Mkuu wa Kitengo cha Mifumo Mbadala ya kidigitali wa Benki ya Exim Silas Matoi (Aliyekaa Kulia), akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo Exim WhatsApp Banking unaolenga kuwawezesha wateja wa Benki ya Exim kupata huduma mbalimbali za kibenki ikiwamo kuangalia salio, kuhamisha fedha, kutuma fedha kwenda mitandao ya simu, kulipia bili na huduma za serikali, pamoja na huduma zinazohusiana na kadi za benki kupitia kupitia WhatsApp. Huduma hii ni sehemu ya mikakati ya benki hiyo kuleta ubunifu unaoendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia pamoja na uhalisia wa maisha ya kila siku ya wateja. Aliyekaa kushoto ni Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza. Uzinduzi huo umefanyika Mei 21, 2026 katika za makao makuu ya Benki ya Exim jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM, Mei 21, 2026 — Benki ya Exim Tanzania hii leo imezindua huduma yake ya Exim WhatsApp Banking, suluhisho jipya la kidijitali lililobuniwa kufanya huduma za kibenki za kila siku kuwa za haraka, rahisi na zinazofikika kwa kupitia jukwaa la WhatsApp.

Huduma hii inawawezesha wateja kupata huduma mbalimbali za kibenki moja kwa moja kupitia WhatsApp. Huduma hizo ni pamoja na kuangalia salio, kuhamisha fedha, kutuma fedha kwenda simu za mkononi, kufanya malipo kwa wafanyabiashara, kulipia huduma za Serikali kupitia GePG pamoja na huduma zinazohusiana na kadi za benki. Mteja anaweza kupata huduma zote hizi kupitia jukwaa la WhatsApp bila uhitaji wa kupakua programu nyingine yoyote wala haja ya kutembelea tawi la benki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Kitengo cha Mifumo Mbadala ya Kidijitali wa Benki ya Exim, Bw. Silas Matoi, alisema mfumo huo umebuniwa kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki na kuimarisha ubora wa huduma kwa wateja.

“Kupitia Exim WhatsApp Banking, wateja wetu sasa wanaweza kuangalia salio kwenye akaunti zao, kutuma fedha kwenda kwenye mitandao ya simu, kulipa bili na malipo mbalimbali ya Serikali, kupata huduma zote zinazohusiana na kadi pamoja na kufanya miamala mingine moja kwa moja kupitia WhatsApp. Hii inaondoa ulazima wa aidha kupakua au kubadilisha programu mbalimbali au kupitia mifumo migumu, kwani sasa huduma zote muhimu za kibenki zinapatikana sehemu moja, iliyozoeleka, rahisi na inayopatikana kwa watu wote,” alisema Matoi.

Katika hatua nyingine, Matoi alieleza kuhusu ubora wa teknolojia iliyotumika kubuni mfumo huo na kutoa hakikisho kuhusu usalama wa huduma hiyo.
“Tumejenga suluhisho hili huku tukizingatia misingi ya usalama na urahisi wake. Wateja wetu wasiwe na wasiwasi, wanaweza kufanya miamala kwa kujiamini wakijua kuwa kila mawasiliano yanalindwa kupitia mifumo salama ya uthibitishaji ikiwemo uthibitisho wa PIN. Wakati huo huo, mfumo huu unasalia kuwa rahisi, wa haraka na mwepesi kutumia, kwa sababu lengo kubwa ni kufanya huduma za benki kidijitali ziwe za kawaida na zinazofikika kwa kila mteja,” aliongeza.

Huduma hii mpya ya Exim WhatsApp Banking inawawezesha wateja wa Benki ya Exim kufanya miamala yao ya kila siku kupitia jukwaa hilo wanalolitumia kila siku, hivyo kuondoa ulazima wa kupakua programu tofauti huku wakifurahia huduma za kibenki zilizo rahisi, za haraka na zilizozoeleka.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza, alisema kuanzishwa kwa huduma hiyo kunadhihirisha dhamira endelevu ya benki hiyo katika kuleta ubunifu na kuboresha huduma kwa wateja.

“Wateja wetu tayari wanatumia WhatsApp kila siku kwa mawasiliano yao, kufanya biashara na kusimamia shughuli zao za kila siku. Kwa kuleta huduma za benki ndani ya mazingira hayo hayo, tunafanya huduma za kifedha kuwa rahisi kufikiwa, kueleweka na kutumika kwa urahisi zaidi. Mteja wetu hapaswi kujifunza mfumo mpya au kupakua programu nyingine ili tu kuangalia salio lake au kulipa bili. Huduma za benki zinapaswa kufanyika kulingana na namna unavyoishi na kufanya kazi, na si vinginevyo,” alisema Kauthar.

Aliongeza kuwa uzinduzi huo ni sehemu ya mikakati mipana ya benki ya kuendelea kuleta ubunifu unaochochewa na mahitaji halisi ya wateja na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

“Tunazingatia namna wateja wetu wanavyoishi, tunaelewa mifumo na majukwaa wanayoyaamini, na kisha tunabuni suluhisho rahisi linaloendana na maisha yao ya kila siku. Huduma ya benki kupitia WhatsApp si tu njia mpya ya kutoa huduma, bali pia hatua inayodhihirisha kuwa Benki ya Exim ni benki inayokua sambamba na wateja wake, inayosikiliza mahitaji yao na kufanya maisha yao ya kifedha kuwa rahisi zaidi kila siku,” alisema.

Wateja wanaweza kupata huduma hii kwa kuanzisha mawasiliano kwa njia ya ujumbe kupitia namba rasmi ya WhatsApp ya Benki ya Exim Tanzania (+255 675 800 100), ambapo wataelekezwa kupitia mchakato rahisi wa usajili ikiwemo kuweka PIN kabla ya kuanza kutumia huduma mbalimbali zinazopatikana.

Benki ya Exim pia imeeleza kuwa ina mpango wa kupanua huduma hii kwa kuongeza vipengele vingine ikiwemo maombi ya mikopo na huduma za uwekezaji, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake endelevu wa mageuzi ya kidijitali.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: