Na Mohammed Hammie
Wakati masuala ya hedhi yakiendelea kuzungumzwa kwa sauti ya chini katika jamii nyingi, kijana mmoja kutoka kijiji cha Lipwidi mkoani Mtwara ameibuka kuwa sauti ya mabadiliko kwa kutoa elimu ya hedhi salama kwa wanawake, wasichana na wanaume.
Makungu Mrope (24), anayefahamika kwa jina la “Kaka wa Hedhi”, amesema ameamua kujitoa kuelimisha jamii ili kuondoa mtazamo kwamba hedhi ni suala la siri linalowahusu wanawake pekee.
Mrope amesema msukumo wa kufanya kazi hiyo ulianza tangu utotoni baada ya kushuhudia dada yake akipata hedhi akiwa shuleni na kudhalilishwa na wanafunzi wenzake.
“Walianza kumzomea na kuimba kuwa amechinja kuku. Ilikuwa aibu kubwa sana,” amesema.
Amesema tukio hilo lilimuumiza zaidi baada ya kuona dada yake akikosa kwenda shule kwa wiki nzima kutokana na fedheha aliyopata.
“Tukio lile liliniumiza sana. Ndipo nikaweka nia kwamba nitakapokuwa mkubwa nitaelimisha kuhusu hedhi salama ili wasichana wasipitie mateso kama yale,” amesema.
Baada ya kushindwa kuendelea na masomo ya juu ya sekondari, Mrope amesema alianza kujielimisha kupitia zahanati ya kijiji pamoja na machapisho ya Wizara ya Afya, kabla ya kuanza rasmi kutoa elimu kwa jamii.
Jitihada zake zilitambuliwa na uongozi wa kijiji cha Lipwidi ambao ulimpa kibali cha kuendesha shughuli hizo rasmi. Tangu hapo, amekuwa akitembelea shule mbalimbali kutoa elimu ya hedhi salama.
Amesema kila asubuhi hutembelea shule ya sekondari aliyosoma ambako hupata dakika 30 wakati wa gwaride la asubuhi kuzungumza na wanafunzi na kujibu maswali yao.
“Sifanyi kazi hii peke yangu. Mara nyingi nashirikiana na wataalamu wa afya kutoka zahanati ya kijiji,” amesema.
Mbali na kutoa elimu, Mrope pia hujihusisha na biashara ya kuuza nguo za kiume, huku dukani kwake pia zikipatikana taulo za kike (pedi). Amesema kila mnunuzi hupata pia maelekezo ya matumizi sahihi pamoja na umuhimu wa usafi wa hedhi.
Kwa mujibu wa Mrope, wanaume wana nafasi kubwa katika kubadili mtazamo wa jamii kuhusu hedhi kwa kusaidia kuondoa unyanyapaa na kuongeza uelewa sahihi wa afya ya uzazi.
“Ninapenda kuwaelimisha wanaume wenzangu kuhusu umuhimu wa hedhi kwa wanawake na wasichana. Wengi wameanza kubadilika,” amesema.
Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Hedhi kila mwaka Mei 28, juhudi za Mrope zinaendelea kuhamasisha jamii kuongeza uelewa, kuondoa aibu na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa salama vya hedhi kwa wasichana na wanawake.
Kupitia kazi hiyo, “Kaka wa Hedhi” ameendelea kuwa mfano wa mabadiliko katika jamii, akionesha kuwa elimu ya hedhi salama ni jukumu la kila mmoja bila kujali jinsia.



Toa Maoni Yako:
0 comments: