Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, John Ryoba, ametoa wito kwa madiwani kutumia fursa ya Chuo cha Furahika kupeleka vijana kupata mafunzo ya ufundi bure ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza katika mahafali ya wahitimu wa chuo hicho yaliyofanyika mwishoni mwa wiki, Ryoba alisema taasisi hiyo imekuwa mkombozi kwa vijana wengi waliokatisha masomo au kuishia kidato cha nne kutokana na changamoto mbalimbali.
Alisema mafunzo yanayotolewa chuoni hapo yanawawezesha vijana kupata ujuzi wa fani mbalimbali unaohitajika katika soko la ajira, huku akihimiza viongozi kuwabaini vijana wenye uhitaji na kuwapeleka chuoni hapo.

“Hiki ni chuo cha kipekee kinachotoa mafunzo bure, hivyo nawatoa wito madiwani wa Dar es Salaam na nchi nzima kuhakikisha wanawafikia vijana wenye mazingira magumu wapate elimu ya ufundi. Mimi katika Kata ya Kinyerezi nitaanza na wanafunzi 30,” alisema Ryoba.

Aidha, alisema juhudi hizo zinaunga mkono azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwezesha vijana kupata elimu na ujuzi wa vitendo unaowawezesha kujitegemea.

Katika hatua nyingine, Ryoba alitangaza kutoa ajira kwa mwanafunzi mmoja aliyefanya vizuri pamoja na kumlipia ada mwanafunzi mwingine ili kuendeleza masomo yake. Pia aliwahimiza wahitimu kuendelea kujifunza ili kufikia malengo makubwa maishani.
Naye mwakilishi wa Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mirambo Shabani, alisema chuo hicho kinatoa mchango mkubwa katika kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea, huku Kaimu Mkuu wa chuo, Dkt. David Msuya, akiwataka wahitimu kuepuka tabia zisizofaa na kujikita katika kazi ili kufanikisha ndoto zao.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: