Na Mwandishi Wetu, Accra, Ghana
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, amezitaka nchi za Afrika kuacha kutegemea matamko na ahadi zisizoambatana na utekelezaji, badala yake ziongeze uwekezaji wa ndani, uwajibikaji na matumizi ya ubunifu ili kuimarisha mifumo ya afya barani humo.
Dk. Kikwete alitoa kauli hiyo Julai 20, 2026, wakati akizungumza katika Mjadala wa Ngazi ya Juu wa Sera uliofanyika katika Hoteli ya Kempinski jijini Accra, Ghana, pembezoni mwa Mkutano Maalumu wa Umoja wa Afrika kuhusu Afya.
Mjadala huo uliwakutanisha mawaziri, watunga sera, taasisi za kikanda, washirika wa maendeleo, viongozi wa sekta binafsi na wataalamu wa afya kutoka mataifa mbalimbali, ukiandaliwa kwa ushirikiano kati ya African Renaissance Trust, Wakfu wa Jakaya Mrisho Kikwete, Tume ya Umoja wa Afrika na wadau wengine.
Akizungumza katika mkutano huo, Dk. Kikwete alisema utegemezi wa muda mrefu wa misaada ya nje katika kugharamia sekta ya afya hauwezi kuendelea kuwa msingi wa mifumo ya afya ya Afrika, hasa wakati misaada ya maendeleo inapopungua na mahitaji ya huduma bora za afya yakiongezeka.
Alisema bara hilo linapaswa kuongeza uwezo wa kugharamia huduma zake za afya kupitia mapato ya ndani, matumizi yenye ufanisi wa rasilimali na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.
“Ujumbe kutoka Eswatini hadi Accra ni mmoja; Afrika lazima igharamie, izalishe na ilinde mustakabali wake wa afya,” alisema.
Dk. Kikwete alikumbusha kuwa ni miaka 25 sasa tangu kupitishwa kwa Azimio la Abuja la mwaka 2001 lililozitaka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kutenga angalau asilimia 15 ya bajeti zao kwa sekta ya afya, lakini nchi nyingi bado hazijafikia lengo hilo.
Alisema hali hiyo imeendelea kuchangia mzigo mkubwa wa magonjwa kama UKIMWI, kifua kikuu, malaria, pamoja na vifo vinavyoweza kuzuilika vya wajawazito na watoto wachanga.
Katika hotuba yake, Dk. Kikwete alieleza kuwa usalama wa afya ya mama na mtoto unapaswa kuwa kipaumbele kikuu, akibainisha kuwa takribani wanawake 260,000 hufariki kila mwaka duniani kutokana na matatizo yanayohusiana na ujauzito na kujifungua, huku karibu asilimia 70 ya vifo hivyo vikirekodiwa barani Afrika.
Alisisitiza kuwa changamoto si ukosefu wa maarifa, dawa au teknolojia, bali ni kushindwa kuzifikisha huduma hizo kwa wananchi wanaozihitaji.
“Mama anaporudi nyumbani salama, ni kwa sababu fedha, ushahidi wa kisayansi na utoaji wa huduma vimefanikiwa kukutana,” alisema.
Akitoa mfano wa Tanzania, Dk. Kikwete alisema ushirikiano kati ya Wakfu wa Jakaya Mrisho Kikwete, Wizara ya Afya na taasisi za utafiti umechangia kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto kupitia tafiti na mikutano ya kisayansi inayofanyika kila baada ya miaka miwili.
Alisema juhudi hizo zimechangia kupungua kwa vifo vya wajawazito kutoka zaidi ya vifo 550 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa hai hadi vifo 104, hatua inayoiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kufikia lengo la Maendeleo Endelevu la kupunguza vifo hivyo hadi 70 ifikapo mwaka 2030.
Aidha, alisema mafanikio ya sekta ya afya hayapaswi kupimwa kwa kiwango cha fedha kinachotengwa pekee, bali kwa matokeo yanayowafikia wananchi.
“Swali si tunatumia kiasi gani katika afya. Swali ni kama uwekezaji wetu unawafikia wananchi wanaouhitaji zaidi,” alisema.
Katika mkutano huo pia ulizinduliwa mfumo wa African Renaissance Health Financing Insights Dashboard, utakaosaidia serikali kufuatilia ahadi za kifedha, matumizi ya bajeti, mapungufu ya fedha pamoja na matokeo ya uwekezaji katika sekta ya afya.
Dk. Kikwete alisema mfumo huo utasaidia kuimarisha uwajibikaji na ushirikiano kati ya wizara za afya na wizara za fedha ili kuhakikisha fedha zinazotengwa zinaleta matokeo yanayotarajiwa.
Pia alihimiza Afrika kupunguza utegemezi wa dawa na chanjo kutoka nje kwa kuwekeza katika uzalishaji wa ndani, kuimarisha Wakala wa Dawa wa Afrika na kutumia fursa za biashara ya kikanda kuimarisha usalama wa afya.
Katika mapendekezo yake, Dk. Kikwete aliwasilisha vipaumbele vitano ambavyo ni kuifanya afya kuwa uwekezaji wa kimkakati, kuongeza mapato ya ndani kupitia bima na kodi bunifu, kulinda huduma muhimu wakati misaada inapopungua, kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ushirikiano wa kikanda.
Kwa upande wake, Kamishna wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia Afya, Masuala ya Kibinadamu na Maendeleo ya Jamii, Balozi Amma Twum-Amoah, alisema mafanikio ya sera za afya yanapaswa kupimwa kwa maboresho yanayoonekana katika maisha ya wananchi.
Akihitimisha hotuba yake, Dk. Kikwete alisema Afrika haina upungufu wa mikakati wala ubunifu, bali changamoto iliyopo ni utekelezaji wa maamuzi yaliyokwishafikiwa.
“Tuondoke Accra tukiwa na dhamira ya kubadili ahadi kuwa bajeti, bajeti kuwa programu, programu kuwa matokeo yanayopimika, na matokeo kuwa maisha marefu, yenye afya na uzalishaji zaidi kwa wananchi tunaowahudumia,” alisema.




Toa Maoni Yako:
0 comments: