Articles by "HABARI ZA BIASHARA"
Showing posts with label HABARI ZA BIASHARA. Show all posts
Mkuu wa Kitengo cha Mifumo Mbadala ya kidigitali wa Benki ya Exim Silas Matoi (Aliyekaa Kulia), akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo Exim WhatsApp Banking unaolenga kuwawezesha wateja wa Benki ya Exim kupata huduma mbalimbali za kibenki ikiwamo kuangalia salio, kuhamisha fedha, kutuma fedha kwenda mitandao ya simu, kulipia bili na huduma za serikali, pamoja na huduma zinazohusiana na kadi za benki kupitia kupitia WhatsApp. Huduma hii ni sehemu ya mikakati ya benki hiyo kuleta ubunifu unaoendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia pamoja na uhalisia wa maisha ya kila siku ya wateja. Aliyekaa kushoto ni Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza. Uzinduzi huo umefanyika Mei 21, 2026 katika za makao makuu ya Benki ya Exim jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM, Mei 21, 2026 — Benki ya Exim Tanzania hii leo imezindua huduma yake ya Exim WhatsApp Banking, suluhisho jipya la kidijitali lililobuniwa kufanya huduma za kibenki za kila siku kuwa za haraka, rahisi na zinazofikika kwa kupitia jukwaa la WhatsApp.

Huduma hii inawawezesha wateja kupata huduma mbalimbali za kibenki moja kwa moja kupitia WhatsApp. Huduma hizo ni pamoja na kuangalia salio, kuhamisha fedha, kutuma fedha kwenda simu za mkononi, kufanya malipo kwa wafanyabiashara, kulipia huduma za Serikali kupitia GePG pamoja na huduma zinazohusiana na kadi za benki. Mteja anaweza kupata huduma zote hizi kupitia jukwaa la WhatsApp bila uhitaji wa kupakua programu nyingine yoyote wala haja ya kutembelea tawi la benki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Kitengo cha Mifumo Mbadala ya Kidijitali wa Benki ya Exim, Bw. Silas Matoi, alisema mfumo huo umebuniwa kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki na kuimarisha ubora wa huduma kwa wateja.

“Kupitia Exim WhatsApp Banking, wateja wetu sasa wanaweza kuangalia salio kwenye akaunti zao, kutuma fedha kwenda kwenye mitandao ya simu, kulipa bili na malipo mbalimbali ya Serikali, kupata huduma zote zinazohusiana na kadi pamoja na kufanya miamala mingine moja kwa moja kupitia WhatsApp. Hii inaondoa ulazima wa aidha kupakua au kubadilisha programu mbalimbali au kupitia mifumo migumu, kwani sasa huduma zote muhimu za kibenki zinapatikana sehemu moja, iliyozoeleka, rahisi na inayopatikana kwa watu wote,” alisema Matoi.

Katika hatua nyingine, Matoi alieleza kuhusu ubora wa teknolojia iliyotumika kubuni mfumo huo na kutoa hakikisho kuhusu usalama wa huduma hiyo.
“Tumejenga suluhisho hili huku tukizingatia misingi ya usalama na urahisi wake. Wateja wetu wasiwe na wasiwasi, wanaweza kufanya miamala kwa kujiamini wakijua kuwa kila mawasiliano yanalindwa kupitia mifumo salama ya uthibitishaji ikiwemo uthibitisho wa PIN. Wakati huo huo, mfumo huu unasalia kuwa rahisi, wa haraka na mwepesi kutumia, kwa sababu lengo kubwa ni kufanya huduma za benki kidijitali ziwe za kawaida na zinazofikika kwa kila mteja,” aliongeza.

Huduma hii mpya ya Exim WhatsApp Banking inawawezesha wateja wa Benki ya Exim kufanya miamala yao ya kila siku kupitia jukwaa hilo wanalolitumia kila siku, hivyo kuondoa ulazima wa kupakua programu tofauti huku wakifurahia huduma za kibenki zilizo rahisi, za haraka na zilizozoeleka.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza, alisema kuanzishwa kwa huduma hiyo kunadhihirisha dhamira endelevu ya benki hiyo katika kuleta ubunifu na kuboresha huduma kwa wateja.

“Wateja wetu tayari wanatumia WhatsApp kila siku kwa mawasiliano yao, kufanya biashara na kusimamia shughuli zao za kila siku. Kwa kuleta huduma za benki ndani ya mazingira hayo hayo, tunafanya huduma za kifedha kuwa rahisi kufikiwa, kueleweka na kutumika kwa urahisi zaidi. Mteja wetu hapaswi kujifunza mfumo mpya au kupakua programu nyingine ili tu kuangalia salio lake au kulipa bili. Huduma za benki zinapaswa kufanyika kulingana na namna unavyoishi na kufanya kazi, na si vinginevyo,” alisema Kauthar.

Aliongeza kuwa uzinduzi huo ni sehemu ya mikakati mipana ya benki ya kuendelea kuleta ubunifu unaochochewa na mahitaji halisi ya wateja na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

“Tunazingatia namna wateja wetu wanavyoishi, tunaelewa mifumo na majukwaa wanayoyaamini, na kisha tunabuni suluhisho rahisi linaloendana na maisha yao ya kila siku. Huduma ya benki kupitia WhatsApp si tu njia mpya ya kutoa huduma, bali pia hatua inayodhihirisha kuwa Benki ya Exim ni benki inayokua sambamba na wateja wake, inayosikiliza mahitaji yao na kufanya maisha yao ya kifedha kuwa rahisi zaidi kila siku,” alisema.

Wateja wanaweza kupata huduma hii kwa kuanzisha mawasiliano kwa njia ya ujumbe kupitia namba rasmi ya WhatsApp ya Benki ya Exim Tanzania (+255 675 800 100), ambapo wataelekezwa kupitia mchakato rahisi wa usajili ikiwemo kuweka PIN kabla ya kuanza kutumia huduma mbalimbali zinazopatikana.

Benki ya Exim pia imeeleza kuwa ina mpango wa kupanua huduma hii kwa kuongeza vipengele vingine ikiwemo maombi ya mikopo na huduma za uwekezaji, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake endelevu wa mageuzi ya kidijitali.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Kampuni ya Puma Energy Tanzania imezindua rasmi mfumo wake mpya wa kidijitali wa PRIS unaowawezesha wateja kujikusanyia pointi wanaponunua mafuta, vilainishi na bidhaa mbalimbali katika vituo vyake vya huduma nchini.

Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam umeelezwa kuwa sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo wa kuboresha huduma kwa wateja na kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika sekta ya nishati.

Kupitia mfumo huo, wateja wataweza kupata zawadi mbalimbali ikiwemo bidhaa za matumizi ya nyumbani, chakula pamoja na punguzo la mafuta baada ya kukusanya kiwango maalumu cha pointi kupitia manunuzi yao ya kila siku.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba aliipongeza Puma Energy Tanzania kwa kuendelea kuboresha huduma zake kwa kutumia mifumo ya kidijitali.


Alisema uzinduzi wa PRIS unaendana na jitihada za serikali za kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kukuza uchumi wa kidijitali nchini.

“Ubunifu kama huu unaongeza thamani kwa wananchi kwa kuwawezesha kunufaika moja kwa moja na manunuzi yao kupitia mfumo wa pointi na zawadi,” alisema Makamba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah alisema mfumo huo umebuniwa kwa lengo la kuwaweka wateja katikati ya huduma zote zinazotolewa na kampuni hiyo.

“PRIS ni sehemu ya dhamira yetu ya kuendelea kutoa suluhisho zenye manufaa kwa Watanzania. Mfumo huu unabadilisha matumizi ya kila siku kuwa zawadi zenye thamani,” alisema Fatma.
 

Aliongeza kuwa mfumo huo pia unaunga mkono ajenda ya taifa ya mageuzi ya kidijitali kupitia Mfumo wa Kimkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa mwaka 2024–2034.

Naye Meneja Mauzo wa Puma Energy Tanzania, Sulpis Mmasi alisema programu hiyo imetengenezwa kwa urahisi ili iweze kutumiwa na watu wengi zaidi.
 Alisema wateja wanaweza kupakua programu hiyo, kujisajili kwa kutumia namba ya simu na kuanza kupata pointi mara moja kwa kuonyesha QR Code wanapofanya malipo katika vituo vya Puma.

“Zaidi ya zawadi, mfumo huu unatoa uzoefu wa kisasa unaomwezesha mteja kufuatilia matumizi yake kwa uwazi na urahisi,” alisema Mmasi.
 Kwa mujibu wa kampuni hiyo, mfumo wa PRIS tayari umefanikiwa katika baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Zimbabwe, Malawi na Botswana ambako umeongeza ushiriki wa wateja katika huduma za kampuni hiyo.

Aidha, Mkuu wa Idara ya Sheria na Mahusiano wa Puma Energy Tanzania, Emmanuel G. Bakilana aliwahimiza wananchi kupakua na kutumia programu hiyo ili kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa.

Puma Energy Tanzania ni ubia kati ya Puma Energy na Serikali ya Tanzania, huku kampuni hiyo ikiwa na vituo 95 vya mafuta, maduka 30 ya huduma pamoja na vituo vitano vya kuhifadhi mafuta nchini.



Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Serikali imeipongeza Benki ya CRDB Bank Plc kwa juhudi zake za kuhamasisha uwekezaji nchini kupitia elimu ya fedha, uwekezaji wa hisa na uwezeshaji wa kiuchumi unaolenga kuwajenga vijana kuwa wawekezaji wa baadaye.

Pongezi hizo zimetolewa jana jijini Arusha na Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar wakati akifungua Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB iliyofanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa 31 wa mwaka wa benki hiyo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Semina hiyo ilikuwa na kaulimbiu isemayo “Vijana na Uwekezaji kwenye Hisa” na iliwakutanisha viongozi wa serikali, wanahisa, wataalamu wa masoko ya mitaji pamoja na vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza katika semina hiyo, Waziri Omar alisema vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu katika umiliki wa uchumi kupitia uwekezaji badala ya kutegemea ajira pekee.

“Kaulimbiu ya mwaka huu imebeba ujumbe mkubwa wa kimkakati kwa taifa letu. Vijana hawapaswi kuishia kutafuta ajira pekee, bali wanastahili kushiriki katika umiliki wa uchumi kupitia uwekezaji,” alisema Waziri Omar.

Aidha, aliipongeza benki hiyo kwa hatua ya kufungua Ofisi ya Uwakilishi Dubai, akisema hatua hiyo imeongeza hadhi ya Tanzania katika sekta ya fedha na uwekezaji kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema benki hiyo itaendelea kuwawezesha vijana kupitia huduma za kifedha, ubunifu na programu za maendeleo ya ujasiriamali.

Alisema kupitia CRDB Bank Foundation na programu ya IMBEJU, maelfu ya vijana na wafanyabiashara wadogo wamefikiwa kwa mafunzo, mitaji na ushauri wa biashara.

“Tunaamini vijana wa leo si wateja tu wa benki yetu, bali ni wawekezaji, wabunifu na viongozi wa uchumi wa kesho,” alisema Dkt. Nsekela.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Neema Mori alisema uwekezaji katika hisa ni njia muhimu ya kujenga ustawi wa kifedha wa muda mrefu kwa vijana na familia za Kitanzania.

Profesa Mori alisema mafanikio ya Benki ya CRDB yanaonyesha namna uwekezaji wa muda mrefu unavyoweza kuleta matokeo chanya kwa wanahisa.

Alibainisha kuwa ndani ya miaka mitatu iliyopita thamani ya hisa za benki hiyo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 253, huku bei ya hisa ikifikia wastani wa Sh2,800 kutoka Sh460 mwaka 2023.

Aidha, alisema bodi ya wakurugenzi inapendekeza gawio la Sh90 kwa kila hisa kutokana na matokeo mazuri ya kifedha ya mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 38 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Profesa Mori aliwahamasisha wazazi kuanza kuwawekezea watoto wao hisa mapema ili kuwajengea msingi imara wa maisha ya kifedha ya baadaye.

Benki ya CRDB ni miongoni mwa taasisi kubwa za kifedha Afrika Mashariki na Kati, ikiwa na zaidi ya wateja milioni sita katika nchi za Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na ofisi ya uwakilishi Dubai, Falme za Kiarabu.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati akifungua Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB katika Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa, uliobeba kauli mbiu ya “Vijana na Uwekezaji kwenye Hisa”, semina inayofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), ambapo alitoa wito kwa Taasisi za Fedha nchini kupunguza riba na gharama nyingine za mikopo ili kuwawezesha wananchi wakiwemo vijana kupata mitaji ya kuwekeza kwenye shughuli zao za kiuchumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB katika Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa hao, uliobeba kauli mbiu ya “Vijana na Uwekezaji kwenye Hisa”, uliofunguliwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (hayupo pichani), uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori, akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB katika Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa hao, uliobeba kauli mbiu ya “Vijana na Uwekezaji kwenye Hisa”, uliofunguliwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (hayupo pichani), uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).









 
Na Godfrey Mushi

Waziri Mkuu nchini Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Jamhuri ya Ufaransa, Mheshimiwa Emmanuel Macron, Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Dkt. William Samoei Ruto pamoja na Mke wa Rais wa Kenya, Mama Rachel Ruto, wakati wa chakula cha jioni cha kitaifa kilichoandaliwa kwa heshima ya Wakuu wa Nchi na Serikali wanaoshiriki Mkutano wa Ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa (Africa Forward Summit: Africa–France Partnership for Innovation and Growth) unaofanyika jijini Nairobi, Kenya.


Rais wa Kenya, William Ruto, amempokea Rais wa Sierra Leone, Julius Maada Bio, katika Ikulu ya Nairobi kwa ziara rasmi inayohusiana na Mkutano wa Africa Forward unaotarajiwa kuanza leo Jumatatu Mei 11, 2026 nchini humo.

Akizungumza baada ya mazungumzo yao, Rais Ruto alisema Kenya na Sierra Leone zinaendelea kudumisha uhusiano wa karibu unaojengwa katika misingi ya kuheshimiana, umoja wa Afrika na kudumisha utulivu wa kikanda. Alieleza kuwa mataifa hayo mawili yataendelea kushirikiana katika kusukuma mbele ajenda za maendeleo ya bara la Afrika.

Ruto alisema nchi hizo pia zinashirikiana katika kuhimiza mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa, maboresho ya utawala wa dunia hususan katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pamoja na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Alibainisha kuwa mkutano wa Africa Forward utatoa jukwaa muhimu kwa viongozi wa Afrika kubadilishana mawazo kuhusu changamoto na fursa zinazolikabili bara hilo katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa duniani.

Katika mazungumzo hayo, Rais Ruto pia alimweleza Rais Bio kuhusu azma ya Kenya kugombea nafasi ya jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), ambapo alimwomba kuunga mkono mgombea wa Kenya, Jaji wa Mahakama ya Juu, Njoki Ndung'u.

Ziara hiyo ya Rais Bio nchini Kenya inaonekana kuimarisha zaidi ushirikiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili, huku viongozi hao wakisisitiza umuhimu wa mshikamano wa Afrika katika kutatua changamoto za bara hilo.

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde (wa pili kutoka kushoto), ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, akikata utepe wakati wa hafla ya ufunguzi rasmi wa tawi la Exim Bank Tanzania katika Mkoa wa Geita Region, akiwa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba (wa tatu kutoka kushoto). Pia pichani ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Exim Bank Tanzania, Bw. Jaffari Matundu (wa kwanza kutoka kushoto), pamoja na viongozi wengine wa Serikali na Benki ya Exim katika tukio hilo lilofanyika mnamo tarehe 09 May 2026, Geita.

Na Mwandishi Wetu.

Benki ya Exim Tanzania imezindua rasmi tawi lake jipya mkoani Geita ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupanua huduma za kifedha katika maeneo yenye shughuli kubwa za kiuchumi nchini. Tawi hilo linatarajiwa kuwahudumia wachimbaji wa madini, wakulima, wafanyabiashara wadogo na wa kati pamoja na wananchi wa kawaida.

Uzinduzi huo uliofanyika Mei 9, 2026, ulihudhuriwa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, viongozi wa Serikali, wadau wa sekta ya madini pamoja na wafanyabiashara mbalimbali wa mkoa huo. Waziri Mavunde alisema uwepo wa taasisi za kifedha kama Exim Bank utaongeza upatikanaji wa mitaji kwa wachimbaji na wafanyabiashara, hatua itakayosaidia kukuza uchumi wa wananchi wa Geita.

Alisema sekta ya madini inaendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania, hivyo uwekezaji wa huduma za kifedha katika maeneo ya uzalishaji utaongeza ufanisi na manufaa kwa Watanzania wengi zaidi. Aidha, alibainisha kuwa hatua hiyo inaendana na juhudi za Serikali za kuongeza ushiriki wa wananchi katika sekta ya madini.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania, Bw. Jaffari Matundu, alisema Geita ni moja ya maeneo muhimu yenye ukuaji mkubwa wa shughuli za kiuchumi zinazotegemea sekta ya madini pamoja na biashara zinazoiunga mkono. Alisema kupitia tawi hilo, benki inalenga kutoa huduma salama, za kisasa na zinazokidhi mahitaji ya wateja mbalimbali.

Aliongeza kuwa benki hiyo itaendelea kutoa suluhisho za kifedha zitakazochochea ukuaji wa biashara na kuongeza ushirikishwaji wa kifedha nchini. Matundu alisema jukumu la Exim Bank linaenda zaidi ya kutoa huduma za benki, bali kuwa mshirika wa maendeleo ya biashara na jamii.

Katika kuendeleza uwajibikaji kwa jamii kupitia programu ya Exim Cares, benki hiyo pia ilitoa msaada kwa Hospitali ya Manispaa ya Geita kusaidia kuboresha huduma za afya ya uzazi, watoto wachanga na huduma za dharura. Msaada huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma kwa wakati na kuboresha afya ya jamii.

Benki hiyo imeendelea kuimarisha mtandao wake wa huduma katika maeneo mbalimbali nchini sambamba na kuanzisha ushirikiano wa kimkakati na taasisi tofauti ili kurahisisha huduma za kifedha kwa wananchi na biashara. Hatua hiyo inaonyesha dhamira ya Exim Bank katika kuimarisha uchumi wa Tanzania kupitia ubunifu, uwekezaji na huduma bora za kifedha