Na Mwandishi Wetu
DODOMA, Aprili 4, 2026 — Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza kuongeza muda wa kukamilisha kazi kwa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyochapishwa katika Gazeti la Serikali, Tume hiyo ilianza kazi zake tarehe 20 Novemba, 2025 na ilitarajiwa kukamilisha majukumu yake ndani ya kipindi cha siku 90. Hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali, Tume imeshindwa kukamilisha kazi ndani ya muda uliopangwa.
Imeelezwa kuwa sababu za kuongezwa kwa muda huo ni pamoja na haja ya kuhakikisha uchambuzi wa kina wa ushahidi, taarifa na maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wadau mbalimbali. Aidha, Tume imepewa fursa ya kuwashirikisha wataalamu wa uchunguzi wa kisaikolojia ili kufanikisha kazi zake kwa ufanisi zaidi.
Sababu nyingine ni kuendelea na maandalizi ya ripoti itakayowasilishwa kwa Mheshimiwa Rais pamoja na kutoa nafasi ya kufanya tathmini ya kina ya taarifa zote zilizokusanywa.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka husika imeidhinisha kuongezwa kwa muda wa siku ishirini na moja (21) ili kuruhusu Tume kukamilisha kazi zake ipasavyo kabla ya kuwasilisha ripoti ya mwisho.
Serikali imeendelea kuwahimiza wananchi kushirikiana na Tume kwa kutoa taarifa sahihi na kuendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Taarifa hiyo imetolewa rasmi na Mwenyekiti wa Tume tarehe 3 Aprili, 2026 jijini Dodoma.



Toa Maoni Yako:
0 comments: