Articles by "AFYA"
Showing posts with label AFYA. Show all posts
Na Mwandishi Wetu.

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) inahitaji kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 7 ndani ya kipindi cha miaka miwili kwa ajili ya kufanikisha matibabu ya ubingwa bobezi ya upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu pamoja na upandikizaji wa figo kwa wananchi wenye uhitaji mkubwa wa huduma hizo.

Mahitaji haya yametangazwa leo tarehe 21 Mei 2026 katika Ukumbi wa NIMR Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Abel Makubi katika mkutano wake na wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri, Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jumuiya ya Miitandao Tanzania (JUMIKITA).

Alisema kwa sasa kuna watoto 50 wanaohitaji upondikizaji wa uloto na wengine 50 kwa ajili ya upandfikizaji wa figo.

Mkutano huo ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo, hapo Julai 15 ,2026 ambapo safari ya maadhimisho haya ilizinduliwa rasmi mwezi Oktoba mwaka 2025.
Tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo Oktoba 13,2015, Hospitali ya Benjamin Mkapa imekuwa na dhamira ya kutoa huduma za kibingwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika kuzuia, kuchunguza, na kutibu magonjwa mbalimbali, pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya na kufanya tafiti.

Kwa sasa, BMH inahudumia takribani wananchi milioni 10 kutoka mikoa nane ya Tanzania, ikiwa na vitanda 400 na watumishi 1,073, wakiwemo madaktari bingwa na bingwa bobezi zaidi ya 100.

Kwa mujibu wa Profesa Makubi Hospitali hiyo inatoa huduma 20 za kibingwa na huduma 18 za ubingwa bobezi zikiwemo upandikizaji wa viungo, upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua, uchunguzi wa mishipa ya moyo, huduma za radiolojia ya kisasa, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, ubadilishaji wa nyonga na magoti, upasuaji wa njia ya matundu madogo, pamoja na uchujaji wa damu.

Profesa Makubdi amesema ndani ya miaka 10 ya utendaji, hospitali imepata mafanikio makubwa yaliyochangiwa na uwekezaji wa serikali katika miundombinu na vifaa vya kiasi cha shilingi bilioni 283, huku idadi ya watumishi ikiongezeka kutoka 20 tu mwaka 2015 hadi kufikia 1,076 mwaka 2026.

Hospitali imefanikiwa kupanua na kuboresha huduma za matibabu ya kibobezi, ikiwemo uanzishwaji wa huduma muhimu za upandikizaji figo na uloto kwa watoto wenye selimundu, pamoja na kukuza tiba utalii kwa kuhudumia wagonjwa wa kigeni na viongozi mashuhuri, wakiwemo wagonjwa 2,897 kutoka Burundi, 526 kutoka Comoro, na wengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ubora wa huduma umeongezeka kupitia upasuaji wa matundu na uanzishwaji wa Kliniki ya Kifalme (Royal Clinic) mnamo tarehe 10 Julai 2025, ambayo imeshalaza na kuhudumia wagonjwa 18,607, wakiwemo wagonjwa wa kimataifa 390 waliofanyiwa uchunguzi mkubwa wa afya (Master Health Check-up).

BMH pia imepata ithibati ya kimataifa ya maabara ya ISO 15189:2022, imeboresha mifumo yake ya TEHAMA, imeweka mfumo wa kisasa wa kuelekeza wagonjwa (queuing system) na kutoa maoni, na imefanikiwa kupunguza muda wa mgonjwa kusubiri huduma kutoka wastani wa saa 8 hadi saa 3 tu.

"Tunatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya na hasa ndani ya BMH, na ninatoa wito kwa Watanzania wote kushiriki kuokoa maisha ya wagonjwa huku sisi tukiahidi kuendelea kuishi kwa kauli mbiu yetu ya kuvaa viatu vya mgonjwa, uwajibikaji, na kujituma, " alisema Profesa Makubi.
Katika kuimarisha miradi ya kimkakati, hospitali inaendelea na ujenzi wa jengo la matibabu ya saratani lenye thamani ya shilingi bilioni 32, jengo la matibabu ya figo la shilingi bilioni 44.9 linalojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Japani iliyochangia bilioni 28 na Serikali ya Tanzania iliyochangia bilioni 16.9, uanzishwaji wa Kituo cha Umahiri cha upandikizaji uloto, pamoja na chuo kinachotoa elimu ya ngazi ya Stashahada.

Akizungumzia mwelekeo Preofesa Makubdi alisema taasisi hiyo kwa miaka 10 ijayo inajipanga kubobea zaidi na kuwa kijiji cha utalii wa matibabu katika Makao Makuu ya nchi, Dodoma.

Kuelekea kilele cha tarehe 15 Julai 2026, matukio mbalimbali yamepangwa na mengine tayari yamefanyika ili kuongeza uelewa na ushiriki wa wadau, ikiwemo mikutano iliyofanyika mwezi Aprili 2026 jijini Dar es Salaam na Arusha na Watendaji Wakuu wa Mashirika na Taasisi zote za Umma, ambapo takriban shilingi bilioni 4 zimeshapatikana kutoka kwa wadau wa sekta ya umma na kampuni zenye ubia na serikali.
Aidha, Kongamano la Kisayansi lililoangazia hali ya huduma za upandikizaji viungo nchini lilifanyika tarehe 6 Mei 2026 katika Ukumbi wa Domiya Estate likishirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi, na hivi sasa maandalizi ya dhifa za chakula cha jioni (Gala dinners) pamoja na mbio maalumu za Marathon yanaendelea ili kuchangisha fedha hizo.

Zoezi hili la harambee la kusaidia mfuko wa matibabu ya upandikizaji uloto na figo linafanyika kwa kushirikiana kwa karibu na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa lengo la kuwasaidia Watanzania wasio na uwezo ambao idadi yao inaongezeka kila siku.

Harambee hiyo kubwa itakayofanyika tarehe 15 Julai 2026 jijini Dodoma, inatarajiwa kuongozwa na Mgeni Rasmi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Profesa makubdi ameyaomba Mashirika, taasisi, makampuni, wadau, na wananchi wote kuchangia kupitia njia rasmi zilizowekwa ambazo ni namba ya malipo (Control Number) 986930000001 au kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa akaunti namba 102501000407 zote zikiwa kwa jina la BMH Organ Transplant.





Ujumbe wa Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassanakiwa kwenye mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Dkt. Jean Kaseya pamoja na Ujumbe wake, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 13 Mei, 2026. 



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Dkt. Jean Kaseya pamoja na Ujumbe wake Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 13 Mei, 2026.

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Jean Kaseya, Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC pamoja na ujumbe wake, Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi hao walijadili masuala mbalimbali kuhusu afya ya uzazi, mama na mtoto barani Afrika.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kaseya alisema Africa CDC ina dhamira ya kushirikiana na Rais Samia ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, pamoja na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, kwa lengo la kuimarisha huduma za afya katika sekta hiyo muhimu.

Alisema ushirikiano huo unalenga kuongeza juhudi za kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na kuboresha huduma za afya kwa mama na watoto katika nchi mbalimbali za Afrika.

Dkt. Kaseya alieleza kuwa Tanzania imeonyesha mafanikio makubwa katika sekta ya afya, hususan katika upatikanaji wa huduma kwa wananchi, jambo ambalo linaweza kuwa mfano kwa nchi nyingine barani humo.

Alibainisha kuwa asilimia 85 ya wananchi nchini Tanzania wanapata huduma za afya ndani ya umbali wa kilomita tano kutoka maeneo wanayoishi, hatua aliyosema inaimarisha ajenda ya Afrika ya usalama wa afya na kujitegemea katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Rais Samia alisema Serikali ya Tanzania ipo tayari kuendelea kushirikiana na Africa CDC katika kuendeleza ajenda ya afya ya mama na mtoto, akisisitiza kuwa utekelezaji wa malengo yaliyowekwa unahitaji mipango madhubuti na uratibu wa karibu.

Aidha, Rais Samia aliiagiza Wizara ya Afya kushirikiana kwa karibu na Africa CDC katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha afya ya uzazi, mama na mtoto nchini na barani Afrika kwa ujumla.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inatarajia kutoa vibali vya ajira mpya katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa sekta ya afya pamoja na kada nyingine, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza uhaba wa madaktari na wauguzi nchini.

 Akizungumza Mei 12, 2026 katika Kongamano la Kwanza la Kisayansi la Wauguzi lililoambatana na Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika katika Hotel Verde Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi alisema Serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika kuboresha huduma za afya ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora na ya kisasa.

 Alieleza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya ikiwemo ujenzi wa Hospitali Mpya ya Mnazi Mmoja pamoja na Hospitali ya Saratani Binguni, sambamba na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa na kuimarisha mafunzo kwa watumishi wa sekta hiyo.

 Rais Dkt. Mwinyi pia aliwataka wauguzi nchini kuendelea kufanya kazi kwa kujituma, huruma na kuzingatia maadili ya taaluma yao, akisisitiza kuwa wauguzi wana nafasi kubwa katika kuimarisha huduma za afya na kuokoa maisha ya wananchi.

 Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo, “Kuwawezesha Wauguzi ni Kuokoa Maisha” (Empowering Nurses, Saving Lives).

Mkuu wa Wilaya ya Geita Mh. Hashim Abdallah Komba(kulia) akikabidhiwa moja ya vifaa vya hospitali vilivyotolewa na Afisa Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania Bw. Stanley Kafu (kushoto) kwa lengo la kurudisha kwa jamii. Hafla hii imefanyika kama moja ya huduma za Benki hiyo chini ya Mpango wa Exim Cares ambapo wanatoa misaada kwa sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na mazingira. Tukio hilo limefanyika tarehe 6 May 2026, Mkoani Geita.
Na Mwandishi Wetu, Geita.

Benki ya Exim Tanzania kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii unaojulikana kama Exim Cares, imeendelea kuonyesha dhamira ya kusaidia sekta ya afya baada ya kutoa msaada wa vifaa tiba katika Hospitali ya Manispaa ya Geita, hatua inayolenga kuboresha huduma za afya ya uzazi na dharura kwa wananchi wa mkoa huo.

Msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo wa kuwekeza katika maendeleo ya jamii kupitia sekta muhimu zikiwemo afya, elimu, mazingira, ubunifu na uwezeshaji wa kiuchumi. Kupitia mpango huo, Exim Bank imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya kijamii nchini yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza ustawi wa jamii.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Abdallah Komba, aliipongeza Benki ya Exim kwa moyo wa kujitolea kusaidia jamii, akisema mchango huo utasaidia kuboresha huduma kwa watoto wanaozaliwa kabla ya muda pamoja na wenye changamoto mbalimbali za kiafya.

“Benki ya Exim imeonyesha mfano mzuri wa uwajibikaji kwa jamii kwa kugusa moja kwa moja sekta ya afya ambayo ni muhimu kwa maisha ya wananchi. Msaada huu utasaidia kuokoa maisha ya watoto na akina mama wengi,” alisema Komba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Stanley Kafu, alisema msaada huo umetokana na tathmini ya mahitaji halisi ya hospitali hiyo, huku lengo kuu likiwa ni kusaidia kupunguza changamoto zinazokwamisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wa Geita.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Geita, Dkt. Thomas Mauru, alisema msaada huo utaongeza uwezo wa hospitali katika kutoa huduma kwa wakati na kwa ufanisi, hususan kwa watoto njiti na wale wanaozaliwa na changamoto za kiafya. Alisema vifaa hivyo vitasaidia kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa na hospitali hiyo kwa jamii inayowazunguka.

Mbali na shughuli hiyo ya kijamii, Benki ya Exim inatarajia kuzindua rasmi tawi lake jipya mkoani Geita, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi na wafanyabiashara wa mkoa huo. Uzinduzi huo unatarajiwa kufanywa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
SHIRIKA la Dawa Asili na Ulinzi wa Mazingira(TRAMEPRO) limesema linatambua na kuthamini mchango wao katika kukuza na kuendeleza sekta ya tiba asilia, ambayo imeendelea kuwa tegemeo muhimu kwa wananchi wengi katika huduma za afya.
TRAMEPRO imetoa kauli hiyo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi, 2026.

Akitoa salaam kuhusu maadhimisho hayo ya Siku ya Wafanyakazi duniani Katibu Mkuu wa TRAMEPRO Boniventura Mwalongo amesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa wanaungana na jumuiya ya kimataifa kusisitiza kuwa kazi ni msingi wa utu, heshima na maendeleo ya binadamu.

Amesema Kaulimbiu ya Mei Mosi mwaka huu inasema Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050,hivyo wanasisitiza umuhimu wa kazi zenye staha.

“Mafundisho ya kijamii na kiroho, kama yanavyoakisiwa na World Health Organization, yanaeleza kuwa kazi si tu njia ya kujipatia kipato, bali pia ni wito wa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii yenye haki, mshikamano na ustawi wa wote.

“Sekta ya tiba asilia na mbadala inaendelea kuwa mhimili muhimu wa mfumo wa afya, ikichangia utoaji wa huduma, ajira, uhifadhi wa maarifa ya jadi na kukuza uchumi wa ndani,”amesema na kusisitiza umuhimu wa kazi katika maendeleo ya taifa.

Ameongeza Baba wa Taifa Mwalim Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema:“Kazi ni kipimo cha utu na msingi wa maendeleo ya binadamu.”

Kuhusu takwimu za ajira katika sekta ya tiba asili na mbadala amesema zaidi ya asilimia 70–80 ya watu duniani hutegemea tiba asilia na mbadala kwa kiwango fulani cha huduma za afya;

Amefafanua hali hiyo imezalisha mamilioni ya ajira duniani, zikiwemo za waganga wa jadi, watafiti, wazalishaji wa dawa za asili, washauri wa afya na watoa huduma za tiba jumuishi huku akieleza Shirika la Afya Dunuani inatambua rasmi kundi la wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala kama sehemu ya nguvu kazi ya sekta ya afya duniani.

Amesema kwa Afrika na Tanzania
Barani Afrika, zaidi ya asilimia 80 ya wananchi hutegemea tiba asilia, hivyo kuifanya kuwa sekta muhimu ya ajira vijijini na mijini;

Wakati huo huo amesema TRAMEPRO inasisitiza kuwa haki, usawa na heshima kwa wafanyakazi ni nguzo kuu ya maendeleo endelevu na mwito wao kwa Serikali ni kuendelea kuimarisha sera, sheria na usimamizi wa sekta ya afya na tiba asilia.

Pia kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, utafiti na ubunifu, kukuza ajira na kulinda haki za wafanyakazi na kwa vijana kuchangamkia fursa za ajira na ubunifu katika tiba asilia na mazingira.

Mwalongo amezungumzia umuhimi wa kuzingatiwa haki, mshikamano na uwajibikaji ambapo kwa kufanya hivto litajengwa taifa lenye afya bora, uchumi imara na maendeleo endelevu yanayomgusa kila Mtanzania.

“TRAMEPRO inaendelea kusimama bega kwa bega na Serikali, wadau wa ndani na nje ya nchi, pamoja na wafanyakazi wote katika kuhakikisha sekta ya tiba asilia na mazingira inachangia kikamilifu maendeleo ya taifa.”
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesisitiza kwamba bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27 inapaswa kutoa mwelekeo wa Taifa katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.

Mchengerwa amesema hayo Jumapili Mei 03, 2026 wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wizara ya Afya kilichofanyika ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza.

"Lazima tujiandae kikamilifu kwa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Hili si suala la kadi pekee bali lazima kuwe na utayari wa miundombinu, mifumo, dawa na rasilimali watu imara" alisema Mchengerwa.

Mchengerwa alisisitiza kwamba lazima mifumo ya TEHAMA iwe imara, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba uimarishwe huku akiweka mkazo kwa buzalishaji wa ndani kupewa kipaumbele na Wizara ya Afya.

"Lazima mifumo ya manunuzi itoe kipaumbele kwa wazalishaji wa ndani. Katibu Mkuu nakuagiza usimamie hilo, ununuzi kupitia MSD na mifumo yetu ya manunuzi lazima izingatie hilo lakini kwa kuzingatia ubora" ameongeza.

Mchengerwa aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kupiga hatua ikiwemo kuongeza upatikanaji wa dawa muhimu kufikia wastani wa asilimia 73 kwa mwezi Februari, 2026.

"Pia tumeendelea kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kupitia uwekezaji katika vituo vya afya, hospitali za wilaya, vifaa tiba na rasilimali watu. Haya ni mafanikio ya pamoja chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan" alisema Mchengerwa.

Pia alitoa wito kwa kila mtumishi, kuanzia makao makuu hadi hospitali za rufaa, kutoka idara hadi kituo cha afya, kuhakikisha wanatoa huduma kwa weledi na huruma kwa wananchi.

"Hatutavumilia ucheleweshaji wa huduma usio na sababu. Hatutavumilia upendeleo unaodhalilisha haki za mwananchi" alisisitiza Mchengerwa huku akiagiza Katibu Mkuu kufanyia kazi malalamiko ya wagonjwa kukaa muda mrefu bila kupata huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt Seif Shekalaghe alisema kikao hicho kimelenga kujadili na kupitisha mwelekeo wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27 yenye lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi pamoja na ustawi wa watumishi.

Naye Katibu wa Baraza hilo, Vivian Joseph ambaye ni Afisa Tawala Mkuu Wizara ya Afya alisema kupitia kikao hicho kitasaidia upatikanaji wa bajeti ambayo ni shirikishi kutekelezwa na watumishi wa wizara hiyo baada ya kupitishwa na bunge.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha baraza kuu la wafanyakazi wa wizara hiyo kilichofanyika jijini Mwanza.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha baraza kuu la wafanyakazi wa wizara hiyo kilichofanyika jijini Mwanza.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe akizungumza kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo kilicholenga kujadili na kupitisha bajeti ya mwaka 2026/27.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe akizungumza kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi Wizara ya Afya kilichoketi jijini Mwanza.
Wafanyakazi wa Wizara ya Afya wakifuatilia kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.
Wafanyakazi wa Wizara ya Afya wakifuatilia kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.
Wafanyakazi wa Wizara ya Afya wakifuatilia kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.

Na Jawadu Kinyobwa

Tanzania imezidi kujiimarisha kama kitovu cha mafunzo utawala bora barani Afrika baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, kupokea ujumbe wa watu 25 kutoka nchini Somalia kwa ajili ya programu maalumu ya mafunzo ya kuendesha shughuli za utumishi wa umma kwa ufanisi.

Akizungumza mara baada ya kuwakaribisha wajumbe hao Aprili 28 , Mhe. Kikwete ameeleza kuwa ujio huo ni kielelezo cha imani ambayo mataifa mengine wanayo kwa Tanzania kama nchi ya mfano katika kuimarisha amani, utulivu na maendeleo ya kiutawala. 

Amesema lengo kuu la ugeni huo ni kujifunza namna mifumo ya utumishi wa umma nchini inavyofanya kazi, ikiwemo usimamizi wa rasilimali watu na namna utumishi huo unavyoweza kujibu kero za wananchi kwa haraka na usahihi.

Waziri Kikwete amesisitiza kuwa Watanzania wapaswa kujua kwamba "wamekalia dhahabu" kutokana na mabadiliko makubwa ya kimfumo yaliyofanyika, hususan katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita inayowezesha wananchi kuwasiliana moja kwa moja na serikali yao. 

Amebainisha kuwa matumizi ya teknolojia (Digitalization) yamerahisisha huduma ambapo kwa sasa mtumishi wa umma hahitaji kusafiri kutoka mkoani kwenda Dodoma kufuata huduma, bali anaweza kupata mahitaji yake, ikiwemo maombi ya mikopo na mawasiliano na viongozi, kupitia mifumo ya kidijitali iliyowekwa.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu ambaye pia Naibu Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Bw. Xavier Daudi, amefafanua kuwa wajumbe hao watapitishwa kwenye maeneo muhimu ya kiutendaji ikiwemo muundo wa serikali, mifumo ya Serikali Mtandao (e-Government), na mbinu za kisasa za utunzaji wa nyaraka. 

Amesema upekee wa mifumo ya Tanzania na miundombinu yake ya kisasa ya kiutendaji ndivyo vinavyovutia nchi nyingi za Afrika Mashariki na kwingineko kuja kujifunza.

Awali akizungumza Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Ernest Mabonesho, ambaye ndiye mratibu wa programu hiyo, amebainisha kuwa mafunzo hayo ni matokeo ya makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2025 kupitia Wizara ya Mambo ya Nje. 

Amesema zoezi hilo ni muendelezo wa ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Somalia, wenye lengo la kujenga kuwezesha serikali kufanya kazi kwa tija na kwa manufaa ya mataifa yote mawili.

Naye, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo kutoka Somalia, Ayan Andullahi ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo amejifunza kwa kina kuhusu namna Tanzania ilivyofanikiwa kujenga mifumo madhubuti ya utumishi wa umma inayozingatia uwajibikaji, uwazi na utoaji wa huduma ufanisi na kwa wakati.

Amesisitiza kuwa, uzoefu alioupata, hususan katika matumizi ya mifumo ya kidijitali na uratibu wa rasilimali watu utakuwa chachu ya mageuzi katika taasisi yao pindi watakaporejea nchini Somalia







Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wadau wa Sekta ya Afya pamoja na wageni mbalimbali kabla ya kufungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wadau wa Sekta ya Afya pamoja na wageni mbalimbali kabla ya kufungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili, 2026.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima ya Kibinadamu ya Upasuaji wa Ubongo kutoka kwa Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Tanzania (TNS) Dkt. Othman Kiloloma kwenye hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili, 2026.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima ya Kibinadamu ya Upasuaji wa Ubongo kutoka kwa Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Tanzania (TNS) Dkt. Othman Kiloloma kwenye hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili, 2026.
Wafanyakazi wa Sekta ya Afya wakiwa kwenye hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili, 2026.
Wadau wa Sekta ya Afya wakiwa kwenye hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili, 2026.


Na Mwandishi Wetu.

Chuo Kikuu cha Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS) kimeendelea kuthibitisha ubora wake katika utafiti baada ya watafiti wake kadhaa kuingia katika orodha ya wanasayansi 20 bora nchini kwa mujibu wa AD Scientific Index ya mwaka 2026.

Kwa mujibu wa tangazo rasmi la chuo hicho, Profesa Mecky Matee ameongoza kwa kushika nafasi ya kwanza kitaifa, akifuatiwa na marehemu Profesa Ferdinand Mugusi aliyeshika nafasi ya saba. Wengine ni Profesa Sylvia Kaaya (nafasi ya 13), Profesa Karim Manji (nafasi ya 14), Profesa Bruno Sungunya (nafasi ya 15), pamoja na Profesa Eligius Lyamuya aliyeshika nafasi ya 17.

MUHAS imesema mafanikio hayo yanaakisi mchango mkubwa wa chuo hicho katika tafiti za afya, ubunifu wa kisayansi pamoja na juhudi zake za kuimarisha huduma za afya kitaifa na kimataifa.

Aidha, chuo hicho kimetoa heshima maalum kwa marehemu Profesa Ferdinand Mugusi, kikieleza kuwa mchango wake katika tafiti na malezi ya wataalamu utaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya taaluma ya afya nchini.

Katika taarifa hiyo, MUHAS pia imewapongeza watafiti wengine wa chuo hicho waliotajwa katika viwango vya kitaifa, ikisisitiza kuwa juhudi zao zinaendelea kuimarisha hadhi ya taasisi hiyo katika jumuiya ya kitaaluma.

“Hongera sana kwa mafanikio haya makubwa, endeleeni kuinua kiwango,” ilisomeka sehemu ya ujumbe wa pongezi kutoka MUHAS.