Na Mwandishi Wetu
DAR
ES SALAAM — Taasisi ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) kwa
kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imezindua
rasmi kampeni ya kitaifa ya “Kutoa Ni Moyo” yenye lengo la kuchangisha
fedha na kuongeza uelewa kwa ajili ya kusaidia watoto wanaosumbuliwa na
magonjwa ya moyo nchini.
Kampeni
hiyo iliyozinduliwa Mei 25, 2026 jijini Dar es Salaam inalenga
kuwaunganisha Watanzania kutoka sehemu mbalimbali za jamii ili kuwapa
watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo nafasi ya kupata matibabu na
huduma muhimu za moyo.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge
alisema zaidi ya watoto 16,000 huzaliwa kila mwaka nchini Tanzania
wakiwa na matatizo ya moyo, hali inayozifanya familia nyingi kukumbana
na changamoto kubwa za kiafya na kifedha.
Alisema
takribani watoto 4,000 wanahitaji upasuaji wa moyo kwa haraka, huku
akibainisha kuwa kwa familia nyingi muda si suala la fedha pekee bali ni
suala la kuokoa maisha.
"Kupitia
kampeni ya Kutoa Ni Moyo, tunatoa wito kwa Watanzania wote, taasisi,
makampuni binafsi pamoja na taasisi za serikali kuwa sehemu ya harakati
hizi za kuokoa maisha ya watoto," alisema Dkt. Kisenge.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HTAF, Dkt. Naizihijwa Majani
alisema kampeni hiyo imekusudia si tu kukusanya fedha, bali pia kujenga
uelewa wa muda mrefu kuhusu afya ya moyo na umuhimu wa jamii kushiriki
kusaidia.
Alisema
Tanzania ina utamaduni mkubwa wa mshikamano na kusaidiana, hivyo
kampeni hiyo inalenga kubadili michango midogo ya wananchi kuwa nguvu
kubwa ya kitaifa yenye matokeo makubwa.
"Hii
si kampeni ya kuchangisha fedha pekee, ni harakati inayojengwa juu ya
huruma, umoja na imani kuwa kuokoa maisha ya mtoto ni jukumu la kila
mmoja wetu," alisema Dkt. Majani.
Takwimu
zinaonyesha kuwa magonjwa ya moyo husababisha vifo vya watu milioni
17.9 duniani kila mwaka, huku mtoto mmoja kati ya watoto 100 akizaliwa
akiwa na tatizo la moyo.
Kampeni
hiyo inalenga kukusanya shilingi bilioni 25 kupitia michango ya
wananchi, makampuni, wadau wa maendeleo, taasisi mbalimbali, Watanzania
waishio nje ya nchi, watu maarufu, jumuiya za michezo na jamii kwa
ujumla.

Fedha
zitakazokusanywa zitatumika kugharamia upasuaji na matibabu ya watoto
wenye matatizo ya moyo, uchunguzi wa mapema, programu za elimu ya afya
ya moyo pamoja na kusaidia familia zinazokabiliwa na changamoto hiyo.
Aidha,
kampeni hiyo itatumia mifumo ya kidijitali na majukwaa ya uchangishaji
mtandaoni ili kurahisisha Watanzania kuchangia kwa uwazi na urahisi
kutoka ndani na nje ya nchi.
Taarifa
zinaonyesha kuwa juhudi za awali za uchangishaji tayari zimefanikiwa
kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 3.08 kupitia fedha taslimu na
misaada ya vifaa mbalimbali.


Toa Maoni Yako:
0 comments: