Katika maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani, Askofu Bagonza amegusa
hisia za wengi baada ya kuandika simulizi maalum kuhusu mama yake mzazi,
Dorothea Kagemulo Bagonza, akimtaja kama “Profesa Mnoa Viwango”
kutokana na malezi makali, yenye nidhamu na yaliyowajenga watoto wake
kuwa watu wenye uwajibikaji mkubwa katika maisha.Kupitia ujumbe wake, Askofu Bagonza alisema mama yake alikuwa mtu wa viwango vya juu sana katika kila jambo ndani ya familia, kiasi kwamba hakuna mtoto aliyewahi kufikia kiwango alichoweka. Alieleza kuwa hata kazi ndogo kama kupalilia, kuosha vyombo au kufanya usafi zilipaswa kufanywa kwa umakini mkubwa, vinginevyo mtoto alionekana hajafanya kazi ipasavyo.
“Ukimaliza kupalilia na ukajisikia umefanya kazi nzuri, yeye akija anakwambia umeparaza tu, hujapalilia,” aliandika Askofu huyo, akionyesha namna mama yake alivyosisitiza ubora na umakini katika kila kazi.
Aidha, alisema hata watoto walipofanya vizuri shuleni, mama yao hakuridhika kirahisi. Alisema mtoto angekuwa wa kwanza darasani lakini bado mama yao angewaambia darasa lenyewe huenda lilikuwa la wanafunzi dhaifu, hatua iliyowafanya watoto kujifunza kutoridhika na mafanikio madogo bali kuendelea kujituma zaidi.Katika simulizi hiyo, Askofu Bagonza alieleza kuwa mama yake alikuwa pia mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wanazingatia usafi, nidhamu na matumizi sahihi ya fedha. Alisema watoto walifundishwa kuokoa fedha badala ya kuzitumia hovyo, huku akiba zao zikikaguliwa kila mwezi.
Askofu huyo pia alikumbuka namna mama yake alivyosisitiza maadili ya dini na maisha ya kiroho. Alisema kwenda kanisani ilikuwa lazima kwa watoto wote, na kila mmoja alitakiwa kueleza kile alichojifunza baada ya ibada. Kwa mujibu wa Askofu Bagonza, jambo hilo liliwajenga watoto kuwa watu wenye nidhamu, uelewa na heshima kwa mafundisho ya dini.
Pamoja na ukali wake, Askofu Bagonza alisema mama yake alikuwa na upendo mkubwa kwa watoto wake na kila alichokifanya kilikuwa na lengo la kuwajenga kuwa watu bora katika jamii. Alimshukuru kwa malezi hayo, akisema yamechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio yao maishani.
“Huyo ndiyo mama. Happy Mother’s Day Ma Dorothea. Huna baya,” alihitimisha Askofu Bagonza katika ujumbe wake uliogusa hisia za watu wengi kwenye mitandao ya kijamii.





Toa Maoni Yako:
0 comments: