Rais wa Kenya, William Ruto, amempokea Rais wa Sierra Leone, Julius Maada Bio, katika Ikulu ya Nairobi kwa ziara rasmi inayohusiana na Mkutano wa Africa Forward unaotarajiwa kuanza leo Jumatatu Mei 11, 2026 nchini humo.

Akizungumza baada ya mazungumzo yao, Rais Ruto alisema Kenya na Sierra Leone zinaendelea kudumisha uhusiano wa karibu unaojengwa katika misingi ya kuheshimiana, umoja wa Afrika na kudumisha utulivu wa kikanda. Alieleza kuwa mataifa hayo mawili yataendelea kushirikiana katika kusukuma mbele ajenda za maendeleo ya bara la Afrika.

Ruto alisema nchi hizo pia zinashirikiana katika kuhimiza mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa, maboresho ya utawala wa dunia hususan katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pamoja na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Alibainisha kuwa mkutano wa Africa Forward utatoa jukwaa muhimu kwa viongozi wa Afrika kubadilishana mawazo kuhusu changamoto na fursa zinazolikabili bara hilo katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa duniani.

Katika mazungumzo hayo, Rais Ruto pia alimweleza Rais Bio kuhusu azma ya Kenya kugombea nafasi ya jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), ambapo alimwomba kuunga mkono mgombea wa Kenya, Jaji wa Mahakama ya Juu, Njoki Ndung'u.

Ziara hiyo ya Rais Bio nchini Kenya inaonekana kuimarisha zaidi ushirikiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili, huku viongozi hao wakisisitiza umuhimu wa mshikamano wa Afrika katika kutatua changamoto za bara hilo.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: