Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Tanzania Plc, Joseph Sayi (katikati) akizungumza wakati wa kutangaza udhamini wa Mashindano ya Golf ya Vodacom Corporate Masters 2026, yaliyoandaliwa kwa ushirikiano na Lugalo Golf Club kwa lengo la kuunganisha jumuiya ya wafanyabiashara nchini Tanzania, kuimarisha mahusiano ya kibiashara, kukuza ushirikiano na kuleta fursa zenye tija kwa wateja, washirika wa kibiashara na wadau muhimu nchini. Mashindano hayo yatakayofanyika tarehe 1 Agosti 2026 yanaendelea kuimarisha nafasi ya Vodacom kama mshirika wa kuaminika katika teknolojia na huduma za mawasiliano kwa taasisi na mashirika yanayoendelea kukua katika mazingira ya uchumi wa kidijitali. Uzinduzi huo umefanyika tarehe 16 Julai 2026 jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Katibu wa Corporate Masters, Maryanne Mugo (kushoto) pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Corporate Masters, Ken Mbaya (kulia).

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Vodacom Tanzania PLC imezindua rasmi mashindano ya Vodacom Corporate Masters 2026 yatakayofanyika katika Uwanja wa Gofu wa Lugalo kuanzia Agosti 1, 2026, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uhusiano wa kibiashara, kukuza ushirikiano na kufungua fursa mpya kwa wateja, washirika na wadau wa sekta mbalimbali.

Mashindano hayo, yanayoandaliwa kwa kushirikiana na Oakwood Holdings Limited kupitia kitengo cha Vodacom Business, yatawakutanisha viongozi wa makampuni, wafanyabiashara, wataalamu wa sekta mbalimbali na wapenzi wa mchezo wa gofu kwa lengo la kujenga mitandao ya biashara na kubadilishana uzoefu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Tanzania PLC, Joseph Sayi, alisema kampuni hiyo imeendelea kudhamini mashindano hayo kwa mwaka wa tatu mfululizo kwa kuwa yanaendana na dhamira ya kuimarisha mahusiano ya muda mrefu na jumuiya ya wafanyabiashara.

Alisema mashindano hayo si ya michezo pekee, bali ni jukwaa linalowakutanisha viongozi wa biashara, wabunifu na watoa maamuzi ili kujadili fursa mpya za uwekezaji na kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali.

Sayi alisema katika kipindi chote cha mashindano hayo, Vodacom Business itaonesha suluhisho mbalimbali za kidijitali ikiwemo huduma za mawasiliano, usalama wa kidijitali na teknolojia za biashara zinazosaidia taasisi kuongeza ufanisi, kukuza biashara na kuimarisha ushindani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Corporate Masters, Ken Kariuki, alisema mashindano hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la makampuni kujitangaza, kujenga mitandao ya kibiashara na kuzalisha fursa mpya za biashara huku yakiimarisha ushiriki wa wateja.

Mashindano hayo yatashirikisha timu 10 za makampuni zitakazowania taji la Vodacom Corporate Masters 2026, sambamba na maonesho ya biashara, burudani, maonesho ya vitu vya kale na eneo maalumu la watoto, hatua inayolenga kuwafanya washiriki na familia zao kufurahia tukio hilo katika mazingira rafiki.

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: