika nchini Monaco kuanzia tarehe 1 hadi 9 Mei 2026.

Mkutano huo wa kimataifa uliwakutanisha viongozi wa kijeshi na wadau wa michezo kutoka zaidi ya nchi 130 duniani kwa lengo la kuimarisha mshikamano, diplomasia ya michezo na amani kupitia kaulimbiu ya “Friendship Through Sport.”
Benki ya CRDB, ikiwa miongoni mwa wadau wakubwa wa maendeleo nchini, imeendelea kuunga mkono jitihada za vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na michezo ya majeshi, hatua inayoimarisha ushirikiano wake na taasisi za Serikali katika kukuza ustawi wa askari na familia zao.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliongozwa na Brigedia Jenerali Saidi Hamisi Saidi, akisaidiana na Luteni Kanali Penina Anthony Igwe. Kutoka CRDB, ujumbe unajumuisha Meneja wa Kitengo cha Wateja Maalum, Crispin Sichalwe pamoja na Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Emmanuel Tupeligwe.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Sichalwe alisema CRDB imeendelea kutoa huduma maalum za kifedha kwa wanajeshi ndani na nje ya nchi, ikiwemo mikopo nafuu, bima na huduma za kifedha zinazowafikia popote walipo.

“Tunatambua mchango mkubwa wa majeshi katika usalama wa Taifa, hivyo tunahakikisha wanapata huduma bora na za haraka kupitia kitengo chetu maalum,” alisema.
Kwa upande wake, Tupeligwe alisisitiza kuwa CRDB itaendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia elimu ya fedha na huduma zinazowafikia wanajeshi hata wakiwa katika maeneo ya mbali au majukumu ya kimataifa.

Aidha, benki hiyo imeendelea kuimarisha ushirikiano wake wa kimkakati na JWTZ ili kuhakikisha wanajeshi wanapata huduma bora za kifedha kwa urahisi, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika maendeleo na usalama wa Taifa.

Na Jawadu Kinyobwa 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewataka wahitimu wa Taasisi ya Uongozi kuwa viongozi waadilifu, wenye nidhamu na uthubutu ili kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Akizungumza Mei 15, 2026 katika Mahafali ya Tisa ya Taasisi hiyo yaliyofanyika katika Mlimani City jijini Dar es Salaam, Mhe. Ridhiwani alisema dunia ya sasa inahitaji viongozi wenye maadili, uwajibikaji na uwezo wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.

Alisema uadilifu ni sifa muhimu ya kiongozi bora na mwenye kuaminika, hivyo wahitimu wanapaswa kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuwa viongozi wanaozingatia haki, uwazi na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.“Nawakumbusha umuhimu wa kuwa viongozi wenye uzalendo. Tukumbuke msemo wa wahenga kwamba adhabu ya msaliti ni malipo ya usaliti wake. Usaliti mkubwa katika uongozi wa umma ni sawa na ubadhirifu wa mali za umma,” alisema Ridhiwani.

Aidha, aliwataka wahitimu hao kulinda rasilimali za taifa na kuweka mbele maslahi ya wananchi katika maamuzi yao ya kila siku ili kusaidia kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Alisema Tanzania inahitaji viongozi waaminifu na wenye uwajibikaji ambao watatumia nafasi zao kuendeleza ustawi wa wananchi na kuimarisha misingi ya utawala bora.
Sambamba na hilo, Waziri Ridhiwani alisema uongozi unaozingatia haki na uwazi utaendelea kuitangaza vyema Tanzania pamoja na Taasisi ya Uongozi ndani na nje ya nchi.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Bw. Kadari Singo alisema taasisi hiyo imetimiza miaka 15 tangu kuanzishwa kwake rasmi Julai mwaka 2010 kwa Hati ya Rais kama Kituo cha Utaalamu wa Hali ya Juu kwa ajili ya kujenga na kuimarisha viongozi barani Afrika.

Alisema kwa kipindi hicho, taasisi hiyo imefanikiwa kutoa mafunzo mbalimbali ya uongozi, kuandaa mijadala ya kisera pamoja na kufanya tafiti na machapisho yaliyosaidia kukuza maarifa ya kiuongozi.

Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Burhan Mohamed alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa wa kiuongozi na kuwasaidia kufanya maamuzi yenye tija kwa taasisi na jamii.

Alisema mahafali hayo hayakuwa tu hitimisho la mafunzo, bali yalikuwa ishara ya mabadiliko makubwa ya kiuongozi na maendeleo binafsi waliyoyapata ndani ya miezi sita ya programu hiyo.











Na Mwandishi wetu- MBEYA

Mkurugenzi msaidizi wa Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano  ya Dharura kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Bi. Jane Kikunya amewataka Wajumbe wa Timu  ya kukabiliana na Dharura na Uendeshaji  wa Kitio  cha Operesheni  na Mawasiliano  ya Dharura ya  Mkoa wa  Mbeya kufanya kazi kwa ushirikiano, mshikamano na mawasiliano ya karibu ili kutekeleza wajibu wao kwa weledi na ufanisi unaotakiwa.

Mkurugenzi huyo, ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tano yanayolenga kuziandaa timu za kukabiliana na Maafa za Mkoa huo.

Aidha, mafunzo hayo  ambayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu yanatolewa kwa Wajumbe wa Kamati ya Wataalamu ya Usimamizi  wa Maafa, Wajumbe wateule wa Timu ya kukabiliana na Dharura ya Mkoa na wataalamu wa Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura, Waratibu wa Maafa Mkoa na Halmashauri.

Vilevile, Bi. Jane amesema mafunzo hayo yatakuwa mhimili muhimu katika kuhakikisha Mkoa unajiandaa vyema ili kukabiliana na matukio ya dharura kwa haraka hivyo ni lazima timu lengwa ifanye kazi kwa mshikamano ili kuleta ufanisi unaohitajika.

Kwa upande wao  wanufaika wa mafunzo hayo wameishukuru Serikali kwa namna inavyofanya jitihada kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira salama.
*Asema Serikali itaendelea kuongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu
 
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka taasisi za elimu nchini kutowazuia wanafunzi kufanya mitihani ya masomo yao kwa kushindwa kulipa ada.
 
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuongeza fedha za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na vyuo vya kati ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike na mikopo hiyo.
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo (Alhamisi Mei 14, 2026) Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Latifa Khamis Juwakali aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kiuhusu wanafunzi wanaozuiwa kufanya mitihani kwa kutokulipa ada.
Katika maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani, Askofu Bagonza amegusa hisia za wengi baada ya kuandika simulizi maalum kuhusu mama yake mzazi, Dorothea Kagemulo Bagonza, akimtaja kama “Profesa Mnoa Viwango” kutokana na malezi makali, yenye nidhamu na yaliyowajenga watoto wake kuwa watu wenye uwajibikaji mkubwa katika maisha.

Kupitia ujumbe wake, Askofu Bagonza alisema mama yake alikuwa mtu wa viwango vya juu sana katika kila jambo ndani ya familia, kiasi kwamba hakuna mtoto aliyewahi kufikia kiwango alichoweka. Alieleza kuwa hata kazi ndogo kama kupalilia, kuosha vyombo au kufanya usafi zilipaswa kufanywa kwa umakini mkubwa, vinginevyo mtoto alionekana hajafanya kazi ipasavyo.

“Ukimaliza kupalilia na ukajisikia umefanya kazi nzuri, yeye akija anakwambia umeparaza tu, hujapalilia,” aliandika Askofu huyo, akionyesha namna mama yake alivyosisitiza ubora na umakini katika kila kazi.

 Aidha, alisema hata watoto walipofanya vizuri shuleni, mama yao hakuridhika kirahisi. Alisema mtoto angekuwa wa kwanza darasani lakini bado mama yao angewaambia darasa lenyewe huenda lilikuwa la wanafunzi dhaifu, hatua iliyowafanya watoto kujifunza kutoridhika na mafanikio madogo bali kuendelea kujituma zaidi.

Katika simulizi hiyo, Askofu Bagonza alieleza kuwa mama yake alikuwa pia mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wanazingatia usafi, nidhamu na matumizi sahihi ya fedha. Alisema watoto walifundishwa kuokoa fedha badala ya kuzitumia hovyo, huku akiba zao zikikaguliwa kila mwezi.

Mbali na hilo, aliandika kuwa maisha ya nyumbani yalijengwa katika misingi ya kazi na kujituma. Watoto walipewa majukumu ya kwenda shambani, kufanya kazi za nyumbani na kushiriki shughuli mbalimbali za familia bila uvivu. Hata mtoto aliyekuwa akijisikia vibaya hakuruhusiwa kulala muda mwingi bali alipewa kazi nyepesi karibu na nyumbani ili kuendelea kuwa sehemu ya majukumu ya familia.

Askofu huyo pia alikumbuka namna mama yake alivyosisitiza maadili ya dini na maisha ya kiroho. Alisema kwenda kanisani ilikuwa lazima kwa watoto wote, na kila mmoja alitakiwa kueleza kile alichojifunza baada ya ibada. Kwa mujibu wa Askofu Bagonza, jambo hilo liliwajenga watoto kuwa watu wenye nidhamu, uelewa na heshima kwa mafundisho ya dini.

Pamoja na ukali wake, Askofu Bagonza alisema mama yake alikuwa na upendo mkubwa kwa watoto wake na kila alichokifanya kilikuwa na lengo la kuwajenga kuwa watu bora katika jamii. Alimshukuru kwa malezi hayo, akisema yamechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio yao maishani.

“Huyo ndiyo mama. Happy Mother’s Day Ma Dorothea. Huna baya,” alihitimisha Askofu Bagonza katika ujumbe wake uliogusa hisia za watu wengi kwenye mitandao ya kijamii.